Kuendelea harakati hatari za kijeshi za Marekani barani Asia
(last modified Sun, 18 Jun 2023 10:26:49 GMT )
Jun 18, 2023 10:26 UTC
  • Kuendelea harakati hatari za kijeshi za Marekani barani Asia

Sera hatari za kijeshi na za kichochezi za Marekani katika bara kubwa duniani yaani bara la Asia zingali zinaendelea.

Mapema siku ya Ijumaa ya tarehe 16 Juni, nyambizi ya silaha za nyuklia ya "USA Michigan," ilitia nanga katika bandari ya Busan iliyoko umbali wa kilomita 320 kusini mashariki mwa Seol, mji mkuu wa Korea Kusini.

Kutia nanga nyambizi hiyo ya nyuklia ya Marekani katika bandari ya Korea Kusini kumekuja baada ya Korea Kaskazini kulalamika siku moja kabla yake yaani Alkhamisi ya tarehe 15 Juni, 2023, kwamba, mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na Marekani karibu na mipaka ya majini ya Korea Kaskazini ni tishio kwa nchi hiyo na ndio maana serikali ya Pyongyang iliamua kufanya majaribio moja ya makombora yake ya balestiki ya masafa mafupi kuelekea upande wa Bahari ya Japan. Kabla ya hapo pia Korea Kaskazini ilikuwa imetangaza kuwa, itazidi kujiimarisha kijeshi ili kukabiliana na vitisho vya Marekani. Ni jambo lililo wazi kuwa, luteka ya kijeshi ya Marekani huko Korea Kusini kwa kisingizio ya kumbukumbu ya mwaka wa 17 wa muungano wa nchi hizo mbili ni tishio, ni uchochezi na ni hatari kubwa kwa Pyongyang hususan kutokana na kufanyika kwake katika umbali wa kilomita 25 tu kutoka kwenye mpaka wa pamoja wa Korea Kusini na Korea Kaskazini. Mazoezi hayo ya kijeshi ya Marekani yanaweza kuchochea zaidi moto wa vita baina ya Korea mbili. 

Popote wanapoingia, wanajeshi wa Marekani hufanya uharibifu mkubwa

 

Wakati wa ziara ya rais wa Korea Kusini mjini Washington mwezi Aprili mwaka huu, marais wa nchi mbili za Marekani na Korea Kusini walitiliana saini hati maalumu iliyopewa jina la Azimio la Washington. Mkataba huo ulitiwa saini kwa kisingizio cha kuiimarisha kijeshi Korea Kusini kwa madai kuwa eti Korea Kaskazini ni tishio kubwa kwa Korea Kusini. Ikijibu chokocho hizo, Wizara ya Ulinzi wa Korea Kaskazini mbali na kulaani uchochezi huo wa Marekani ilisema kuwa, kufanyika mazoezi ya kijeshi ya Marekani huko Korea Kusini  karibu na mpaka wa Korea Kaskazini ni uchochezi wa wazi na hautaachwa hivi hivi bila ya kupata majibu yanayostahiki kutoka kwa Pyongyang.

Serikali ya Korea Kaskazini imesema kuhusu mkataba wa silaha za nyuklia baina ya Marekani na Korea Kusini kwamba, maadamu Washington inaendelea na siasa zake za kiuadui zenye shabaha ya kuupindua utawala wa Korea Kaskazini, kamwe isifikirie kwamba Pyongyang itaachana na juhudi zake za kuimarisha zaidi makombora na silaha zake za nyuklia. Kim Yo Jong, dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini amesema, hatua ya Marekani ya kujizatiti kwa silaha za nyuklia huko Korea Kusini haina matunda mengine zaidi ya kushadidisha ukosefu wa amani tu duniani. Vile vile amesema, makubaliano baina ya marais wa Marekani na Korea Kusini ni hatua inayoonesha uadui na chuki kubwa mno za madola hayo mawili dhidi ya Korea Kaskazini na matokeo yake ni kutumbikizwa hatarini tu amani na usalama wa ukanda wa kaskazini mashariki mwa bara la Asia na dunia nzima kwa ujumla. 

Marekani na madola ya Magharibi hayaruhusu kabisa kuishi pamoja kwa salama Korea mbili

 

Kichekesho kikubwa ni kwamba, viongozi hao hao wa Marekani ambao wanachochea machafuko na ukosefu wa amani katika ukanda wa kaskazini mashariki mwa Asia, ndio hao hao wanaojipa uthubutu wa kujifanya ndio viranja wa kupigania haki, usalama na amani katika maeneo mengine duniani. 

Kwa upande wake, serikali ya Korea Kaskazini muda wote inasisitiza kuwa, uchochezi wa Marekani na waitifaki wake katika eneo hilo ikiwemo Korea Kusini ndiyo sababu ya kuongezeka na kuwa makali mashindano ya kujilimbikizia silaha hatari nchi za ukanda huo; suala ambalo matunda yake ni kutoweka utulivu na kudhoofika usalama na amani baina ya Korea mbili. Kila baada ya Marekani kufanya luteka za kijeshi kwenye maeneo ya karibu na Korea Kaskazini, serikali ya Pyongyang nayo huwa inafanyia majaribio makombora yake ya balestiki. Lengo la Korea Kaskazini ni kuutangazia ulimwengu kuwa inafuatilia kwa karibu uchochezi wa kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa eneo la kusini mashariki mwa Asia na karibuni na mipaka yake. Vile vile lengo la Pyongyang ni kuonesha kuwa ina nguvu za kutosha za kijeshi za kuzuia shambulio lolote lile dhidi yake. Kiujumla ni wajibu tusema kuwa, uchochezi wa kijeshi wa Marekani katika ukanda wa kusini mashariki mwa Asia bila ya shaka yoyote ndio unaochochea mashindano ya silaha katika eneo hilo na hivyo kuandaa mazingira ya kukosekana amani na utulivu katika eneo hilo nyeti na muhimu duniani.

Tags