Askofu Mkuu wa Anglikana amuomba Museveni asipasishe sheria dhidi ya ushoga
https://parstoday.ir/sw/news/world-i95490-askofu_mkuu_wa_anglikana_amuomba_museveni_asipasishe_sheria_dhidi_ya_ushoga
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana lenye makao makuu yake mjini Canterbury nchini Uingereza anatazamiwa kumuandikia barua Rais Yoweri Museveni wa Uganda, kumuasa asipasishe kuwa sheria muswada wa kupambana na ushoga na mahusiano ya watu jinsia moja uliopitishwa hivi karibuni na Bunge la nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 25, 2023 07:14 UTC
  • Askofu Mkuu wa Anglikana amuomba Museveni asipasishe sheria dhidi ya ushoga

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana lenye makao makuu yake mjini Canterbury nchini Uingereza anatazamiwa kumuandikia barua Rais Yoweri Museveni wa Uganda, kumuasa asipasishe kuwa sheria muswada wa kupambana na ushoga na mahusiano ya watu jinsia moja uliopitishwa hivi karibuni na Bunge la nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Lambeth Palace, Msemaji wa Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby, amesema kiongozi huyo wa 'Kanisa la Uingereza' na jamii ya Wanglikana duniani atamuandikia barua Museveni kumtaka autupilie mbali muswada huo. 

Kabla ya hapo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana huko Wales, Andrew John alisema muswada huo unatia wasiwasi mkubwa na kukirihisha, na eti hauendani na mafundisho ya Kristo (Yesu), Nabii Issa AS. Amesema pia atamuandukia barua Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Uganda, Stephen Samuel Kaziimba kumueleza hofu yake juu ya muswada huo.

Jumanne iliyopita, Bunge la Uganda kwa kauli moja lilipitisha muswada wa sheria inayoharamisha kujitambulisha kama mtu mwenye uhusiano wa jinsia moja au LGBTQ na kuzipa mamlaka madaraka makubwa katika kukabiliana na raia wa nchi hiyo wanaojihusiha na uovu huo.

Aidha wabunge hao wamepitisha kipengee kwenye muswada huo kinachotaka hukumu ya kifo kwa watakaopatikana na hatia ya kuwa mahusiano maovu ya jinsia moja. Muswada huo unasubiri saini ya Rais Museveni ili iwe sheria.

Rais wa Uganda

Museveni amekuwa akilaani vikali mahusiano ya jinsia moja kwa muda mrefu na mwaka 2013 alitia saini sheria ya kukabilkiana na uovu huo. Tayari zaidi ya nchi  nchi 30 za Afrika, ikiwemo Uganda, zimepiga marufuku mahusiano ya jinsia moja.

Februari mwaka huu, viongozi wa Kanisa la Kianglikana barani Afrika walitishia kujitenga na Kanisa mama la Uingereza kwa kubariki na kuruhusu ndoa na mahusiano ya watu wenye jinsia moja. Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Uganda, Stephen Samuel Kaziimba Mugalu alisema: Sisi kama Kanisa la Uganda hatuwezi kuunga mkono uamuzi huo, Mungu hawezi kubariki kitu ambacho amekitaja kuwa ni dhambi.