Berlusconi amlaumu Rais Zelensky kwa vita vya Ukraine
Waziri Mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi amesema Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine ndiye aliyemsukuma kwenye vita Rais Vladimir Putin wa Russia.
Shirika la habari la LaPresse la Italia limevujisha sauti ya Berlusconi akiwaambia Wabunge wa nchi hiyo ya Italia kuwa, "Putin hakutaka kuingia vitani, lakini alisukumwa kufanya hivyo kutokana na Ukraine kuendelea kufanya mashambulizi mtawalia dhidi watu wanaotaka kujitenga katika eneo la Donbas."
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo wa Italia mwenye miaka 86, baada ya Zelensky kuchaguliwa kuwa rais mnamo Aprili mwaka jana, alishadidisha mara tatu mashambulizi dhidi ya maeneo yanayotaka kujitenga na Ukraine, na kwa msingi huo akawa ameisukuma ukutani Russia na kuilazimisha ingie katika vita visivyokuwa na mwisho.
Haya yanaripotiwa siku chache baada ya kura ya maoni ya kutaka kujiunga na Russia maeneo manne ya mkoa wa Donbas ulioko mashariki mwa Ukraine kufanyika.
Kulingana na matokeo rasmi ya kura hiyo iliyofanyika kuanzia Septemba 23 hadi 27, 99.23% ya wapiga kura katika Jamhuri ya Watu wa Donetsk, 98.42% katika Jamhuri ya Watu wa Luhansk, 93.11% katika mkoa wa Zaporizhia na 87.05% ya wakazi wa mkoa wa Kherson waliunga mkono maeneo yao yawe sehemu ya Shirikisho la Russia.
Tarehe 30 Septemba, Rais Vladimir Putin wa Russia alisaini katika hafla maalumu, mikataba ya kuyaunganisha maeneo hayo ya Ukraine na ardhi ya nchi hiyo.