Aug 29, 2023 09:29 UTC
  • Profesa Saeed Alborz
    Profesa Saeed Alborz

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Daktari bingwa wa upasuaji ambaye ni maarufu nchini Iran kwa mara ya kwanza amefanikiwa kupata mbinu ya kutibu ugonjwa adimu wa magonjwa ya uzazi duniani.
Saeed Alborzi, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Shiraz cha Sayansi ya Tiba, alizaliwa katika mji mkuu Tehran mwaka 1956 na kukulia katika mji wa kusini wa Shiraz.
Alborzi ni mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Jumuiya ya Laparoscopy ya Iran. 
Kuhusu shughuli zake za utafiti, Alborzi alianza kufanya kazi kama mshiriki wa kitivo katika Chuo Kikuu cha Shiraz cha Sayansi ya Tiba mnamo 1988 . Akiwa kama profesa msaidizi kwa takriban miaka 10 na profesa mshiriki kwa miaka minane, sasa amekuwa profesa kamili kwa takriban miaka 20.
Daktari huyo mashuhuri alikuwa mkurugenzi wa Jumuiya ya Asia ya Endometriosis na Adenomyosis (ASEA) kutoka 2020 hadi 2022, na kwa sasa ni mjumbe wa Bodi Maalum ya ASEA. Yeye pia ndiye mwanzilishi wa taaluma ya laparoscopy na endometriosis nchini Iran.
Akizungumzia upasuaji wa tatu aliofanya kwa mara ya kwanza duniani huko Shiraz, Alborzi amesema, "Nilifanya upasuaji wa kwanza kwa kutumia peritoneum graft kujenga kizazi kwa wale ambao wana uterasi inayofanya kazi, ya kwanza ikiwa ni takriban miaka 20 iliyopita.”
Profesa ameongeza, “Ya pili ilifanyika mwaka 2008; upasuaji wa metroplasty ya Laparoscopic kwa kesi za uterasi mara mbili, ambayo makala yake ilichapishwa katika jarida la Marekani, na upasuaji wa tatu umefanywa katika miaka ya hivi karibuni, na makala yake pia kuchapishwa katika moja ya majarida ya kimataifa."
Mbinu ya Daktari Alborzi inaweza kutibu utasa kwa kiwango kikubwa na kutatua matatizo ya ujauzito.
Alborzi ameshinda tuzo nyingi na kusifiwa katika matamasha mbalimbali ya kisayansi ya kitaifa na kimataifa.
Profesa huyo mashuhuri wa Iran ameandika vitabu viwili kuhusu matibabu ya ugumba na makala zaidi ya 100, nyingi zikiwa zimechapishwa katika majarida ya kimataifa, na pia ana cheti cha cheo cha juu cha kisayansi chenye fahirisi ya juu zaidi ya H katika masuala ya magonjwa ya wanawake nchini.
Licha ya kuwa na fursa nyingi za kuhamia nchi tofauti, amekataa kuondoka Iran "kwa ajili ya upendo wa kutumikia nchi yake."

Utafiti mpya uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la Ajira Duniani, ILO umebaini kuwa matumizi ya Akili Mnemba au (Artificial Intelligence- AI) yanaongeza fursa za ajira kwa binadamu badala ya kuzisambaratisha tofauti na fikra zilizoshamiri ya kwamba matumizi ya AI yataondoka kabisa jukumu la binadamu.

Utafiti huo wa Akili Mnemba na Ajira: Uchambuzi wa kimataifa juu ya madhara ya AI kwenye idadi na aina za ajira umechapishwa karibuni na ILO huko Geneva, Uswisi ukidokeza kwamba ajira nyingi na viwanda vinakabiliwa na kiwango kidogo cha matumizi ya mashine zenye Akili Mnemba yakiwemo maroboti na kwa kiwango kikubwa itahitaji binadamu kuweko sambamba na mashine hizo badala ya fikra kwamba binadamu hatohitajika tena.

ILO ikinukuu utafiti huo imesema, “Kwa hiyo athari kubwa ya teknolojia hii inaweza kuwa sio kuondoa ajira za binadamu bali uwezekano wa mabadiliko ya ubora wa ajira, hasa kwenye kazi za mtulinga na zinazotegemea fikra za mfanyakazi.”

