Aug 26, 2022 07:25 UTC
  • UN yataka dunia iwasaidie wakimbizi Waislamu wa Rohingya

Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuwasaidia kwa hali na mali wakimbizi Waislamu wa Rohingya walioko nchini Bangladesh.

Noeleen Heyzer alitoa mwito huo Alkhamisi usiku katika siku ya nne ya safari yake ya kuitembelea Bangladesh na kusisitiza kuwa, Wabangladesh wameendelea kuwa wakarimu kwa wakimbizi Warohingya, na kuna haja kwa nchi za dunia na hususan za eneo kuisaidia serikali ya Dhaka kubeba mzigo wa kushughulikia maslahi ya wakimbizi hao.

Ameeleza bayana kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kutafuta suluhu jumuishi, pana na ya kudumu ya mgogoro huo, na kwamba mgogoro huo katu haufai kusahaulika au kupuuzwa.

Mwito wa  Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umekuja siku chache baada ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Michelle Bachelet kusema hali bado haifai kwa wakimbizi Warohingya kurejea Myanmar.

Nyumba za Warohingya zilizochomwa moto Rakhine

Alisisitiza kuwa, bado si salama kwa karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Warohingywa waliowachache wanaoteswa kurejea katika nchi yao.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano tangu jeshi la Myanmar lifanye mauaji makubwa ya Warohingya katik jimbo la Rakhine, Bachelet alisafiri hadi Bangladesh Agosti 14  na wakati wa safari yake ya siku nne, alikutana na viongozi wa kidini na kutembelea maeneo kadhaa kwenye kambi ya Cox’s Bazar. 

Tags