Nebenzya: Mlipuko wa Nord Stream ni ugaidi wa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i94352-nebenzya_mlipuko_wa_nord_stream_ni_ugaidi_wa_kimataifa
Mwakilishi wa Kudumu wa Shirikisho la Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa milipuko iliyotokea kwenye mabomba ya gesi ya Nord Stream 1 na Nord Stream 2 ni ugaidi wa kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 22, 2023 23:03 UTC
  • Nebenzya: Mlipuko wa Nord Stream ni ugaidi wa kimataifa

Mwakilishi wa Kudumu wa Shirikisho la Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa milipuko iliyotokea kwenye mabomba ya gesi ya Nord Stream 1 na Nord Stream 2 ni ugaidi wa kimataifa.

Tarehe 27 Septemba, 2022, kuliripotiwa uharibifu mkubwa kwenye mabomba ya Nord Stream, na wataalamu wa matetemeko ya ardhi wa Uswidi walirekodi milipuko miwili mnamo Septemba 26 kando ya njia za mabomba hayo.
Kulipuliwa kwa mabomba ya Nord Stream 1 na 2 kulishusha chini usafirishaji wa gesi na kuvuja kwa bidhaa hiyo katika Bahari ya Baltic.

Vasily Nebenzya, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba:"Kama wengi wenu mnakumbuka, tangu wakati huo ilikuwa wazi ni nani alihusika na kitendo hiki cha ugaidi wa kimataifa,"

Mwanadiplomasia huyo wa Russia pia ameashiria umuhimu wa kufunguliwa mashtaka dhidi ya wahusika wa hujuma ya Nord Stream ili kuzuia mwanzo wa enzi za "machafuko na uharibifu usiotasawarika kwa wanadamu wote."

Shirikisho la Russia limefungua kesi ya kuchunguza kitendo hicho cha ugaidi wa kimataifa. 

Mnamo siku ya Jumatano ya tarehe 8 Februari, ripota mchunguzi wa Marekani, Seymour Hersh, alitoa ripoti yake ya uchunguzi aliofanya, akiishutumu serikali ya Washington kuwa ndiyo iliyohusika na miripuko iliyotokea Septemba mwaka jana kwenye mabomba ya usafirishaji gesi ya Nord Stream. 

Kulingana na chanzo cha habari cha kuaminika kilichozungumza na Hersh, mada za miripuko ziliwekwa kwenye mabomba makuu katika Bahari ya Baltic mnamo Juni 2022 na wazamiaji wa Jeshi la Marekani kwa kutumia kivuli cha mazoezi ya kijeshi ya shirika la kijeshi NATO na kisha yakaripuliwa baadaye kwa kutumia rimoti kutokea mbali.