Mar 30, 2016 06:40 UTC
  • Maingiliano ya Marekani na Iran  mwaka mmoja uliopita

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii itakayoangazia kwa kifupi maingiliano baina ya Iran na Marekani katika mwaka uliopita wa 1394 Hijria Shamsia.

Uhusiano wa Iran na Marekani katika kipindi cha miaka 37 iliyopita, yaani baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni uhusiano uliojaa uadui na uhasama.

Tokea uanzishwe mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani daima imekuwa ikitekeleza njama zisizo na kikomo za kuuangusha mfumo huo kuanzia kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli, kuusaidia utawala wa Kibaath wa Iraq katika vita vyake vya miaka minane vya kulazimishwa dhidi ya Iran na kupanga njama za kimataifa dhidi ya Iran kwa njia ya vikwazo n.k.

Katika miongo ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikitumia visingizio kadhaa kuiwekea Iran vikwazo vya pande zote. Kati ya visingizio hivyo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuupinga utawala wa Kizayuni, madai kuwa inaunda silaha za maangamizi ya umati, kukiuka haki za binadamu na madai kuwa Iran inajaribu kueneza mapinduzi ya Kiislamu duniani. Baada ya kuibuliwa suala la nyuklia la Iran mwaka 2003, serikali ya Marekani ilijitokeza kama mpinzani mkuu wa mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Washington imetekeleza njama kubwa za kuisakama Iran na kulipeleka faili la nyuklia la Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Marekani haikuridhika na kiwango hicho cha uhasama bali ilisonga mbele na kuiwekea Iran vikwazo vya upande mmoja mwaka 2010 ikishirikiana na waitifaki wake wa Ulaya. Vikwazo hivyo vilikuwa vikali mno kiasi cha Rais Barack Obama wa Marekani kuvitaja kuwa shahidi zaidi katika historia.

Baada ya kuingia Rais Hassan Rouhani madarakani Iran mwaka 2013, kulianza duru mpya ya mazungumzo baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ya kundi la 5+1 yaani China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani. Hapo maingiliano ya Iran na Marekani yalianza katika fremu ya mazungumzo ya nyuklia tu katika kundi la 5+1 na kwa mara ya kwanza kukafanyika mazungumzo ya ana kwa ana baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbili yaani Mohammad Javad Zarif wa Iran na John Kerry wa Marekani. Mazungumzo hayo hayakuwa na kifani katika historia ya maingiliano ya Iran na Marekani baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Baada ya duru kadhaa za mazungumzo huko Geneva, New York na Vienna baina ya Iran na kundi la la 5+1, hatimaye Marekani iliafikiana na washirika wake wa Ulaya katika kundi hilo na kupasisha mapatano ya nyuklia yaliyopewa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Mapatano hayo kimsingi yalitambua ramsi shughuli za nyuklia za Iran kwa malengo ya amani. Baraza la Usalama nalo mnamo Juni 20 2015 lilipasisha azimio nambari 2231 kuhusu utekelezwaji wa mapatano hayo ya nyuklia. Baada ya hapo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ulitoa ripoti na kuthibitisha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran hauna malengo ya kijeshi na hivyo mapatano ya nyuklia ya JCPOA yakaanza kutekelezwa. Wakala wa IAEA pia ulithibitisha kuwa Iran imetekelza ahadi zake katika mapatano ya nyuklia na hivyo kuanzia Januari 2016, vikwazo vikaanza kuondolewa hatua kwa hatua.

@@@@

Pamoja na kutatuliwa kadhia ya nyuklia ambayo ilikuwa kisingizio cha uhasama wa Marekani dhidi ya Iran, watawala wa Washington wameanzisha visingizio vipya kuishinikiza Iran.

Serikali ya Wademocrat Marekani hivi karibuni ilitangaza kuwa, hata kama imefuta au kusimamisha kwa muda baadhi ya vikwazo dhidi ya Iran lakini imesisitiza mara kwa mara kuwa kuna vikwazo ambavyo vitabakia. Tarehe 17 Januari 2016, siku moja tu baada ya kuanza kutekeleza mapatano ya nyuklia ya Iran, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo kutokana na mpango wake wa makombora ya kijihami ya balistiki.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, watu 11 ambao wanadaiwa kushiriki katika mpango wa makombora ya balistiki Iran wamewekwa katika orodha ya vikwazo vya Marekani.

Adam Szubin Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani alibainisha kuhusu kisingizio cha vikwazo vipya dhidi ya Iran na kudai kuwa, eti mpango wa makombora ya balistiki ya Iran ni tishio kwa usalama wa eneo na dunia. Aliongeza kuwa, Iran imewekewa vikwazo ili kuzuia kuimarika mpango wake wa makombora ya balisitiki. Alidai kuwa Marekani ina wasiwasi kuhusu kuimarika Iran kijeshi hasa kuhusiana na kombora la balistiki la 'Emad'.

Marekani pia imekasirika baada ya kubaini kuwa Iran ina maghala ya chini ya ardhi ya makombora ya kujihami kwani hilo linamaanisha kuwa itakuwa vigumu kuishambulia Iran kijeshi. Hii ndio sababu kuu ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vipya. Mbali na mbinu hiyo ya vikwazo, Marekani pia inatumia njia nyingine kukabiliana na uwezo wa makombora ya Iran. Serikali ya Barack Obama inashirikiana na waitifaki wake katika eneo, hasa utawala wa Kizayuni wa Israel katika kukabiliana na uwezo mkubwa wa makombora ya Iran.

