Maelfu ya wahajiri wamepigwa na kudhalilishwa katika mipaka ya EU
Ripoti mpya iliyotolewa na shirika moja la kutetea haki za binadamu imefichua kuwa, maelfu ya wahajiri walipewa kichapo cha mbwa, baadhi wakadhalilishwa na wengine wakazuiliwa kinyume cha sheria kabla ya kurejeshwa waliokotoka na askari wa mipaka ya nchi za Umoja wa Ulaya.
Ripoti hiyo iliyopewa anuani ya 'Kitabu Cheusi cha Kurejeshwa Nyuma 2022' imekusanya mamia ya kesi za wahajiri wakiwemo wanawake na watoto wadogo kufanyiwa vitendo vya kinyama na askari wa ulinzi wa mipaka ya EU ndani ya miaka 2 iliyopita, kabla ya kufukuzwa na kulazimishwa kurejea walikotoka.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo yenye kurasa 3,173 ya shirika linalofuatilia jinai dhidi ya wahajiri mipaka la 'Border Violence Monitoring Network' walinzi hao wa mipaka ya EU wanatumia mbinu za kikatili kuzuia wahajiri kuingia katika nchi za bara Ulaya.
Baadhi ya mbinu hizo, kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo ya haki za binadamu, ni vichapo vikali vya muda mrefu, kuvuliwa nguo kwa lazima, kunajisiwa, kunyolewa (kichwa) kwa lazima, kupigwa shoti na vifaa vya umeme, na hata kuzuiliwa kwa kipindi kirefu katika mazingira ya kuogofya.
Ripoti hiyo iliyokusanya ushahidi na simulizi za wahajiri zaidi ya 700 inaeleza kuwa, baadhi ya walinzi wa mipaka ya nchi za EU mbali na kuwatukana na kuwadhalilisha wahajiri, lakini pia wanaachia mbwa wawashambulie wahamiaji hao.
Ripoti hiyo imezikosoa vikali nchi wanachama wa EU za Poland, Lithuania na Latvia kwa kupasisha sheria zinazohalalisha kutumia mbinu hizo za kikatili kuwarejesha nyuma wahajiri.
Ripoti hiyo imetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za kisheria waliohusika na ukatili huo dhidi ya wahajiri kwa kutumia mbinu za kinyama, sanjari na kuitaka EU iwakumbatie wahajiri pasi na ubaguzi au kujali utaifa wao.