Pakistan yaanza kutekeleza mchakato wa kuitosa sarafu ya dola
Pakistan imechukua hatua ya kwanza ya kivitendo ya kutekeleza sera yake mpya ya kuachana na sarafu ya dola katika miamala na mabadilishano yake ya bidhaa, kwa kutumia sarafu ya Yuan ya China kununua mafuta ghafi ya Russia kwa bei nafuu.
Hayo yalisemwa jana Jumatano na Waziri wa Mafuta wa Pakistan, Musadik Malik na kuongeza kuwa, muamala wa serikali kwa serikali wa ununuzi wa tani 100,000 za mafuta ya Russia umefanyika kwa kutumia safaru ya China.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, shehena ya kwanza ya mafuta ghafi ya Russia iliwasili Pakistan mnamo Juni 12, na kupakuliwa katika bandari ya mjini Karachi, kusini mwa nchi hiyo.
Nchi nyingi hivi sasa zimeamua kutafuta sarafu mbadala ya kufidia nafasi ya sarafu ya dola katika miamala na mabadilishano yao ya bidhaa na washirika wao wa biashara kama China, India na Russia.
Ukiritimba wa miongo mingi wa sarafu ya dola katika mabadilishano ya kimataifa umekumbwa na changamoto katika miezi ya hivi karibuni. Wafanyabiashara wa mafuta duniani hivi karibuni wameanzisha kampeni ya kutumia sarafu mbadala zisizo dola ya Marekani katika miamala yao.
Mabadiliko hayo yamesababishwa na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia na uhaba mkubwa wa sarafu ya dola katika nchi mbalimbali duniani. Iran, Ghana, Misri, Russia na India ni miongoni mwa nchi zinazofanya baadhi ya miamala yao ya kibiashara kwa kutumia sarafu zao za ndani.