Nyaraka za Uingereza: Bush aliiamuru CIA kutafuta shakhsia mbadala wa Arafat
https://parstoday.ir/sw/news/world-i93574-nyaraka_za_uingereza_bush_aliiamuru_cia_kutafuta_shakhsia_mbadala_wa_arafat
Rais wa zamani wa Marekani George W Bush aliliamuru Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kumtafuta shakhsia mbadala ili kuchukua nafasi ya aliyekuwa Kiongozi wa Palestina mwendazake Yasser Arafat baada ya kupamba moto Intifadha ya Pili ya Wapalestina mwaka 2001. Hayo ni kwa mujibu wa nyaraka za Uingereza zilizotolewa hadharani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2023 04:24 UTC
  • Nyaraka za Uingereza: Bush aliiamuru CIA kutafuta shakhsia mbadala wa Arafat

Rais wa zamani wa Marekani George W Bush aliliamuru Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kumtafuta shakhsia mbadala ili kuchukua nafasi ya aliyekuwa Kiongozi wa Palestina mwendazake Yasser Arafat baada ya kupamba moto Intifadha ya Pili ya Wapalestina mwaka 2001. Hayo ni kwa mujibu wa nyaraka za Uingereza zilizotolewa hadharani.

Marekani ilifanya jitihada hizo za kutafuta mbadala wa Arafat baada ya kufeli makubaliano ya Camp David mwaka 2000 kati ya Arafat na Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala wa Kizayuni Ehud Barak. Pande mbili zilikutana kuzungumza baada ya kupamba moto machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika eneo la Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Ghaza. 

Nyaraka hizo za BBC zinaeleza kuwa, Bush alikuwa na matarajio ya mapema kwamba Ariel Sharon ambaye alimrithi uongozi Ehud Barak angetumia eneo la Ukanda wa Ghaza kuibua mgawanyiko kati ya Wapalestina. Nyaraka hizo zilizonaswa zinaweka wazi kuhusu majadiliano yaliyofanywa kati ya Marekani na Uingereza miezi michache baada ya Bush na serikali yake ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Wahafidhina Mamboleo kuingia White House. 

Rais wa wakati huo wa Marekani, George W.Bush 

Intifadha ya Pili ya Wapalestina ilikuwa imepamba moto wakati George W. Bush alipoapishwa kuwa Rais wa Marekani mwezi Januari mwaka 2001. Mapambano hayo ya Intifadha yalishika kasi mwishoni mwa Septemba 2000 wakati Ariel Sharon alipoingia katika uwanjwa wa msikiti Mtukufu wa al Aqsa; kitendo ambacho kilitajwa na Wapalestina kama kitendo cha uchokozi na uchochezi. 

Wakati huo serikali ya Bush ilimtaka Kiongozi wa PLO Yassir Arafat asitishe Intifadha hiyo ya Pili ya Wapalestina eti ili kuandaa mazingira ya kuanza mazungumzo ya usalama kati ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel. Si hayo tu, bali serikali ya Bush ililipiga veto rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iliyokuwa imependekeza kutumwa kikosi cha waangalizi wa UN ili kuwalinda raia wa Palestina mkabala wa wanajeshi wa Israel.