Jan 29, 2023 02:36 UTC
  • Jenerali Mmarekani atabiri vita na China mwaka 2025, anawaambia maafisa wajitayarishe

Jenerali wa nyota nne wa Jeshi la Wanahewa la Marekani ameonya kuhusu uwezekano wa kutokea mzozo wa kijeshi kati yake na China kuhusu eneo la Taiwan mapema mwaka 2025, na hivyo amewataka makamanda kushinikiza vikosi vyao kufikia utayari wa juu zaidi kwa operesheni za kijeshi.

Katika taarifa iliyotolewa kwa mara ya kwanza kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa na baadaye kuthibitishwa na Pentagon, Mkuu wa Kamandi ya Usafiri wa Anga katika Jeshi la Anga la Marekani, Jenerali Mike Minihan, alisema “Natumai nimekosea. Hisia zangu zinaniambia tutakuwa vitani 2025.

Jenerali Minihan ameongeza kuwa lengo kuu la vita hivyo tarajiwa linapaswa kuwa kuizuia, na ikiwa lazima, kuishinda China.

Aidha amesema kwa sababu Taiwan na Marekani zitakuwa na uchaguzi wa rais mwaka 2024, Marekani "itashughulishwa," na Rais wa China Xi Jinping atapata fursa ya kuingia Taiwan.

Ameongeza kuwa, "kwa timu ya Xi, sababu na fursa zote zimeunganishwa kwa ajili ya 2025." Memo iliyotiwa saini na Jenerali Mike Minihan inaelekezwa kwa makamanda wote wa vitengo vyote anga katika Kamandi ya Usafiri wa Anga na makamanda wengine wa Kikosi cha Wanahewa cha Marekani.

Msemaji wa Pentagon amethibitisha kuwepo memo hiyo na kuongeza kwamba, "ndio, ni ukweli kwamba alituma memo hiyo."

Hata hivyo amedai kuwa maoni ya Jenerali Minihan hayawakilishi maoni ya Pentagon kuhusu China. Maafisa wakuu wa Marekani wamedai katika miezi ya hivi karibuni kuwa wana ushahidi kwamba China inaongeza kasi ya muda wake wa kuchukua udhibiti wa Taiwan.

China ina mamlaka juu ya kisiwa cha Taiwan na inasisitiza sera ya ‘China Moja’, ambapo karibu nchi zote za dunia zinatambua sera hiyo, kumaanisha kwamba hazitaanzisha mawasiliano ya kidiplomasia na serikali ya kisiwa hicho chenye serikali iliyotangaza kujitenga na China.

Mvutano juu ya kisiwa hicho kinachojitawala uliongezeka kufuatia ziara ya uchochezi kisiwani humo mnamo Agosti na Nancy Pelosi, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani. Serikali ya China inasisitiza kuwa suala la Taipei ni mstari mwekundu ambao haupaswi kuvukwa na yeyote.

Tags