Mar 09, 2023 07:07 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan: Uislamu ni mlindaji mkubwa zaidi wa haki za wanawake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amesema, Uislamu ni mlindaji mkubwa zaidi wa haki za wanawake.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Radio Pakistan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Bilawal Bhutto Zardari, ameyasema hayo alipohutubia kongamano la "Wanawake katika Uislamu" lililofanyika New York Marekani sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambapo mbali na kubainisha hadhi na nafasi ya wanawake katika dini tukufu ya Uislamu amesema: Uislamu unalinda kikamilifu haki zote za wanawake, unapinga kutumiwa rangi, asili na jinsia kama msingi wa kuwapambanua na kuwatafautisha watu; na mwanamke ana hadhi maalumu ya kijamii na kiraia katika jamii ya Kiislamu.
Bilawal Bhutto Zardari, amezungumzia nafasi na mchango mkubwa wa wanawake katika historia ya Uislamu, hususan sifa tukufu za tabia na akhlaqi za Bibi Khadija (as) mke wa Mtume Muhammad SAW na Bibi Zainab (as), binti wa Imamu wa kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani Imam Ali AS na akasema: Historia ya Uislamu inaonesha kuwa wanawake wa Kiislamu wametoa mchango mkubwa katika nyanja zote za maisha, ikiwemo elimu, biashara, uchumi na siasa ambapo kwa kuzingatia ushiriki hai na amilifu wa wanawake wa Kiislamu katika medani za kimataifa za zama hizi, yote hayo yanaonyesha umuhimu wa haki za wanawake katika Uislamu.
Bilawal Bhutto Zardari (wa pili kushoto) akihutubia mkutano wa "Wanawake Katika Uislamu", New York Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ametilia mkazo pia ushiriki na mchango mzuri wa wanawake wa Kiislamu katika masuala ya nchi na maendeleo ya kivitendo na akaongeza kuwa: katika dini ya Uislamu mwanamke ana utambulisho wa kujitegemea wa kijamii na kisheria, na haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi na kijamii za wanawake zinahifadhiwa na kulindwa kikamilifu.

Katika hotuba yake hiyo Bilawal Bhutto Zardari ameashiria pia matatizo ya wanawake katika maeneo na nchi kama Iraq, Afghanistan, Ukraine au baadhi ya nchi za Kiafrika ambazo zimekabiliwa na vita na akasema: Jamii ya Kimataifa inapaswa kufanya juhudi athirifu zaidi kwa ajili ya kurejesha haki za wanawake.../

 

Tags