Mashirika 290 yamtaka Biden asimamishe hujuma za Israel dhidi ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87716-mashirika_290_yamtaka_biden_asimamishe_hujuma_za_israel_dhidi_ya_palestina
Zaidi ya mashirika 290 ya Marekani na kimataifa yametoa mwito kwa Rais Joe Biden wa nchi hiyo yakimtaka achukue hatua za kivitendo za kuzuia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 02, 2022 07:33 UTC
  • Mashirika 290 yamtaka Biden asimamishe hujuma za Israel dhidi ya Palestina

Zaidi ya mashirika 290 ya Marekani na kimataifa yametoa mwito kwa Rais Joe Biden wa nchi hiyo yakimtaka achukue hatua za kivitendo za kuzuia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Palestina.

Katika barua yao kwa Biden, mashirika hayo yamemtaka rais huyo wa Marekani aandae mipango ya makusudi ya kukomesha hujuma za wanajeshi wa Israel dhidi ya asasi za kiraia za Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Barua hiyo imesema, licha ya sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa kulaani kitendo cha fedheha cha Israel cha kuyaweka mashirika ya kiraia ya Palestina katika orodha yake ya ugaidi, lakini Washington imesalia kimya na haijachukua hatua yoyote ya kupinga mchezo huo mchafu wa kisiasa wa Tel Aviv.

Utawala haramu wa Israel uliyataja mashirika sita ya kiraia ya Wapalestina kama makundi ya kigaidi Oktoba mwaka jana 2021, chini ya sheria yake tata ya eti Kupambana na Ugaidi.

Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wakilalamikia chokochoko za Israel

Mashirika hayo 290 ya kimataifa yamesema Washington imeenda mbali zaidi na kubatilisha visa halali ya mmoja wa viongozi wa mashirika hayo yaliyohujumiwa na Israel.

Yamesema hatua zilizochukuliwa na Marekani hazijakuwa na matokeo mengine, ghairi ya kuushajiisha utawala wa Tel Aviv kuendeleza na hata kushadidisha ukandamizaji wake dhidi ya Wapalestina.