Utafiti huo umegundua kuwa ajira ya ukarani inaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na teknolojia ya Akili Mnemba ambapo robo ya kazi anazofanya karani zinaweza kufanywa na mashine huku zaidi ya nusu zikitegemea binadamu na mashine.

Hata hivyo kazi ya umeneja, ufundi na zenye ueledi zitaathirika kidogo mno na uwepo wa teknolojia ya AI.

Utafitu huo uliowakilisha sampuli kutoka dunia nzima umebaini tofauti kati ya nchi za kipato cha juu na cha chini ukimulika miundo ya sasa ya kiuchumi na pengo la teknolojia.

Kwa nchi za kipato cha juu ni asilimia 5.5 tu ya ajira zote itakumbwa na Akili Mnemba ilihali kwa nchi za kipato cha chini Akili Mnemba inaweza kuchukua asilimia 0.5 ya ajira.

Hata hivyo kwa upande mwingine, utafiti umegundua kuwa iwapo nchi zitakuwa na sera sahihi, mwelekeo mpya wa mabadiliko ya kiteknolojia yanaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi zinazoendelea.

Kijinsia, Akili Mnemba itaathiri zaidi ajira zinazoshikiliwa na wanawake ikilinganishwa na wanaume ambapo utafiti unaonesha kuwa hiyo inatokana na ukweli kwamba wanawake ni wengi kwenye ajira za ukarani kuliko wanaume.

Waandishi wa ripoti ya utafiti huu wanasema changamoto iliyoko sasa ni binadamu kuwa nyuma katika kuingia kwenye mpito wa teknolojia na hivyo kinachotakiwa ni binadamu kuongoza mpito huo badala ya kuchelea.

 

Na Shirika la Utafiti wa Misitu nchini Kenya (KEFRI), tawi la Lamu, liko mbioni kuunusuru na kuuhifadhi mojawapo ya miti adimu na ambayo iko kwenye hatari ya kuangamia ulimwenguni, unaojulikakana kitaalamu kama Euphorbia tanaensis.

Duniani kote, mti huo unapatikana, japo kwa uchache, kwenye msitu wa Witu, Kaunti ya Lamu pekee.

Afisa na Mwanasayansi Mtafiti wa KEFRI, tawi la Lamu,  Henry Komu, amenukuliwa na gazeti la Taifa Leo akisema mikakati kabambe inaendelezwa na ofisi yake kwa ushirikiano na mashirika mengine ya kuhifadhi mazingira pamoja na makundi ya kijamii yanayojihusisha na uhifadhi wa mazingira kuhakikisha mti huo unapandwa na kukuzwa kwa wingi Lamu.

Kulingana na Bw Komu, dhamira kuu ya juhudi hizo ni kuhakikisha idadi ya mti adimu wa Euphorbia tanaensis inaongezwa kwenye msitu wa Witu na katika maeneo mengine nchini ili usiangamie.

Juhudi za kutafiti uwepo wa mti huo na kupeana majina zilianza miaka ya 1970s kupitia Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira-asili (International Union for Conservation of Nature-IUCN).

Jukumu la IUCN ni kufuatilia juhudi zinazoendelezwa katika kunusuru miti na viumbe-asili adimu ulimwenguni.

Utafiti uliotekelezwa na muungano huo ulipelekea kugunduliwa kuwepo kwa miti minne pekee ya Euphorbia tanaensis iliyokomaa ndani ya msitu wa Witu, kaunti ya Lamu.

Euphorbia tanaensis ni miongoni mwa miti adimu 100 iliyoorodheshwa na IUCN na ambayo iko kwenye hatari zaidi ya kuangamia ulimwenguni.

Anasema juhudi za KEFRI pia zilifaulisha ukuzaji wa miche 51 ya aina hiyo ya mti kwenye misitu ya Witu katika Kaunti ya Lamu, na Arabuko-Sokoke katika Kaunti ya Kilifi mwaka 2018.

Afisa Mkuu wa Shirika la Misitu nchini Kenya (KFS) Peter Mwangi, amesema tayari wameanzisha mazungumzo na KEFRI na pia jamii kuhusiana na mti huo wa Euphorbia tanaensis akisisitiza haja ya hamasa kuuhusu mti huo kuendelea kusambazwa mashinani.

Baadhi ya watu huutumia mti huo kama dawa ya mitishamba huku wengine wakichoma magamba yake kwa lengo la kutoa moshi wa kufukuza mbu.