Aug 05, 2022 01:14 UTC
  • Utafiti: Polisi ya Marekani imeua raia 700 ndani ya miezi 7

Mamia ya raia wameuawa na askari polisi wa Marekani tokea mwanzoni mwaka huu 2022 hadi sasa, huku duru mbalimbali zikiendelea kulaani ukatili wa polisi ya nchi hiyo dhidi ya raia hususan Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Utafiti wa kufuatilia mienendo ya polisi ya Marekani umefichua kuwa, raia zaidi ya 700 wameuawa katika miezi saba ya kwanza ya mwaka huu, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya mwaka tangu ufuatiliaji huo uanze kufanywa mwaka 2013.

Samuel Sinyangwe, muasisi wa taasisi ya kufuatilia mauaji yanayofanywa na polisi ya Marekani ya Mapping Police Violence amesema, iwapo mageuzi ya haraka hayatafanywa ili kuangazia mauaji hayo, watu wengine 440 watauawa mikononi mwa polisi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Utafiti wa taasisi hiyo imeeleza kuwa, uwezekano wa kuuawa Mmarekani mweusi ni mara tatu zaidi ikilinganishwa na Mmarekani mweupe katika miji mikubwa 48 kati ya 50 ya nchi hiyo.

Maandamano ya kulalamikia mauaji ya Wamarekani weusi

Kwa mujibu wa shirika la Mapping Police Violence, watu zaidi ya 2,500 wameuawa wakiwakimbia maafisa wa polisi ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka saba iliyopita, na kuna uwezekenao mkubwa wa idadi hiyo ikaongezeka zaidi katika miaka ijayo.

Mauaji ya Mmarekani mweusi, George Floyd tarehe 25 Mei mwaka 2020 yaliibua wimbi la malalamiko na maandamano ndani na nje ya nchi kupinga ukatili wa polisi ya Marekani, chini ya vuguvugu la 'Black Lives Matter'.

Tags