Sep 26, 2023 06:51 UTC
  • Sura ya Annajm, aya ya 43-62 (Darsa ya 968)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 968 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 53 ya An-Najm. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 43 hadi 49 ya sura hiyo ambazo zinasema:

وَأَنَّهُ هُوَ أَضْحَكَ وَأَبْكَىٰ

Na kwamba Yeye ndiye anaye leta kicheko na kilio.

 وَأَنَّهُ هُوَ أَمَاتَ وَأَحْيَا

Na kwamba Yeye ndiye anaye fisha na kuhuisha. 

وَأَنَّهُ خَلَقَ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ

Na kwamba Yeye ndiye aliye umba jozi, dume na jike.

مِن نُّطْفَةٍ إِذَا تُمْنَىٰ

Kutokana na mbegu ya uzazi inapo miminwa.

وَأَنَّ عَلَيْهِ النَّشْأَةَ الْأُخْرَىٰ

Na kwamba ni juu yake ufufuo mwengine.

وَأَنَّهُ هُوَ أَغْنَىٰ وَأَقْنَىٰ

Na kwamba ni Yeye ndiye anaye tosheleza na kutajirisha.

وَأَنَّهُ هُوَ رَبُّ الشِّعْرَىٰ

Na kwamba hakika Yeye ndiye Mola Mlezi wa nyota ya Shii'ra. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoonyesha jinsi mamlaka ya utawala wa Allah TWT yalivyokienea kila kitu, namna Yeye Allah alivyo Mola Mlezi wa ulimwengu wote na kwamba hatima ya kila jambo inaishia kwake Yeye Mola Muumba aliyetukuka. Baada ya maelezo hayo, aya hizi tulizosoma zinataja mifano mingine ya mambo yaliyo kwenye mamlaka ya Allah SWT na kueleza kwamba: uhai na mauti yenu nyinyi wanadamu pamoja na viumbe vingine vyote yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamkuja kwenye hii dunia kwa irada na kutaka nyinyi wenyewe; na ni Yeye ndiye atakayekuondoeni hapa duniani. Kucheka na kulia, ambazo ni miongoni mwa sifa maalumu na za kipekee zinazowapambanua wanadamu na viumbe vingine vyenye uhai, amekujaalieni Yeye Mola katika nafsi na maumbile yenu ili muweze kudhihirisha hisia zenu za furaha na majonzi na za mguso na mwathiriko wa ndani ya nyoyo na kuishi maisha yaliyotawaliwa na uchangamfu na harakati. Na ni Yeye Allah pia ambaye amekuumbeni katika jinsia ya dume na jike ili kizazi chenu na vizazi vya viumbe vingine viendelee kuwepo duniani. Ameweka mfumo wa viumbe kuzaliana na kuongezeka kutokana na tone la mbegu hafifu, ambayo baada ya muda mfupi hubadilika na kuzaliwa kiumbe kamili. Na ni Yeye Allah pia, ambaye baada ya ulimwengu huu, amekuwekeeni ulimwengu mwingine ili mjue kwamba yale mtakayoyapanda kwa matendo na amali zenu hapa duniani, mtakwenda kuyavuna huko akhera Siku ya Kiyama; na hakuna lolote alifanyalo mja ila atalipwa kwalo. Na ni Yeye Allah SWT pia ndiye anayekuneemesheni kwa mali na utajiri kupitia biashara na uzalishaji mkaweza kujikidhia mahitaji yenu na kuendesha maisha yenu. Na si ardhi pekee na wakazi wa ardhini, bali hata mbingu na nyote zote, ziwe zile mnazozijua kwa majina yao au msizozijua, zote hizo Muumba na Mola wao ni yeye Allah SWT. Kama ni hivyo, ni kwa sababu gani mnawaendea wengine ambao mnawaitakidi na kuwafanya washirika wa Mwenyezi Mungu kwa kuwaadhimisha na kuwanyenyekea? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, asili na chimbuko la kila kitu linatokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu, hata kama vitu hivyo vitaonekana kidhahiri kuwa na mgongano, kwa sisi wanadamu kukihisi kimoja kizuri na cha kheri, na kingine kibaya na cha shari; kama uhai na mauti au kicheko na kilio. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mfumo wa jozi, yaani kuwepo dume na jike katika viumbe, ambao ndio unaowafanya waendelee kuwepo ni miongoni mwa maajabu ya kustaajabiwa ya ulimwengu huu na ni mojawapo ya alama za tadbiri na hekima za Mwenyezi Mungu Mtukufu katika uendeshaji wa ulimwengu. Halikadhalika aya hizi zinatutahadharisha kuwa tusizichukulie mali na utajiri wowote tulionao kuwa ni vitu vinavyotokana na sisi wenyewe, kwa sababu chochote anachokizalisha au kukitengeneza mwanadamu kinatokana na malighafi aliyoiumba Mwenyezi Mungu pamoja na akili na uelewa, ambao Yeye Mola Mwenyezi amemjaalia kiumbe huyo.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 50 hadi ya 55 ambazo zinasema:

