Kuongezeka hitilafu kati ya Marekani na Saudi Arabia
(last modified Mon, 10 Oct 2022 09:18:01 GMT )
Oct 10, 2022 09:18 UTC
  • Kuongezeka hitilafu kati ya Marekani na Saudi Arabia

Kundi la wabunge wa chama cha Democratic cha Marekani wametaka kuondolewa wanajeshi wa nchi hiyo kutoka Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, kwa jina jingine Imarati, kufuatia uamuzi wa kundi la OPEC-Plus kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa milioni 2 kwa siku.

Uamuzi huo umefikiwa licha ya mashinikizo ya Marekani na mataifa mengine ya Magharibi ya kutaka uzalishaji zaidi wa mafuta ufanyike, jambo ambalo limepunguza kiwango cha mafuta katika soko ambalo tayari linakabiliwa na hali ngumu. Tom Malinowski kutoka jimbo la New Jersey, Sean Casten kutoka jimbo la Illinois na Susan Wild kutoka jimbo la Pennsylvania hivi karibuni waliwasilisha mswada wa sheria ambao unalenga kuondolewa majeshi yote ya Marekani kutoka Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu na vile vile kuondolewa katika nchi hizo mifumo ya makombora ya Patriot na Thaad. Wabunge hao wa chama cha Democratic wametoa taarifa wakisema: Uzalishaji wa mafuta umepunguzwa sana na Saudi Arabia na Imarati, katika hali ambayo Rais Biden katika miezi ya hivi karibuni alizitaka nchi zote mbili kujiepusha na jambo hilo, kitendo ambacho kinaonyesha chuki ya wazi dhidi ya Marekani na ni ishara tosha kwamba hizo zinaunga mkono Russia katika vita vyake dhidi ya Ukraine.

Hatua ya wabunge wa chama cha Democratic katika Bunge la Congress ya Marekani kwa hakika inaonyesha kukasirishwa Washington na hatua ya Riyadh ya kupuuza matakwa ya Marekani kwa OPEC-Plus kwa ajili ya kutopunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa milioni 2, ambapo Saudi Arabia ni miongoni mwa wanachama wenye ushawishi mkubwa katika kundi hilo. Kwa kuzingatia kukaribia uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Marekani ambao umepangwa kufanyika  Novemba 2022, hatua hiyo ambayo kwa hakika itaongeza bei ya nishati na hasa petroli nchini Merika, imetoa pigo kubwa la kisiasa kwa wabunge wa chama cha Democratic na Rais Joe Biden wa Marekani, suala ambalo bila shaka litapelekea baadhi ya wabunge hao kupoteza viti vyao katika Congress.

OPEC-Plus

Kufuatia ushirikiano wa Saudi Arabia na Russia katika kupunguza uzalishaji wa mafuta ndani ya mfumo wa OPEC-Plus, Seneta Bernie Sanders wa Marekani ameitaja Riyadh kuwa mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani na kutaka kuondolewa vikosi vyote vya kijeshi vya Marekani nchini humo na kupigwa marufuku nchi hiyo ya Kiarabu kuuziwa silaha na zana za kijeshi za Marekani.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, utawala wa Saudia unafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kufunika tofauti na pengo lililojitokeza kati ya Washington na Riyadh na kulifanya jambo hilo kutokuwa na umuhimu mkubwa. Kuhusiana na suala hilo, Adel al-Jubeir, Waziri Mshauri katika Masuala ya Kigeni wa Saudi Arabia amejibu ukosoaji huo wa maafisa wa Marekani kuhusiana na uamuzi wa hivi karibuni wa OPEC-Plus kwa kusema kuwa uhusiano kati ya Marekani na Riyadh ni wa kistratijia na kuwa umejengeka katika msingi wa ushirikiano na muungano. Ameendelea kusema kuwa fikra kwamba Saudi Arabia imepunguza uzalishaji mafuta kwa lengo la kuidhuru Marekani haina ukweli wowote.

Licha ya uhalalishaji huo, ukweli unaodhihiri wazi ni hamu ya Riyadh ya kushirikiana na Russia katika suala zima la kuainisha sera za mafuta, ikiwa ni pamoja na kupunguza au kuongeza uzalishaji na uuzaji wa mafuta nje ya nchi kwa mujibu wa mahitaji ya soko la kimataifa. Suala hilo pamoja na kupanuka kusiko kwa kawaida kwa uhusiano wa Saudi Arabia na China, kunaonyesha kuwa Riyadh inafuatilia uhusiano wa muda mrefu na wapinzani wa kimataifa wa Merikani yaani Russia na China, kwa kuzingatia uhusiano wake baridi wa hivi sasa na Washington hasa katika kipindi hiki cha serikali ya Biden. Suala hilo halijafichika machoni pa viongozi na wabunge wa Marekani.

Suala jingine ni kwamba sasa serikali ya Biden inalazimika kutoa akiba zaidi ya kimkakati ya mafuta ili kukabiliana na uhaba wa mafuta katika masoko ya kimataifa, ambao bila shaka utasababisha kuongezeka kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu. Katika jitihada za kupunguza bei ya mafuta, Joe Biden hivi karibuni aliamuru kutolewa kiasi kikubwa cha mafuta kutoka hifadhi ya kimkakati ya Marekani cha takriban mapipa milioni 180 kwa muda wa miezi sita. Ikulu ya White House tayari imetangaza mipango ya kutoa mapipa milioni 10 zaidi ya mafuta ifikapo mwezi Novemba.

Hifadhi ya nishati ya kimkakati

Hali hiyo imepelekea kupungua zaidi kwa akiba ya kimkakati ya mafuta ya nchi hiyo, jambo ambalo lilikuwa halijawahi kuonekana tena katika kipindi cha miaka 38 iliyopita. Aidha, wiki hii, Biden ameitaka seriakli yake na pia Congress kutafuta njia za kuongeza uzalishaji wa nishati ya Marekani na kupunguza udhibiti wa OPEC katika kuainisha bei ya mafuta. Baadhi ya machaguo aliyonayo Biden kwa sasa ni kuendelea kutumia akiba ya kimkakati ya mafuta au kuchunguza njia za kuyazuia mashirika ya mafuta ya Marekani kuuza nje bidhaa hiyo. Hata hivyo, ni wazi kuwa njia hizo hazitaweza kuzuia kuongezeka kwa bei ya nishati nchini humo. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa mwelekeo wa mafuta duniani hautakuwa kama inavyotaka Washington, suala ambalo kwa hakika ni dalili nyingine ya wazi ya kupungua ushawishi wa Marekani katika ngazi za kimataifa.