Sep 04, 2022 03:38 UTC
  • Mzozo mpya wa Russia na Magharibi kuhusu nishati

Mawaziri wa fedha wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda duniani, zinazojulikana kama G7, walikubaliana Ijumaa, Septemba 2, katika mkutano uliofanyika kwa njia ya video, kuweka mipaka ya bei kwa mauzo ya mafuta ya Russia.

Katika taarifa yao, walitangaza kwamba wanakusudia kuweka vizuizi kwa usafirishaji wa baharini wa mafuta ghafi na bidhaa za mafuta za Russia, na kwamba wako tayari kuanza tena kuipa Russia huduma za usafirishaji wa mafuta kuelekea masoko ya kimataifa iwapo tu itazingatia mipaka hiyo ya bei iliyowekwa na nchi hizo. Mawaziri hao wa G7 wamesema wameanzisha mchakato maalumu ambao utahakikisha kwamba nchi zilizoko hatarini na ambazo zinategemea sana nishati ya Russia hazitadhurika na mabano hayo ya bei na kwamba kwa sasa zitaendelea kununua nishati kutoka masoko ya kimataifa likiwemo la Russia. Wakati huo huo wametaka kuongezwa uzalishaji wa mafuta na kukaribisha uamuzi wa OPEC wa kuongeza uzalishaji huo.

Washington imekaribisha hatua hiyo na kulezea matumaini yake kuwa itavuruga pakubwa mauzo ya mafuta ya Russia. Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen amesifu hatua hiyo ya G7 na kusema kupungua kwa bei ya nishati duniani na kunyimwa Putin fursa ya kunufaika na mapato ya mafuta kutampelekea apunguze makali yake katika vita vya Ukraine. Yellen ameendelea kusema kuwa ana hamu kubwa kuona hatua hiyo ya G7 ikitekelezwa kivitendo na kundi hilo pamoja na washirika wengine katika wiki zijazo. Amesema: "Jambo hilo bila shaka litaathiri uwezo wa Russia katika utekelezaji wa operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine na kuharakisha kuzorota kwa uchumi wake."

Kampuni ya nishati ya Russia Gazprom

Hatua hiyo ya G7, ambayo inalenga moja kwa moja kudhoofisha uchumi wa Russia na kupunguza mapato yake ya fedha za kigeni, imekabiliwa na majibu makali kutoka Moscow. Kabla ya mkutano wa kawaida wa G7, Dmitry Peskov, Msemaji wa Kremlin, alisema kwamba kuwekewa mipaka na vikwazo bei ya mafuta ya Russia kutavuruga utulivu wa bei katika soko la mafuta.

Katika kukabiliana na njama na uadui huo wa wateja wake wa Magharibi barani Ulaya, Russia imechukua hatua kadhaa. Kampuni ya Gazprom ya Russia ilitangaza Ijumaa kuwa kutokana na kuvuja kwa bomba la Nord Stream 1, usafirishaji wa gesi kupitia njia hiyo, ambayo ni mojawapo ya njia kuu za kusambaza gesi kwenda Ulaya, umesimamishwa kabisa. Usafirishaji wa gesi kwenda Ulaya kupitia bomba hilo utasitishwa hadi hitilafu ya vifaa itakapotatuliwa. Hivyo, bomba hilo muhimu la kupeleka gesi Ulaya limefungwa kwa muda usiojulikana.

Kabla ya hapo, ilisemekana kuwa usafirishaji wa gesi kupitia bomba hilo ungerejea katika hali yake ya kawaida kuanzia Jumamosi ya jana. Vyacheslav Volodin, Spika wa Duma ya Russia, amesisitiza kwamba vikwazo vya Magharibi dhidi ya nchi hiyo vimezisababishia matatizo ya nishati serikali za Magharibi na hasa Ulaya. Amesema: Usalama wa nishati kwa Ulaya hauwezi kupatikana bila Russia.

Kwa mtazamo wa Moscow, kuna machaguo mawili tu kwa nchi za Ulaya. Chaguo la kwanza ni kufuta vikwazo dhidi ya Russia na kuzindua bomba la gesi la Nord Stream 2, ambalo kwa hakika linakamilisha bomba la Nord Stream 1 na ambalo kwa sasa liko tayari kutumika. Bomba hilo halitumiki kwa sasa kutokana na hatua za kiuhasama za serikali ya Ujerumani. Chaguo la pili ni kuendelea na mbinu ya uhasana wa sasa dhidi ya Russia, ambalo bila shaka litasababisha kuongezeka kwa matatizo ya kiuchumi na hali ngumu zaidi ya maisha kwa raia wa nchi za Ulaya.

Bomba la gesi ya Russia la Nord Stream 2

Kwa maelezo hayo, inaonekana kwamba makabiliano na kwa kweli vita vya nishati kati ya Russia na Magharibi vimeingia katika awamu mpya, ambapo kila upande unatumia uwezo wake wote kwa lengo la kuudhuru upande wa pili. Hasa kambi ya Magharibi ambayo kupitia kundi la G7, imeyawekea mipaka ya bei mafuta ya Russia yanayouzwa nje ya nchi na kuamini kwamba jambo hilo litatoa pigo kali kwa uchumi wa nchi hiyo na shughuli zake za kijeshi huko Ukraine.

Kwa upande wake, Moscow nayo imezidisha shinikizo la gesi dhidi ya Ulaya. Hata hivyo, madhara ya vita hivyo vya nishati vinavyoendelea kwa viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma, hasa katika masuala ya gesi, yataziathiri zaidi nchi za Ulaya ambazo zinategemea sana gesi ya Russia, na ambazo zimekuwa na matarajio makubwa ya kudhaminiwa nishati ya gesi hasa katika kipindi kinachokaribia cha baridi kali, kwa ajili ya kuzalisha joto na umeme na kuendelea kwa shughuli zao za viwanda.

Tags