Jul 27, 2023 03:43 UTC
  • Safari ya Rais Raisi barani Afrika ilijikita katika masuala ya sayansi na teknolojia

Katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani, tutaangazia safari ya hivi karibuni ya Rais Ebrahim Raisi barani Afrika ambapo suala la uhusiano wa sayansi na teknolojia baina ya Iran na Afrika lilipewa kipaumbele.

Katika siku za Julai 12,13 na 14, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizitembelea nchi tatu za Afrika ambazo ni Kenya, Uganda na Zimbabwe. Katika safari hiyo, Iran na nchi hizo tatu zilitiliana saini mapatano 21 katika sekta mbali mbali zikiwemo za sayansi, teknolojia na tiba.

Katika safari hiyo Rais wa Iran aliweza kushuhudia miradi ya sayansi na teknolojia ya Iran katika nchi hizo.

Kwa mfano, ndege zisizo na rubani (drone) zinazozalishwa na makampuni ya teknolojia za kisasa nchini Iran zilizinduliwa katika Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Jamhuri ya Kiislamu mjini Nairobi kwa madhumuni ya kuuzwa katika nchi hiyo na maeneo mengine ya Afrika

Kwa mujibu wa taarifa, ndege zisizo na rubani za kampuni zinazotumia maarifa za Iran, ambazo zina matumizi mawili ya "kunyunyizia" mashamba ya kilimo na pia "usimamizi wa mashamba", uchoraji ramani na kubaini iwapo kuna wadudu waharibifu wa shambani, zilizinduliwa wakati wa safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kaiislamu ya Iran mjini Nairobi Julai 12.

Rais Raisi (kushoto) na Rais Ruto

Droni hizo zilizinduliwa wakati Sayyid Ebrahim Raisi,  alipotembelea Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran (IHIT) mjini Nairobi kama sehemu ya safari yake nchini Kenya.

Ndege hiyo isiyo na rubani inayojulikana kama Pelikan 2 imetengenezwa na kampuni ya Iran, ambayo ina uwezo wa kipekee kama vile kuandaliwa kwa ajili ya kazi katika kipindi cha dakika 2, kunyunyizia hekta 2 katika kila oparesheni n.k.

Akiwa katika Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran Rais wa Iran alisema jumba hilo ni moja ya vituo vinavyoongoza katika maendeleo ya uuzaji nje wa bidhaa zinazotokana na teknolojia mpya. 

Katika kituo hicho, zaidi ya kampuni 35 za teknolojia mpya za Iran zinaonesha na kusafirisha bidhaa zao nchini Kenya katika nyanja za dawa, vifaa vya matibabu, kilimo, ujenzi n.k.

Akizungumza na waandishi habari baada ya mazungumzo yake na Rais wa Iran, Rais William Ruto wa Kenya alisema kwamba Kenya  itatumia utajiri wa Iran katika teknolojia na uvumbuzi kwa manufaa ya maendeleo yake.

Alidokeza kwamba kuanzishwa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Nairobi kutatoa jukwaa mwafaka kwa biashara za Iran na Kenya.

Aidha Rais wa Kenya alitangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itazindua kiwanda cha kisasa cha kuunganisha magari nchini Kenya.

Hali kadhalika alidokeza kuwa hati 5 za ushirikiano zilizotiwa saini baina ya nchi hizo mbili katika nyanja za tiba ya mifugo, mawasiliano, utamaduni, uvuvi na teknolojia zitakuwa na manufaa kwa nchi hiyo.

Safari ya Rais Ebrahim Raisi nchini Kenya inatathminiwa kuwa na umuhimu mkubwa katika mabadilishano ya teknolojia na nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Rais wa Iran akiwa na Rais wa Uganda

Akiendelea na safari yake barani Afrika Rais wa Iran alielekea Uganda ambapo akizungumza na Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo aliahidi kubadilishana uzoefu wa nchi yake katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na Uganda.

