Russia: Ulaya ni mtumwa na mfuasi aliyesalimu amri kwa Marekani
-
Vasily Nebenzya
Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kwamba Ulaya haijawahi kunyenyekea na kuwa mtumwa wa Marekani kiasi hiki cha sasa katika kipindi chote cha historia.
Vasily Nebenzya ambaye alikuwa akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amekosoa kujisalimisha kwa nchi za Ulaya kwa Marekani na kusema kwamba kwa sasa hakuna uhusiano wowote kati ya Umoja wa Ulaya na Russia.
Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa mwezi Julai 2022, Umoja wa Ulaya ulikata kabisa uhusiano wake na Moscow, na pato la taifa la nchiz a umoja huo limeshuka hadi karibu sifuri. Ameongeza kuwa viwango vya mfumuko wa bei katika nchi za Ulaya vimeongezeka na kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Vasily Nebenzya pia ameashiria kuhusika kwa Washington katika mlipuko wa mabomba ya kusafirisha gesi ya Nord Stream na kusema kuwa Ulaya haijawahi "kuwa mtumwa" kwa Marekani kwa kiasi hiki cha sasa katika historia ya bara hilo.
Nebenzya amesema Brussels imenyamaza kimya kuhusu kadhia ya mabomba la Nord Stream, ambayo yalilipuliwa na Marekani.
Awali Mwakilishi wa Kudumu wa Shirikisho la Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa milipuko iliyotokea kwenye mabomba ya gesi ya Nord Stream 1 na Nord Stream 2 ni ugaidi wa kimataifa.
Tarehe 27 Septemba, 2022, kuliripotiwa uharibifu mkubwa kwenye mabomba ya Nord Stream, na wataalamu wa matetemeko ya ardhi wa Uswidi walirekodi milipuko miwili mnamo Septemba 26 kando ya njia za mabomba hayo.Kulipuliwa kwa mabomba ya Nord Stream 1 na 2 kulishusha chini usafirishaji wa gesi na kuvuja kwa bidhaa hiyo katika Bahari ya Baltic.
Mnamo siku ya Jumatano ya tarehe 8 Februari, ripota mchunguzi wa Marekani, Seymour Hersh, alitoa ripoti yake ya uchunguzi aliofanya, akiishutumu serikali ya Washington kuwa ndiyo iliyohusika na miripuko iliyotokea Septemba mwaka jana kwenye mabomba ya usafirishaji gesi ya Nord Stream.