Nowruz Katika Utamaduni na Mafundisho ya Kiislamu
Tuko katika siku za awali za mwaka mpya wa Kiirani wa 1396 Hijria Shamsia ambao ulianza Machi 21. Siku za kuanza mwaka mpya wa Kiirani hujulikana kama Nowruz au Nairuzi na huadhimishwa kwa furaha na shangwe kote Iran na nchi zinazozungumza Kifarsi pamoja na mataifa yote ambayo kwa njia moja au nyingine yana uhusiano na ustaarabu na utamaduni wa Iran.
Tuko katika siku za awali za mwaka mpya wa Kiirani wa 1396 Hijria Shamsia ambao ulianza Machi 21. Siku za kuanza mwaka mpya wa Kiirani hujulikana kama Nowruz na huadhimishwa kwa furaha na shangwe kote Iran na nchi zinazozungumza Kifarsi pamoja na mataifa yote ambayo kwa njia moja au nyingine yana uhusiano na ustaarabu na utamaduni wa Iran. Siku Kuu ya Nowruz huanza sambamba na kuwadia msimu wa machipuo na hivyo hayo mawili huwa ni sehemu ya utamaduni wa Iran. Nowruz ni siku ya kwanza ya machipuo..., ni siku ya kuhuishwa upya ardhi pamoja na mazingira...., ni siku kuu muhimu kwa Wairani. Tokea zama za kale, Nowruz imekuwa ni siku ya kusherehekea kuhuishwa upya ardhi baada ya msimu wa baridi kali, ni sherehe ya ushindi wa nuru dhidi ya kiza, ni sherehe ya kuenea furaha kote duniani.
Baada ya kudhihiri Uislamu zaidi ya miaka 1400 iliyopita, watu wa Iran ya kale waliikumbatia dini hii tukufu na kusilimu. Baada ya hapo sherehe za Nowruz nazo hatua kwa hatua zilianza kuchanganyika na itikadi za Kiislamu na hivyo kuchukua muelekeo wa kidini. Nowruz huanza kwa machipuo baada ya mimea kudidimia na kupoteza uhai wakati wa msimu wa baridi kali. Kwa msingi huo Nowruz ni kumbusho kuhusu namna mwanadamu atakavyohuishwa katika siku ya kiyama baada ya mauti yake. Halikadhalika Nowruz huambatana na dua na amali nyingi ambazo ni mustahabu. Moja ya nukta muhimu zaidi katika ustaarabu wa Nowruz ni kuwepo Qur'ani Tukufu katika meza au zulia la Nowruz. Kusoma aya za Qur'ani katika dakika na lahadha za kwanza za kuingia mwaka mpya na kuibusu Qur'ani kila aliye katika mjumuiko wa kuukarbisha mwaka mpya, n.k ni kati ya ishara ya namna Wairani walivyoipa utambulisho wa Kiislamu sherehe za Nowruz.
Kuna riwaya mbali mbali kuhusu Nowruz na utukuzaji wa siku hiyo. Riwaya hizo zinathibitisha kuwa Uislamu unatambua Nowruz kama siku muhimu na ndio sababu katika vitabu vya mafuqaha na vitabu vinginevyo vya Kiislamu kumetajwa mengi kuhusu siku hiyo na mila na desturi zake. Moja ya mila na desturi za Nowruz ni usafi na utakasifu. Sheikh Abbas Qummi, msomi mkubwa wa Kiislamu katika kitabu chake maarufu cha Mafatihal-Jinan ameandika hivi: "Imam Sadiq AS alimwambia mmoja kati ya wanafunzi wake aliyejulikana kwa jina la Mualla bin Khunais kuwa: "Ikifika Nowruz, oga josho na uwe nadhifu kwa kuvaa mavazi mazuri zaidi na ujipake uturi bora zaidi na katika siku hiyo ufunge saumu kisha, usali (sala maalumu) na usujudu sijda ya kushukuru."