Wakati wa safari ya Rais Raisi nchini Uganda, Ofisi ya Ubunifu na Teknolojia ya Iran ilizinduliwa katika sherehe mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda.

Ofisi hiyo ni kitovu cha maonesho ya bidhaa zinazotokana na maarifa ya Iran nchini Uganda katika nyanja mbalimbali za chakula, kilimo, dawa, vifaa vya matibabu, chanjo za mifugo na kuku, dawa za asili, virutubisho vya chakula na ndege zisizo na rubani za kilimo.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa ofisi hii ni kuunda masoko mapya ya nje na kuanzisha bidhaa za teknolojia ya kisasa katika masoko ya Afrika, pamoja na kujenga uwanja wa kuendeleza ushirikiano wa pamoja, hasa Afrika Mashariki.

Baada ya kuondoka Uganda, Rais wa Iran alielekea Zimbabwe na kulakiwa na mwenzake, Emmerson Mnangagwa.

Katika hotuba yake, Rais Mnangagwa wa Zimbabwe aliitaka Iran kutumia fursa za uwekezaji zilizopo nchini Zimbabwe.

Alisema: "Tunakaribisha uwekezaji katika sekta kadhaa za uchumi wetu hasa madini, tuna fursa kubwa katika madini, afya, kilimo, nishati, maendeleo ya miundombinu, sayansi na teknolojia."

Katika safari hiyo, ya siku moja mikataba 12 ilitiwa saini ikiwa  ni pamoja na mipango ya kuunda kiwanda cha kutengeneza matrekta nchini Zimbabwe na kampuni ya Iran na mshirika wa ndani. Mikataba mingine ilihusi ushirikiano katika nishati, kilimo, dawa na mawasiliano ya simu pamoja na miradi ya utafiti, sayansi na teknolojia.

Akiwa ameandamana na Rais Ebrahim Raisi katika ziara barani Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian alielezea mtazamo wa Iran kwa bara hilo na matarajio ya ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu na mataifa ya Afrika.

Aliongeza kuwa "Mtazamo wa Iran kuhusu Afrika ni tofauti kabisa na ule wa ukoloni mamboleo au toleo lake la zamani." 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha alisema Iran ina azma ya kuhamisha teknolojia yake hadi Afrika na kuliwezesha bara hilo kufikia maendeleo.

Rais Raisi akiwa katika  Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Jamhuri ya Kiislamu mjini Nairobi

Wakati huo huo, Mkuu wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Taasisi ya Sayansi, Teknolojia na Uchumi cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinachohusiana na mashirika ya elimu na maarifa amesema kuwa, mchakato wa kupeleka vifaa 50 vya matibabu na zaidi ya aina 10 za dawa za Iran barani Afrika, umeanza.

Amir-Hossein Miir Abadi, Mkuu wa  Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Taasisi ya Sayansi, Teknolojia na Uchumi cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinachoshughulikia mashirika ya elimu na maarifa ametangaza habari ya kuanza zoezi hilo na kuongeza kuwa, tayari upasishaji wa kupelekwa nchini Kenya zaidi ya vifaa 50 vya matibabu na dawa aina mbili za Iran umeshafanyika. Vile vile zoezi la kupasisha usafirishaji wa aina nyingine 10 za dawa za Iran hadi nchini Kenya, limo katika utekelezaji. 

Vile vile amesema, uzalishaji wa bidhaa za kilimo, sekta ya chakula na mifugo ni miongoni mwa mambo ambayo yanahitajiwa mno na nchi za bara la Afrika.

Mkuu wa  Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Taasisi ya Sayansi, Teknolojia na Uchumi cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema, huko nchini Uganda pia kumefunguliwa maonyesho maalumu ya bidhaa za mashirika ya Iran yanayotegemea elimu na maarifa kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Jaamiatul Mustafa na kimsingi mazingira ya kuweka miundombinu ya kupelekwa nchini humo bidhaa za mashirika hayo ya Iran tayari yameandaliwa.

 

Tags