Austria, nchi ya EU yashuhudia ongezeko la wasiojua kusoma, kuandika
(last modified Sun, 01 Jun 2025 07:05:21 GMT )
Jun 01, 2025 07:05 UTC
  • Austria, nchi ya EU yashuhudia ongezeko la wasiojua kusoma, kuandika

Karibu thuluthi moja ya watu nchini Austria wana uwezo mdogo wa kusoma, jambo linaloashiria ongezeko la kuogofya la watu wasiojua kusoma na kuandika nchini humo, ofisi ya takwimu za serikali ya nchi hiyo ya Umoja wa Ulaya imesema.

Kupungua huko kwa uwezo wa kusoma na kuandika kunaonekana haswa miongoni mwa wale walio na kazi zinazohitaji sifa za kati au za chini, Shirika la Takwimu la Austria lilisema katika taarifa yake ya karibuni.

Nchini Austria, nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya ambayo ina jamii ya watu milioni tisa, asilimia 29 au karibu watu milioni 2.6 wana kiwango cha chini cha kusoma na kuandika, kwa mujibu wa data kwenye tovuti ya shirika hilo.

Aidha kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya watu walio na matatizo ya kusoma iliongezeka kwa asilimia 11.9 kati ya mwaka 2012 na 2023.

Kiwango cha wastani cha kusoma na kuandika miongoni mwa Waaustria wenye umri wa miaka 16 hadi 65 ni pointi 254, ambayo ni chini sana ya wastani wa pointi 260 zilizowekwa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD).

Watu kati ya miaka 16 hadi 24 wapo juu ya wastani wa vigezo vya OECD, huku wazee wakionekana kuwa na ujuzi wa chini wa kusoma kuliko kiwango kinachotarajiwa, shirika hilo lilisema.

Kwa mujibu wa Shirika la Takwimu la Austria, idadi ya watu walio na ujuzi mdogo wa kufanya hesabu nyepesi za kila siku pia iliongezeka kwa asilimia 6.7 kati ya 2012 na 2023, ambayo ni sawa na asilimia 22.6 ya watu wote.