Wakati wa machipuo mapya ya mazingira, ni wakati muafaka wa kuwa na uhusiano uliojaa ikhlasi na muumba wa mbingu na ardhi. Katika lahadha hii ya kuchipua tena mimea, mwenye kufanya ibada anaweza kumuomba Mola Muumba atuletee mabadiliko katika hali zetu iwe ni katika tabia, kauli na vitendo. Ombi hili huwa katika dua maalumu na fupi ambayo Wairani huomba kwa unyenyekvu na khushuu wakati wa kuingia mwaka mpya. Katika lahadha hiyo ya kuukaribiwa mwaka mpya, Wairani wakiwa pamoja na familia na jamaa zao hunyanua mikono na kumuomba Mola Mlezi kwa kusema.
بسم ﷲ الرّحمن الرّحیم
یا مقلّب القلوب والأبصار، یا مدبّر اللّیل والنّهار، یا محوّل الحول والأحوال، حوّل حالنا إلى أحسن الحال
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu.
Ewe unayebadilisha nyoyo na macho ya watu. Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana! Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.
Kwa hivyo katika dua hii tunaanza kwa kutaja mabadiliko katika moyo kwani pia katika msimu wa machipuo moyo wa sayari ya dunia kama ambavyo moyo wa mwanadamu unahitajia mabadiliko na machipuo mapya ambayo, ili kuyafikia, kuna haja ya kusimama imara. Hapa busara na uono wa mbali una nafasi muhimu katika yale yanayojiri moyoni. Katika sehemu nyingine ya dua hiyo Mwenyezi Mungu ametajwa kama Mpangiliaji wa Usiku na Mchana ambapo usiku na mchana ni nembo za kiza na nuru. Iwapo Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kupangilia usiku na mchana yeye pia ndiye aliyeumba nuru na kiza na hivyo yeye ndie mwenye uwezo wa kuondoa kiza katika nyoyo zetu na kutuangazia nuru ya maarifa yake katika nyoyo zetu kama amabvyo tunasoma katika Sura Al Baqara sehemu ya aya ya 257 katika Qur'ani Tukufu kuwa: " Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani...
Katika sehemu ya mwisho ya dua hiyo Mwenyezi Mungu SWT ametajwa kama Mbadilishaji wa mwaka na mazingira na hapo Muumini anamtaka Mola Mlezi adilishe hali yake iwe bora ya hali. Hii ni kwa sababu ubora wa mwandamu uko katika kubadilika hali yake kubwa bora zaidi. Mtu kuwa na hali bora zaidi kuna maana ya kufika katika ubora ambao humepelekea yeye kuwa na sifa ya mwanadamu.
Moja ya kati ya mila na desturi muhimu za Nowruz ni kutandika zulia au kuandaa meza ya 'Sin Saba" yaani meza ambayo juu yake kuna vitu saba vinavyoanza kwa herufi ya sin ya lugha ya Kifarsi. Meza hii huwa imeandaliwa siku au masaa kadhaa kabla ya kuingia mwaka mpya na hukunjwa katika siku ya 13 ya Farvardin ambao ni mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria Shamsia. Familia hujumuika katika meza hii ambapo Qur'ani Tukufu huwa na nafasi maalumu. Kuchaguliwa nambari saba katika meza hiyo ya 'Haft Sin' kuna maana au ibra muhimu na yenye kuzingatiwa. Mwanazuoni maarufu Allamah Majlisi ambaye ameandika kitabu chenye Jildi 110 kinachojulikana kama Bihar al-Anwar anafafanua ifuatavyo kuhusu herufi hizo saba za sin ifuatavyo: "Kuna mbingu saba kama ambavyo ardhi nazo ni saba na kuna malaika wakuu saba. Hivyo iwapo wakati wa kuingia mwaka mpya utasoma aya saba za Qur'ani Tukufu ambazo zinaanza na herufi ya sin Malaika watakulinda na kukuepusha na madhara ya mbingu na ardhi."
