May 16, 2023 01:31 UTC
  • Idara ya Kuzuia Uhalifu Ujerumani: Makumi ya misikiti imeshambuliwa nchini

Idara ya Kuzuia Uhalifu ya Ujerumani imetangaza kwamba makumi ya mashambulizi dhidi ya misikiti yamesajiliwa nchini humo mwaka 2022.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Kuzuia Uhalifu ya Ujerumani limechapisha ripoti yake ya mwaka 2022 kuhusu idadi ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya misikiti nchini humo, ambayo inaonyesha kuwa mashambulizi 62 ​​yalirekodiwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14 ikilinganishwa na mwaka 2021.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mengi kati ya mashambulizi haya yalifanywa na watu binafsi au makundi ya mrengo wa kulia yenye mitazamo ya kuchupa mipaka.

Ikumbukwe kuwa, shirika la Al-Azhar la kupambana na misimamo mikali awali lilitoa ripoti kadhaa zinazoonyesha ongezeko la mashambulizi ya watu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia dhidi ya Waislamu na maeneo yao matukufu, na vilevile uchochezi unaoendelea kufanywa dhidi yao katika hotuba za hadhara na kurasa za mitandao ya kijamii.

Shirika hilo la Al-Azhar limesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya hujuma na propaganda chafu za kueneza chuki dhidi ya Uislamu yanahitaji kuchukuliwa hatua kali zaidi dhidi ya makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na kuzidisha juhudi za kueneza itikadi ya kuvumiliana na kuishi pamoja kwa amani katika jamii.

Msikiti uliochomwa moto, Uholanzi

Nchi za Magharibi, ikiwemo Ujerumani, zimeruhusu hujuma na vitendo vyote vya kuuvunjia heshima Uislamu na matakatifu ya Kiislamu, kama vile Mtume Muhammad (saw) na Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha kulinda uhuru wa kusema na kujieleza; na serikali na sheria za nchi hizo zinawaunga mkono na kuwahami watu na makundi yanaopiga vita Uislamu yakiwemo makundi ya mrengo wa kulia yenye itikadi kali.

Tags