Russia: Tuko tayari kuimarisha uhusiano na Arab League
Rais wa Russia amesisitiza kuwa Moscow iko tayari kuimarisha uhusiano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League). Rais Vladimir Putin ameeleza hayo katika kukaribia mkutano wa Arab League huko Algeria.
Rais Vladimir Putin jana aliwatumia ujumbe viongozi wa nchi za Kiarabu wanaoshiriki katika Mkutano wa 31 wa Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kueleza kuwa: Moscow iko tayari kuimarisha uhusiano na jumuiya hiyo ili kudhamini usalama wa kikanda na kimataifa.
Wakati huo huo Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisisitiza katika mazungumzo na Ahmed Aboul Gheit Katibu Mkuu wa Arab League juu ya hamu ya Russia na jumuiya hiyo ya kutatua hali ya mgogoro Asia Magharibi na kaskazini mwa Afrika na kuboresha usalama na hali ya uthabiti katika eneo.
Hivi karibuni pia Lavrov alikutana na kufanya mazungumzo na Hussein Ibrahim Taha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) na kueleza kuwa: Russia imeliweka suala la kuimarisha ushirikiano na nchi za Kiislamu za vipaumbele vya siasa zake za nje.
Mkutano wa 31 wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi za Kiarabu umeanza tangu jana huko Algiers mji mkuu wa Algeria. Ajenda kuu za mkutano huo zinahusiana na masuala ya dharura ya kikanda ikiwemo hali ya mgogoro huko Yemen, Libya na Russia, kadhia ya Palestina na pia njia za kudhamini usalama wa chakula na kuimarisha uhusiano miongoni mwa nchi za Kiarabu.