Msemaji wa Kremlin: Moscow haitayarejesha maeneo yaliyounganishwa na Russia
Feb 28, 2023 22:52 UTC
Msemaji wa ofisi ya rais wa Russia amesema, Moscow haitabadilisha msimamo wake kuhusu mikoa minne ya Ukraine iliyojiunga na nchi hiyo mwaka 2022 baada ya kuitisha kura ya maoni.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Dmitry Peskov, msemaji wa ofisi ya rais wa Russia alitangaza jana Jumanne kuwa maeneo hayo manne yaliyounganishwa na nchi hiyo mwaka 2022 yanahusiana na masuala ya ndani ya Russia na akaongezea kwa kusema, ikiwa Ukraine itakubali kujiunga maeneo hayo manne na ardhi ya Russia, Moscow itakuwa tayari kufanya mazungumzo na Kyiv kwa ajili ya kukomesha vita.
Kuanzia Septemba 23 hadi 27, 2022, kura za maoni zilifanyika katika maeneo ya Donetsk, Luhansk, Zaporizhia na Kherson kuhusiana na kujiunga na Russia. Akthari ya wakazi wa maeneo hayo walipiga kura kuunga mkono uamuzi wa kujiunga na nchi hiyo.
Mnamo Septemba 30, 2022, Rais Vladimir Putin wa Russia na wakuu wa maeneo hayo manne walitia saini makubaliano ya maeneo yao kuunganishwa na Moscow.
Aidha, mnamo Oktoba 4, 2022, Putin aliidhinisha sheria inayohusu mikataba ya kukubaliwa maeneo hayo kuwa sehemu ya shirikisho la Russia.
Wizara ya Ulinzi ya Ukraine hivi karibuni ilitangaza kuwa sharti muhimu zaidi la Kiev kuanza mazungumzo na Moscow ni kuondolewa vikosi Russia katika maeneo yote ya ardhi ya Ukraine.
Hata hivyo, Moscow inasisitiza kuwa inazingatia masharti yake tu iliyotoa na itakuwa tayari kufanya mazungumzo yanayokubaliwa na akili timamu.../
Tags