Sep 04, 2023 10:27 UTC
  • Sura ya At-T’uur, aya ya 41-49 (Darsa ya 964)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 964 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 52 ya At-T’uur. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 41 hadi 43 ambazo zinasema:

أَمْ عِندَهُمُ الْغَيْبُ فَهُمْ يَكْتُبُونَ

Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wanaandika?

أَمْ يُرِيدُونَ كَيْدًا ۖ فَالَّذِينَ كَفَرُوا هُمُ الْمَكِيدُونَ

Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka.

أَمْ لَهُمْ إِلَٰهٌ غَيْرُ اللَّهِ ۚ سُبْحَانَ اللَّهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ

Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametakasika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye.

Katika darsa iliyopita tuliona jinsi Allah SWT alivyowahoji wapinzani wa Bwana Mtume SAW na kuwataka waeleze ni kwa msingi gani na kwa kutegemea hoja na ushahidi gani wanamuelekezea Mtume wa Mwenyezi Mungu kila aina ya tuhuma. Katika muendelezo wa masuali hayo, aya hizi tulizosoma zinasema: Kwani hawa wapinzani wanaweza kudai kwamba wao wenyewe wana mawasiliano na ulimwengu wa ghaibu na wanapokea moja kwa moja wahyi na kwa hivyo hawana haja ya maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo amemletea Mtume wake?! Au ni kwamba, wameamua tu kupanga na kula njama za kumdhuru Mtume wa Allah, ilhali inawapasa wao wajue kuwa, wao wenyewe wanaongozwa na irada ya Mola, na hizo njama zao wanazopanga madhara yake yatawarudia wenyewe! Kama wao wametegemea nguvu bandia za wanaowaitakidi kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu wajue kwamba, hao wanaowategemea hawana uwezo wa kuwanusuru wala kuwasaidia kwa lolote mbele ya qudra na nguvu za Allah SWT. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mojawapo ya mbinu za kuwalingania na kuwaelimisha watu wapotofu ni kuwatupia masuali kadhaa kwa ajili ya kuwazindua na kuwashajiisha watafakari na kutaamali juu ya mambo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ghairi ya Mitume na mawalii wa Allah, mtu mwingine yeyote yule anayedai kuwa na mawasiliano na ulimwengu wa ghaibu, dai lake hilo halina mashiko yoyote ya kielimu wala ya kukubalika kiakili; na maneno yake hayo ni batili. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mwenyezi Mungu ni mlinzi na mtetezi wa waja wake waumini na wenye msimamo thabiti; na popote inapolazimu, huchukua hatua ya kuzima njama za maadui dhidi ya waja wake hao.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 44 hadi 46 ambazo zinasema:

وَإِن يَرَوْا كِسْفًا مِّنَ السَّمَاءِ سَاقِطًا يَقُولُوا سَحَابٌ مَّرْكُومٌ

Na hata wange ona pande la mbingu linaanguka wange sema: Ni mawingu tu yaliyo bebana. 

فَذَرْهُمْ حَتَّىٰ يُلَاقُوا يَوْمَهُمُ الَّذِي فِيهِ يُصْعَقُونَ

Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakayoangamizwa.

 يَوْمَ لَا يُغْنِي عَنْهُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ

Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa.

Aya hizi zinabainisha upeo wa ukaidi na ufidhuli wa wapinzani na wakanushaji wa haki kwa kueleza kwamba, ikiwa adhabu ya Mwenyezi Mungu itateremshwa kutoka mbinguni kwa sura ya pande la jiwe, basi wao wataikadhibisha hiyo pia na kusema: haya ni mawingu tu ya angani yaliyotuama na kuporomoka kwa sura hii. Wao hawakanushi ukweli wa kiroho na kimaanawi pekee bali wanapotosha hata hakika na ukweli wanaoweza kuuhisi na kuuona kwa macho yao ili tu wapate njia ya kumkanusha Allah SWT. Kwa hivyo aya zinaendelea kumhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: wewe waache hawa watu kama walivyo waendelee na mambo yao. Si kwamba wamelala hata uhitaji kuwaamsha. Ni watu waliojifanya tu kuwa wamelala; kwa hivyo, vyovyote utakavyojaribu kufanya hawatazinduka. Ni mauti na maangamizi tu ndiyo yatakayowaamsha, lakini uzindukaji huo hautawafalia kitu wakati huo. Isitoshe, mpango na njama yao ya kuizima haki na kuifuta dini ya Mwenyezi Mungu hautawasaidia kwa namna yoyote ile na hawatapata chochote kile cha kuwaokoa. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, ubishi na ukaidi hupofua macho yaliyoko kwenye kichwa cha mtu yakashindwa kuuona ukweli wa kimaada, seuze kuukubali ukweli wa kiroho na kimaanawi ambao inapasa uonekane na kukubaliwa na macho ya moyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mwongozo na mafundisho ya uongofu yanayotolewa na Mitume ni kwa ajili ya watu wenye kiu ya kuujua ukweli na haki, si kwa walioamua kuifanyia haki inadi, ubishi na ukaidi. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, wapinzani huwa hawapangi wala hawafikirii katika mahesabu yao suala la wao kuangamizwa na kutoweka. Hujidhani kuwa wao watabaki milele na wataweza kupanga na kutekeleza mipango na njama zao, hali ya kuwa wakati wowote atakapotaka Allah, mauti na maangamizi yatawapata watu hao na njama zao zitayoyoma na kutoweka.

Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 47 hadi 49 za sura yetu ya At-T'uur ambazo zinasema:

وَإِنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا عَذَابًا دُونَ ذَٰلِكَ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ

 Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hiyo, lakini wengi wao hawajui.

  وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ

Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumhimidi Mola wako Mlezi unapo simama,

 وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَإِدْبَارَ النُّجُومِ 

Na usiku pia msabihi, na zinapo kuchwa nyota. 

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu kuteremshwa adhabu kwa wakanushaji wabishaji na wenye inadi kwa kusema: adhabu ya Mwenyezi Mungu haihusiani na akhera pekee, bali inaweza kuwashukia watu hao hata hapa duniani na katika barzakhi pia; lakini kwa kuwa wao hawajui chochote kuhusu wahyi, hawana habari juu ya jambo hilo na wala hawafikirii kuzirekebisha nafsi zao na kujinusuru na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Katika sehemu ya mwisho ya aya hizi, -ambazo ndizo aya za mwisho za Suratu-T'uur-, na baada ya kubainishwa aina mbalimbali za tuhuma na njama za maadui, Allah TWT anamwambia Mtume wake ya kwamba: ili uweze kulitekeleza jukumu tulilokupa la Utume, kuwa imara na thabiti. Sisi tunaendelea kukuongoza na kukulinda na wala hatujaghafilika nawe hata kwa lahadha moja, hata tukuwache peke yako mwenyewe na mambo yako. Lakini ili kuweza kujijenga kiroho, inakupasa udumishe mawasiliano yako na Allah na uwe ukimhimidi na kumsabihi Yeye kutwa kucha, asubuhi na jioni; kufanya hivyo kutakuondolea dhiki ya kuwa mhitaji kwa watu na kukuunganisha na chemchemi na chanzo kikuu cha qudra na adhama, ambacho ni Allahu Jalla fii Ulaahu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, madhalimu hawajui chochote kuhusu mwisho wa matendo yao maovu, si hapa duniani wala huko akhera; vinginevyo wasingekuwa wakifanya wanayoyafanya. Kwa maneno mengine ni kwamba, wasingeendelea kuzidhulumu nafsi zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika kuilinda dini ya Allah, inatupasa tuwe thabiti na imara katika kukabiliana na wapinzani wakaidi na wenye inadi na tuwe na subira na uvumilivu wa kuhimili na kustahamili masaibu na misukosuko itakayotufika katika njia hiyo. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kama mtu atakuwa na imani ya yakini kuwa Allah SWT anawaona na anawapa auni na msaada wake wale wanaojitolea nafsi zao na kufanya juhudi katika njia yake, subira na ustahamilivu wa mtu huyo utaongezeka na hatoacha katu kuendeleza juhudi zake katika njia ya haki. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, dua na kunong'ona na Allah na kumdhukuru Yeye Mola kwa ulimi vina taathira kubwa katika kuufanya moyo na akili ya mtu iwe imara zaidi kiimani kwa ajili ya kutekeleza amri za Allah SWT. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 964 ya Qur'ani imefikia tamati; na ndiyo inayotuhitimishia pia tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 52 ya At-T'uur. InshaaLlah tuwe tumeaidhika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah, atughufirie madhambi yetu, azifanye thabiti imani zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

 

 

 

 

Tags