Jumatatu tarehe 30 Disemba 2024
https://parstoday.ir/sw/radio/event-i120770
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Jumadithani 1446 Hijria sawa na Disemba 30 mwaka 2024.
(last modified 2024-12-30T02:55:01+00:00 )
Dec 30, 2024 02:55 UTC
  • Jumatatu tarehe 30 Disemba 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 28 Jumadithani 1446 Hijria sawa na Disemba 30 mwaka 2024.

Katika siku kama hii ya leo na miaka 856 iliyopita alifariki dunia Abul-Qasim al-Shatibi, msomi mashuhuri wa Qur'ani aliyekuwa maarufu kwa jina la Imamul Qurra. Abul-Qasim alizaliwa mwaka 538 Hijiria.

Mbali na kuwa mtaalamu mkubwa katika taaluma ya usomaji wa Qur'ani, alikuwa pia mtaalamu wa elimu ya tajweed, tafsiri ya Qur'an, Hadithi, sarufi ya lugha ya Kiarabu na elimu nyinginezo za kipindi hicho. Licha ya kuwa kipofu lakini alisifika kwa kuwa hodari na alifanikiwa kuhifadhi hadithi nyingi kifuani mwake.

Msomi huyo wa Kiislamu ameacha athari kwa vizazi vya baada yake na miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kitabu kiitwacho "al Qasidatus Shatwibiyyah" kilichokusanya masuala yanayohusiana na elimu ya tajweed.   

Miaka 144 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, alifariki dunia alimu na mtaalamu wa fasihi wa Kiirani, Mirza Muhammad bin Sulaiman Tankabani.

Mbali na kubobea katika elimu ya fiq'hi, Tankabani pia alikuwa mtaalamu katika fasihi na mshairi mkubwa katika kipindi chake. Muhammad bin Suleiman ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na "Al Fawaidu fii Usuliddin" na " Qisasul-Ulama." Katika kitabu hicho kilichochapishwa mara kadhaa nchini Iran alizungumzia maisha ya maulama wa kabla yake.   

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, magaidi wa mashirika mawili ya kijasusi ya Israel walishambulia kitongoji cha Balad al-Sheikh huko Palestina na kuchoma moto nyumba za kitongoji hicho.

Moto huo uliwateketeza na kuwaua shahidi Wapalestina 60. Siku hiyo hiyo kundi jingine la kigaidi la Israel lililojulikana kwa jina la Irgun lilidondosha mabomu katikati ya kundi la Wapalestina na kuwaua shahidi 17 kati yao.

Mashambulio hayo yaliyoshadidi mwishoni mwa mwaka 1947 na mwanzoni mwa 1948, yalikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao ili kuasisisiwa utawala pandikizi na ghasibu wa Israel katika ardhi hizo.   

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita iliundwa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha pamoja Shia na wafuasi wa Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) kote duniani, kujenga uhusiano baina yao, kunyanyua juu kiwango cha shule za kidini, kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza baina ya wafusi wa Ahlul Bait na madhehebu nyingine za Kiislamu na kadhalika.

Tarehe 31 Disemba mwaka 1994 yaani miaka 30 iliyopita, Idhaa ya Kiswahili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliasisiwa kwa shabaha ya kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wazungumzaji wa lugha hiyo.

Matangazo ya Idhaa hii yalianza sambamba na sherehe ya kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran yanahusu masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika. Kwa sasa unaweza kuyasikiliza matangazo yetu kwa njia ya moja kwa moja na kupitia hifadhi ya matangazo wakati wowote. Unaweza pia kuyapata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran kupitia simu ya mkononi bila ya kutoa malipo yoyote isipokuwa gharama zako za kawaida za Intaneti kupitia njia ya kupakua aplikesheni ya matangazo yetu ya IRIB World Service.

Tarehe 30 Disemba miaka 18 iliyopita Saddam Hussein mtawala katili na dikteta wa zamani wa Iraq, alinyongwa baada ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi yake.

Saddam alizaliwa mwaka 1937 karibu na mji wa Tikrit uliopo umbali wa kilomita 140 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kujiunga na chama cha Baath akiwa na umri wa miaka 20.

Dikteta huyo alifanikiwa kuwa naibu wa Ahmad Hassan al Bakr kufuatia mapinduzi yaliyojiri ndani ya chama hicho cha Baath mnamo mwaka 1968. Mwaka 1979 Saddam alikuwa Rais wa Iraq na muda mfupi baada ya kushika madaraka alianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisaidiwa na madola ya Magharibi na kufanya mauaji na maafa mengi. Kwa msaada wa madola hayo, Saddam alipata silaha za kemikali na kuzitumia dhidi ya mataifa ya Iran na Iraq. Saddam aliendelea kufanya mauaji ya kila aina dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani, chini ya himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi ikiwemo Marekani. 

Dikteta Saddam Hussein