Marekani kuiwekea vikwazo China ili 'kuzuia' kuvamiwa Taiwan
Marekani imeripotiwa kuwa inatafakari kuiwekea China vikwazo ili kuzuia eti mashambulizi tarajiwa ya kijeshi ya Beijing dhidi ya kisiwa cha Taiwan.
Shirika la habari la Reuters limenukuu vyanzo vilivyokaribu na kadhia hiyo na kueleza kuwa, Marekani na Umoja wa Ulaya zinatathmini suala la kuiwekea China vikwazo, ili kuizuia kutwaa Taipei kwa nguvu.
Tayari nchi hizo za Magharibi zimeiwekea China vikwazo shadidi, na katika mpango huo mpya zinataka kupanua mashinikizo hayo ya kiuchumi, na kuzuia kabisa nchi za dunia kufanya biashara au kuwekeza na Beijing katika masuala hasasi ya kitenolojia kama hifadhi ndogo za tarakilishi (microchip) na suhula za mawasiliano.
Serikali ya Beijing inasisitiza kuwa, Taipei sharti iunganishwe na ardhi kuu ya China, hata kama ni kwa kutumia nguvu za kijeshi. Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China, na imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taiwan; na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo.

Hivi karibuni, Marekani ilipeleka meli zake mbili za kivita kwenye Lango Bahari la Taiwan katika safari ya kwanza ya kichokozi kama hiyo tangu ziara yenye utata ya Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi huko Taiwan.
Siku chache zilizopita, China ilikosoa vikali mpango mpya wa serikali ya Marekani wa kuiuzia Taiwan silaha zenye thamani ya dola bilioni 1.1, ikisisitiza kuwa mawasiliano yoyote ya kijeshi na Taipei ni ukiukaji wa kanuni ya "China Moja".