Taliban: Skuli za wasichana zimefunguliwa katika mikoa 10 ya Afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya muda ya Taliban Afghanistan amesema, skuli za wasichana katika ngazi zote zimefunguliwa katika mikoa kumi ya nchi hiyo.
Baada ya kushika hatamu za madaraka Agosti 15, 2021, kundi la Taliban lilizifunga skuli za wasichana katika ngazi ya kati na sekondari kwa lengo la kufanya baadhi ya marekebisho.
Mwaka wa masomo kwa skuli za Afghanistan huanza tarehe 24 Mei. Ilitazamiwa kuwa skuli za wasichana katika ngazi zote zingefunguliwa tena siku ya Jumanne baada ya kufungwa kwa miezi kadhaa.
Akizungumzia suala la masomo kwa watoto wa kike Afghanistan, Abdulqahar Balkhi msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya serikali ya muda ya Taliban amesema: skuli za elimu ya kati za serikali katika mikoa 10 kati ya 34 ya nchi hiyo zimefunguliwa katika ngazi zote.
Balkhi ameongeza kuwa, katika nchi nzima ya Afghanistan skuli za binafsi za wasichana kuanzia darasa la kwanza hadi ngazi ya chuo kikuu zimefunguliwa.
Kuhusu suala la wafanyakazi wanawake serikalini, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Taliban amebainisha kuwa, akthari ya wafanyakazi wanawake, ambao ni takribani laki moja na 20 elfu wamerejea makazini baada ya kuangushwa serikali iliyopita.
Balkhi ameeleza pia kwamba, wanawake wanafanya kazi katika sekta zote za binafsi nchini Afghaniustan zikiwemo za biashara, benki, ushoni na madukani na kusisitiza kuwa hakuna mipaka yoyote waliyowekea wanawake ya kutembea mijini.
Kudhamini haki za msingi za wanawake, kuzifungua skuli zote za wasichana, kutotumiwa ardhi ya Afghanistan dhidi ya nchi zingine na kuuda serikali pana na jumuishi ni miongoni mwa masharti yaliyotolewa na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuitambua serikali ya Taliban.../