Siku 500 za vita huko Ukraine na mustakbali wake
Vita vya Ukraine vimepitisha siku 500 tangu kuanza na hakuonekani matarajio ya kumalizika vita hivyo vya umwagaji damu barani Ulaya. Vita hivyo ambavyo awali ilidhaniwa kwamba huwenda vingechukua muda mfupi na kumalizka haraka, sasa vimekuwa mapigano ya kijeshi ya muda mrefu na ya umwagaji damu.
Rais Vladimir Putin wa Russia Alhamisi ya Februari 24 mwaka jana alitangaza kupitia hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni, kwamba vikosi vya jeshi la nchi hiyo vitatekeleza oparesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbass. Baada kidogo ya kutangaza operesheni hiyo ya kijeshi, Putin alitaka Ukraine isifanywe ya kijeshi na akatoa wito kwa wanajeshi wa nchi hiyo kuweka chini silaha zao. Kwa utaratibu huo, Moscow ilichukua hatua baada ya kutoa indhari kadhaa kwa viongozi wa ngazi ya juu wa Ukraine ikitaka nchi hiyo isijiunge na NATO na kuitaka iheshimu haki za raia wa Kirusi wanaoishi huko Donbass; na baada ya Kiev kupuuza tahadhari hizo za Moscow. Rais Joe Biden wa Marekani alitoa taarifa baada ya hotuba ya Rais Vladimir Putin ambapo aliitaja Russia kuwa inahusika na vita vya Ukraine na maafa makubwa ya vita hivyo, licha ya kwamba Washington ilipuuza kwa makusudi mchango wake mkubwa na wa moja kwa moja katika hali mbaya ya sasa huko Ukraine.
Matukio mengi ya kisiasa na kijeshi yamejiri katika vita vya Ukraine lakini tunaweza kusema kuwa, mafanikio muhimu zaidi ya Russia katika vita hivyo, licha ya kuuliwa idadi kubwa ya watu na kuangamizwa zana nyingi za kijeshi, ni kuunganishwa rasmi majimbo manne na Russia, ambayo ni nukta muhimu katika mchakato wa vita vya Ukraine.
Vita vya Ukraine pia vinaweza kutathminiwa kuwa ni matokeo ya nia mbaya na tabia ya kupenda vita ya nchi za Magharibi mkabala wa Russia. Ukweli ni kwamba oparesheni ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine bila shaka ni jibu la Moscow kwa chokochoko za kupenda vita za nchi za Magharibi kupitia njia ya kuichochea Ukraine kuwa mwanachama ndani ya muungano wa kijeshi wa Magharibi (NATO) na kuibua vitisho dhidi ya usalama wa taifa wa Russia. Russia ilichukua hatua hiyo baada ya jibu hasi la Marekani na NATO kwa maombi ya kimantiki ya Moscow ambayo ilitaka kutounganishwa Ukraine katika shirika la NATO na kuondoka wanajeshi wa shirika hilo katika mipaka ya mwaka 1997, yaani kabla ya kuanza mchakato wa nchi za Ulaya Mashariki na Kati wa kuomba uanachama katika jumuiya hiyo.
Ushahidi unaonyesha kuwa NATO na Marekani baada ya kipindi cha Vita Baridi, taratibu zilianza kudhihirisha misimamo ya uhasama dhidi ya Russia zikifanya juhudi za kuidhoofisha nchi hiyo. Sasa Marekani na NATO zinavichukulia vita vya Ukraine kama fursa ya aina yake ya kuisambaratisha Russia kijeshi, kiuchumi na hatimaye kisiasa, na wakati huo huo kudidimiza uhalali wa Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin. Kwa muda sasa Marekani imekuwa ikifanya kila iwezalo ili Russia isambaratike na hata kuigawa nchi hiyo. Wasiwasi wa viongozi wa serikali ya Marekani kuhusu silaha za nyuklia za kistratejia za Russia na hatua ya Vladimir Putin ya kukabiliana na sera na mienendo ya kibeberu ya Marekani katika pembe mbalimbali duniani; muhimu zaidi ikiwa ni hatua ya Russia na China ya kuchukua nafasi ya mfumo wa kimataifa wa kiliberali wa Magharibi duniani, vimeifanya Marekani kutumia kila fursa iliyoko mbele yake ili kupunguza uwezo na nguvu ya Russia.