Aidha Bunge la Marekani ambalo linadhibitiwa na Warepublican pia linapanga vikwazo vipya dhidi ya Iran.

Kamati ya Sera za Kigeni ya Baraza la Senate mwezi Februari ilianzisha mkakati wa kuiwekea Iran vikwazo vipya visivyo husiana na kadhia ya nyuklia. Seneta Bob Corker Mkuu wa Kamati ya Sera za Kigeni katika Baraza la Senate anashirikiana na maseneta wengine kuandaa maudhui kadhaa dhidi ya Iran kama vile majaribio ya makombora na masuala ya haki za binadamu ili kuzidi kuiwekea Iran vikwazo.

Aidha Rais wa Marekani mwezi Machi alijadidisha hali ya hatari kuhusu Iran. Ikulu ya White House imetoa taarifa ikisema kuwa baada ya Barack Obama kuidhinisha tena hali ya hatari ya kitaifa kuhusu Iran, mabunge ya Kongres na Senate yatajulishwa rasmi kuhusu uamuzi huo.

Taarifa hiyo ambayo ilitolewa tarehe 9 Machi ilisema: Pamoja na kuwepo mapatano ya nyuklia, baadhi ya hatua na sera za serikali ya Iran ni kinyume cha maslahi ya Marekani na hivyo Iran inahesabiwa kuwa tishio lisilo la kawaida kwa usalama wa taifa, sera za kigeni na uchumi wa Marekani. Kwa msingi huo kuna ulazima wa hali ya hatari kitaifa iendelee kuwepo kuhusu Iran na baadhi ya vikwazo dhidi yake

"Sheria ya Hali ya Hatari ya Kiuchumi Kimataifa" ilipitishwa mwaka 1977 katika Bunge la Kongress ya Marekani. Kwa mujibu wa sheria hiyo, rais wa Marekani anaweza kutangaza hali ya hatari ya kitaifa kufuatia tishio lisilo la kawaida la kigeni kwa usalama wa Marekani.

Hatua zinazochukuliwa katika fremu ya uamuzi huo ni kama vile kuzuia mabadilishano ya kibiashara, kufunga akaunti na kuzuia mali za nchi inayolengwa.

Kwa kutegemea sheria hii, mwezi Machi mwaka 1995 rais wa wakati huo wa Marekani, Bill Clinton alipasisha sheria ya hali ya hatari kuhusu Iran. Sheria hiyo hujadidishwa kila mwaka. Utambulisho wa kujadidishwa hali ya hatari kuhusu Iran ni sehemu ya mkakati wa Marekani wa kuhalalisha sera zake zisizo za kimantiki na za uhasama dhidi ya Iran. Kilicho wazi ni kuwa lengo la uchochezi wa sasa wa Marekani ni kwa lengo la kufikia mkakati huo wa Washington.

Wakati huo huo, kwa kuzingatia utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani na kuanza tena uhusiano wa Iran na nchi za Magharibi, nchi za eneo la kusini mwa Ghuba ya Uajemi zimekuwa zikidai kuwa na wasiwasi kuhusu hatua za Iran katika eneo. Saudi Arabia imekuwa ikiongoza kelele hizo dhidi ya Iran pamoja na kuwa yenyewe ni mhusika mkuu wa kuwasha moto wa fitina katika eneo hasa kuanzisha vita dhidi ya Yemen na kuunga mkono magaidi nchini Syria.

Mwezi Mei mwaka 2015 kabla ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya Iran, Rais Obama wa Marekani, aliwaita watawala waitifaki wa Washington wa nchi za Ghuba ya Uajemi ili kuwahakikishia uungaji mkono wake.

Katika kikao hicho cha Camp David, Marekani iliahidi kuimarisha uwezo wa makombora ya balistiki katika nchi hizo za Kiarabu ili kupunguza upinzani wa nchi hizo kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran. Aidha Marekani imeongeza kasi ya uuzaji wa silaha hatari kwa wiatifaki wake Masharikiya Kati. Mwezi Mei mwaka 2015 Obama aliwasilisha mpango wa pamoja wa nchi za Ghuba ya Uajemi na kusema Washington itaongeza idadi ya silaha inazouza katika nchi hizo.

Kwa maelezo hayo, kinyume na baadhi ya waliokuwa wakitabiri kuboreka uhusiano wa Iran na Marekani katika mustakabli wa karibu, uhalisia wa mambo ni kinyume na hilo.

Hii ni kwa sababu Marekani imeendeleza uadui na uhasama wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia imeshaanza kukiuka na kuvunja ahadi ilizotoa katika mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani. Si tu kuwa Marekani imekiuka ahadi ya kuiondolea Iran, vikwazo bali pia sasa inapitisha vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na hayo yote ni ishara ya uhasama wa Marekani dhidi ya Iran.

Pamoja na hayo serikali ya Marekani imelazimika kukiri kuhusu nafasi muhimu na isiyopingika ya Iran katika masuala ya eneo la Mashariki ya Kati. Ni kwa msingi huo ndio ikalazimika kukiri kuhusu nafasi ya Iran katika utatuzi wa mgogoro wa Syria. Hivyo Washington haikuwa na budi ila kukubali Iran kushiriki katika mazungumzo ya Geneva ya kuutatua mgogoro wa Syria.

Kwa vyovyote vile uadui wa Marekani na taifa la Iran utaendelea lakini ifahamike kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitalegeza msimamo kuhusu misimamo yake ya kimsingi.

Tags