Marekani yakiri; Vikwazo vimepunguza matumizi ya dola duniani
(last modified Thu, 15 Jun 2023 02:51:34 GMT )
Jun 15, 2023 02:51 UTC
  • Marekani yakiri; Vikwazo vimepunguza matumizi ya dola duniani

Waziri wa Hazina ya Taifa ya Marekani amekiri kuwa, vikwazo vya Washington vinaelekea kusambaratisha ukiritimba na matumizi ya safaru ya dola katika miamala ya kibiashara duniani.

Janet Yellen amesema hayo mbele ya Kamati ya Fedha ya Kongresi ya Marekani na kueleza kuwa, vikwazo vya Washington vimepelekea nafasi ya sarafu ya dola katika miamala na mabadilishano ya kibiashara kuporomoka kwa kuwa aghalabu ya nchi zinafadhilisha kutumia sarafu nyingine na njia mbadala.

Waziri wa Fedha wa Marekani ameiambia kamati hiyo ya Kongresi kuwa, "Haistaajabishi kuona nchi zinazohofia kuathiriwa na vikwazo vyetu zinatafuta mbadala wa dola."

Duru za kiuchumi zinaarifu kuwa, wafanyabiashara wa mafuta duniani hivi karibuni wameanzisha kampeni ya kutumia sarafu mbadala, na kuachana na dola ya Marekani katika miamala yao. 

Waziri wa Fedha wa Marekani, Janet Yellen

Haya yanajiri siku chache baada ya Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya kusema kuwa, vikwazo vya Marekani mbali na kukiuka mamlaka ya kujitawala nchi nyingine duniani, lakini pia vinakanyaga sheria na kanuni za kimataifa.

Aidha Alena Douhan ambaye ni Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa juu ya athari mbaya za hatua za upande mmoja alisema karibuni kuwa, vikwazo vya upande moja vimedhoofisha uwezo wa kiutendaji wa UN na kuibua hofu katika ushirikiano wa kimataifa na utawala wa sheria.

Ukiritimba wa miongo mingi wa sarafu ya dola ya Marekani katika mabadilishano ya kimataifa umekumbwa na changamoto katika miezi ya hivi karibuni, huku baadhi ya nchi zikiamua kutumia sarafu zao za taifa kwenye mabadilishano yao.