Putin: NATO inaingilia mambo ya ndani ya mataifa mengi duniani
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa, jeshi la nchi za Magharibi NATO linaingilia mambo ya ndani ya nchi nyingi duniani kinyume cha sheria.
Televisheni ya Russia Today imemnukuu Rais Putin akisema hayo katika kikao cha nchi wanachama wa "Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Barani Asia" (CICA) huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan na kuongeza kuwa, kunahitajika hatua ya pamoja ya kimataifa ya kukabiliana na uingiliaji wa NATO katika masuala ya ndani ya mataifa mengi duniani.
Kwa upande wake, Alexander Venediktov, Naibu wa Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ameliambia shirika la habari la TASS kwamba Moscow inakaribisha juhudi za kuutatua kidiplomasia mgogoro wa Ukraine kwa sharti la kulindwa usalama wa Russia. Amesisitiza kuwa, ombi la Kyiv la kutaka kuungwa na NATO halikubaliki kabisa na kuna hatari likazusha Vita vya Tatu vya Dunia.
Kabla ya hapo pia, msemaji wa Rais Vladimiri Putin wa Russia alikuwa ametangaza kuwa, Katibu Mkuu wa Jeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) amekiri kupitia matamshi yake kuwa muungano huo unapigana vita dhidi ya Russia huko Ukraine.
Dmitry Peskov amesema, matamshi ya Jens Stotenberg Katibu Mkuu wa Nato kuhusu vita huko Ukraine yanadhihirisha kushiriki kikamilifu NATO nchi nchi za Magharibi katika vita vya Ukraine.
Stoltenberg alisema juzi Jumanne wakati wa kikao cha Mawaziri wa Jeshi la Nchi za Magharibi Nato huko Brussels kwamba: ushindi wa Russia katika vita hivyo si pigo kubwa kwa raia wa Ukraine pekee bali litakuwa pigo na kitendo cha hatari kwa nchi zote za Magharibi."