Aya hizi saba za Qur'ani zenye kuanza na herufi ya sin huanza na neno Salam. Kati ya salamu hizi ni Sala na Salamu za Mwenyezi Mungu kwa waumini wa kweli katika Sura Yasin Aya ya 58 isemayo: " "Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu." Katika vitabu vya tafsiri tunasoma kuwa salamu hii ni usalama na utulivu wa kudumu kwa waumini. Katika Tafsir Nemuneh ya Ayatullah Makarim Shirazi anainasibisha aya hii na Mtume Mtukufu SAW na kuandika: "Wakati wakaazi wa janna wakiwa wameghiriki katika neema za janna, nuru huwaangazia kutoka juu na watasikia sauti isemayo: '"Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.” Hii ni Salamu ya Mwenyezi Mungu kwa wakaazi wa janna ambao watakuwa wamevutiwa na uwepo wa Mwenyezi Mungu kiasi cha kughafilika na yote yaliyo hapo. Kisha katika hali hiyo Malaika nao watawatumia salamu."
Moja ya mafundisho muhimu ya Uislamu na yenye baraka tele kwa mtu binafsi na jamii ni Silah-Rahim au kuwa na maingiliano mazuri na jamaa wa kaumu au familia. Moja ya nguzo muhimu za Nowruz ni jamaa katika familia kutembeleana na kujuliana hali kwa mujibu wa maamurisho ya Kiislamu ya Silah-Rahim. Katika riwaya za Kiislamu, mila na desturi hii nzuri ya Nowruz imetajwa na kupewa nafasi muhimu na imetiliwa mkazo sana. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya kustawi na kunawiri roho na kuchipua vipawa vya kifikra na kustawi mwanadamu kisakolojia hutokana na kutekeleza Silah-Rahim kupitia kutembelea waumini, jamaa na marafiki. Natija nzuri ya Sunna hii nzuri ya Mwenyezi Mungu huonekana katika sekta mbali mbali za maisha ya mtu binafsi na jamii. Kati ya manufaa ya kutembeleana au Silah-Rahim ni kupata baraka katika umri, kuondoa umasikini, kupata usahali maishani na muhimu zaidi ya yote kuleta mahaba, ukarimu na moyo wa kusaidiana waumini. Mtume SAW anasema hivi kuhusu Sunaa hii nzuri: "Kutembeleana na kukutana huleta urafiki na mahaba katika nyoyo". Aidha amesema: "Kutembeleana ndugu katika dini, kama futari na Tahajud wakati wa mwisho katika usiku, humletea furaha muumini."
Moja ya mila na desturi nyingine ya Wairani katika siku za awali za mwaka mpya wa Hijria Shamsia ni kutembelea maeneo matakatifu kwa ajili ya Ziara na pia kutembelea makaburi na kuwasomea dua waliotangulia. Kwa hakika kutembelea maeneo hayo huleta utulivu na huwa na taathira kubwa sana yenye manufaa ya kimaanawi yenye kuleta mabadiliko katika maisha ya mwanadamu mwenye kutafakari. Nchini Iran katika siku ya kwanza za Nowruz mamilioni ya wananchi wenye mahaba hutembelea maeneo ya kidini hasa Haram Takatifu ya Imam Ridha AS. Eneo hili takatifu lina ukubwa wa takribani mita milioni moja mraba na huwa limejaa waumini wenye matumaini kama ambavyo wengi pia humiminika katika Haram ya Bibi Maasouma SA mjini Qum na wengine katika Haram ya Ahmad bin Musa SA mjini Shiraz
Tunachukua fursa hii kuwatumia nyote salamu za kheri na fanaka kwa munasaba wa kuanza mwaka mpya wa Hijria Shamsia katika msimu huu wa machipuo nchini Iran. Tunawatakia nyote mwaka uliojaa umaanawi na tunamuomba Mwenyezi Mungu SWT awamiminie baraka zake tele.