Sep 11, 2022 12:06 UTC
  • Maelfu waandamana Uingereza kulaani mauaji ya raia mweusi

Maelfu ya watu wamefanya maandamano katika mji mkuu wa Uingereza, London kulaani mauaji ya mtu mmoja mwenye asili ya Afrika yaliyofanywa na askari polisi wa nchi hiyo.

Waandamanaji hao wamekusanyika katika Medani ya Bunge kabla ya kuandamana katika barabara ya Whitehall katikati ya London, na kisha wakakusanyika katika ofisi za shirika la ujasusi la Scotland Yard.

Wamesikika wapiga nara za kulaani mauaji ya raia huyo mwenye asili ya Afrika aliyetambulika kwa jina la Chris Kaba. Baadhi yao walikuwa wamebeba mabango yenye picha na jina la raia huyo mweusi aliyeuliwa na polisi wa London.

Waandamanaji wengine walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe zisemazo: "Haki kwa Chris Kaba", "Bila uadilifu, hakuna amani" na "Maisha ya watu weusi yana thamani."

Mmoja wa maelfu ya waandamanaji amenukuliwa akisema, "Chris ana mama, familia, ndugu, marafiki na watu waliomfahamu na ambao hivi sasa wameshindwa kuvumilia machungu ya kuuawa kwake."

Maelfu waandamana Uingereza kulaani mauaji ya raia mweusi

Maandamano hayo makubwa ya kulaani wimbi la mauaji ya kiholela yanayofanywa na polisi wa Uingereza dhidi ya wageni hususan raia weusi ulidhaniwa kuwa ni mkusanyiko wa kumuomboleza Malkia Elizabeth wa Pili aliyeaga dunia siku chache zilizopita.

Ripoti ya vyombo vya habari inaonesha kuwa, mauaji ya watu weusi nchini Uingereza hivi sasa yameongezeka kwa kiwango cha kutisha tokea mwaka 2002. Raia 105 wenye asili ya Afrika waliuawa nchini humo mwaka 2020 pekee.

 

 

Tags