Uswisi yatangaza itakapozika taka zake za nyuklia maelfu ya miaka ijayo
(last modified Tue, 13 Sep 2022 08:13:37 GMT )
Sep 13, 2022 08:13 UTC
  • Uswisi yatangaza itakapozika taka zake za nyuklia maelfu ya miaka ijayo

Serikali ya Uswisi imetangaza kuwa imepata mahali ambapo itaweza kuzika taka za nyuklia chini ya ardhi kwa mamia ya maelfu ya miaka ijayo.

Baada ya tukio la nyuklia katika kinu cha Fukushima huko Japan mwaka 2011, Uswisi iliamua kuzima taratibu vinu vyake vya nyuklia.  

Hii ni katika hali ambayo baada ya kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mauzo ya gesi ya Russia tangu kuanza  vita nchini Ukraine mnamo Februari 24, Uswisi imetaka kuzidishwa uzalishaji wa nishati kutoka katika vinu vya nyuklia pamoja na vyanzo vipya vya usambazaji wa nishati ya gesi na mafuta. 

Serikali ya Uswisi imetangaza kuwa imepata eneo zuri kaskazini mwa  Zurich na karibu na mpaka wa Ujerumani kwa ajili ya kuzika taka zake za nyuklia  kwa mamia ya maelfu ya miaka ijayo. Gharama za eneo hilo kwa ajili ya kuzikia taka hizo za nyuklia kwa angalau miaka elfu 200 ijayo imekadiriwa kuwa faranga za Kiswisi bilioni 20 sawa na dola bilioni 20 na milioni 940. Kazi ya uzikaji taka hizo za nyuklia imepangwa kuanza mwaka 2050. 

Mahali Uswisi itakapozika taka zake za nuklia karibu na Zurich 

Kampuni ya kundi la Nagra inayondesha mradi wa utupaji taka za nyuklia ambayo ina uhusiano na kampuni zinazoendesha vinu vya nyuklia na seirikali ya Uswisi baada ya kufanya uchunguzi na tathmini kwa miaka 14 imeeleza kuwa, udongo wa eneo hilo unafaa katika uwanja huo ikilinganishwa na maeneo mengine mawili waliyoyatafiti awali.  

Kampuni ya Nagra mwishoni mwa mwaka 2024 inatazamia kuomba serikali kibali ili kutekeleza zoezi hilo la kuzika taka kutoka katika vinu vinne vya nguvu za nyuklia huko Uswisi.