Ni dhahir shahir kuwa, kwa kuzingatia sera za nyenendo za Wamagharibi na hasa Marekani, uwezekano wa kuendelea na kupanuka zaidi vita huko Ukraine umeongezeka zaidi kuliko huko nyuma. Jambo muhimu ni kwamba katika uwanja wa siasa za ndani za Marekani, kuna upinzani mwingi kwa sera ya serikali ya Joe Biden kuhusiana na vita vya Ukraine. Robert F. Kennedy Junior mgombea wa kiti cha urais nchini Marekani mwaka kesho wa 2024 ambaye pia ni mpwa wa John F. Kennedy rais wa zamani wa Marekani anasema: "Washington imeugeuza mgogoro wa Ukraine kuwa vita vya niaba kati ya Russia na Marekani." Kennedy amesisitiza kuwa: Marekani ilitaka kuanzishwa vita huko Ukraine kutokana na sababu zilizobainishwa na Biden, na lengo halisi la vita hivyo ni kuiondoa madarakani serikali ya Russia. Washington na waitifaki wake wa Magharibi hadi sasa wameipatia Ukraine silaha na zana za kijeshi zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni mia moja; na kwa utaratibu huo kuandaa mazingira ya kuendelea vita hivyo kwa muda mrefu na kuharibiwa pakubwa nchi hiyo kubwa ya Ulaya Mashariki.
Katika hatua ya karibuni, Marekani imepanga kuipatia Ukraine shehena kubwa ya mabomu ya vishada katika fremu ya kifurushi cha msaada wa silaha wenye thamani ya dola milioni 800 kwa serikali ya Kiev. Silaha hizo zilizopigwa marufuku kwa kuzingatia athari na maafa yake makubwa kwa binadamu, zinatumwa Ukraine kwa lengo la kuuwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Russia na kuangamiza zana za kijeshi za nchi hiyo. Wakati huo huo kwa kuzingatia kuwa silaha hizo ambazo zinasambazwa ardhini katika muundo wa risasi ndogo ndogo si tu kuwa zinadumu kwa muda mrefu, bali pia ni hatari na tishio kubwa kwa raia wa kawaida.
Ni wazi kuwa taathira mbaya za mabomu ya vishada zilipelekea kuanzishwa mkataba wa marufuku mabomu ya vishada uliosainiwa mwaka 2008; na hadi kufikia sasa nchi 11 duniani zimejiunga na mkataba huo na nyingine 12 zimesaini hati ya mkataba huo lakini bado hazijapasisha mkataba huo.
Colin Hackett Kahl, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani katika Masuala ya Siasa amekiri kwamba mabomu ya vishada yatakayotumwa na nchi hiyo huko Ukraine huenda yakasababisha vifo vya raia wengi, lakini anasisitiza kuwa, jambo baya zaidi kwa raia wa Ukraine ni kuiona Russia ikishinda vita hivyo!
Uamuzi wa Marekani wa kutuma mabomu ya vishada nchini Ukraine umepingwa vikali na hata nchi waitifaki wa Washington kama Ujerumani, Uingereza na Uhispania.
Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia, amezungumzia uamuzi wa Rais wa Marekani wa kupeleka mabomu ya vishada nchini Ukraine na kusema: "Joe anayesinzia mchana anataka kuanzisha vita vya Akheri Zamani. Azma ya Biden ya kutuma mabomu ya vishada nchini Ukraine yanaiweka dunia kwenye ncha ya hatari."