Mtetemeko wa ardhi waua watu 162 nchini Indonesia
(last modified Tue, 22 Nov 2022 02:37:43 GMT )
Nov 22, 2022 02:37 UTC
  • Mtetemeko wa ardhi waua watu 162 nchini Indonesia

Watu zaidi ya 160 wanaripotiwa kupoteza maisha nchini Indonesia baada ya kutokea mtetemeko wa ardhi katika eneo la Cianjur, mkoa wa Java Magharibi.

Mamlaka za Indonesia zimesema tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 5.6 kwa kipimo cha rishta lilitokea jana Jumatatu, na kusababisha watu zaidi ya 700 kujeruhiwa.

Habari zaidi zinasema kuwa, watu wengine 13,000 wamebaki bila makazi baada ya tetemeko hilo kusababisha hasara katika eneo hilo, na kukata mawasiliano na kuharibu miundombinu.

Tetemeko hilo limehisika katika mji mkuu Jakarta na maeneo mengine ya nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia, kama vile Rancaekek, South Tangerang, na Depok.

Maafisa wa Idara ya Kupambana na Majanga ya Indonesia wamesema juhudi za uokoaji na kutafuta miili ya waliofariki dunia katika tukio hilo la kimaumbile zingali zinaendelea. 

Athari za zilzala iliyotokea Indonesia

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, akthari ya maeneo ya visiwani nchini Indonesia yamekuwa yakishuhudia mitetemeko ya ardhi yenye kusababisha maafa mara kwa mara.

Mwaka 2004 zilzala ya chini ya maji ilitokea katika Bahari Hindi na kusababisha Tsunami katika nchi kadhaa huku Indonesia ikiathiriwa zaidi.

Aidha watu wasiopungua 170,000 walifariki dunia kwenye janga hilo la kimaumbile nchini Indonesia hususan katika mkoa wa Aceh, kaskazini mwa nchi.