وَأَنَّهُ أَهْلَكَ عَادًا الْأُولَىٰ

Na kwamba Yeye ndiye aliye waangamiza A'di wa kwanza,

 وَثَمُودَ فَمَا أَبْقَىٰ

Na Thamudi hakuwabakisha,

وَقَوْمَ نُوحٍ مِّن قَبْلُ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا هُمْ أَظْلَمَ وَأَطْغَىٰ

Na kabla yao kaumu ya Nuhu. Na hao hakika walikuwa ni madhaalimu zaidi, na waasi zaidi;

 وَالْمُؤْتَفِكَةَ أَهْوَىٰ

Na miji iliyo pinduliwa, ni Yeye aliye ipindua.

فَغَشَّاهَا مَا غَشَّىٰ

Vikaifunika vilivyo funika.

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكَ تَتَمَارَىٰ

Basi neema gani ya Mola wako Mlezi unayo ifanyia shaka? 

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa na aya zilizotangulia kuhusu mamlaka na umiliki wa Mwenyezi Mungu juu ya ulimwengu na kiumbe mwanadamu na kueleza kwa kuhoji: kwa nini makafiri na madhalimu hawajifunzi na kupata ibra kutokana na kaumu zilizopita? Kwani hawajui kama baadhi ya staarabu kubwa kubwa ziliangamizwa kutokana na dhulma, madhambi na kuasi kwao na hakuna tena athari yao yoyote iliyosalia? Kaumu kama za akina Aad na Thamudi na pia kaumu ya Nuh na Lut AS, zote hizo ziliasi na kuukufuru wito waliolinganiwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu wa kushikamana na Tauhidi na njia ya uokovu. Matokeo yake, walishukiwa na adhabu ya Allah papa hapa duniani na wote wakaangamizwa isipokuwa wachache tu miongoni mwao waliokuwa waja wema walioiamini na kuifuata haki. Ni ukweli kwamba baadhi ya watu madhalimu na waliokufuru hufurutu mpaka katika utovu wao wa shukurani wakafikia hadi ya kuzisahau neema za kiroho na kimaada wanazojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Watu wa aina hiyo hughariki kwenye lindi la maasi na dhulma mpaka ikalazimu waionje, kwa kuteremshiwa papa hapa duniani, adhabu waliyokuwa wameandaliwa huko akhera. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, kwa kutalii na kusoma historia za waliotangulia, tunatakiwa tujifunze na kupata somo kutokana na hatima mbaya iliyowafika watu hao, ili nasi pia tusije tukafuata njia yao ya kumwasi na kumkufuru Mola wetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, adhabu za Allah hazikuwekwa kwa ajili ya akhera tu. Katika baadhi ya hali, madhalimu hulipwa papa hapa duniani malipo ya maovu wayatendayo na dhulma wazifanyazo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, dhulma na uonevu dhidi ya watu, na kumkufuru na kumwasi Allah SWT ndizo sababu zilizopelekea kuangamizwa kaumu zilizopita.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 56 hadi ya 62 ya sura yetu ya An-Najm ambazo zinasema:

هَٰذَا نَذِيرٌ مِّنَ النُّذُرِ الْأُولَىٰ

Huyu (Mtume) ni mwonyaji miongoni mwa waonyaji waliopita.

 أَزِفَتِ الْآزِفَةُ

Kiyama kimekaribia! 

 لَيْسَ لَهَا مِن دُونِ اللَّهِ كَاشِفَةٌ

Hapana wa kuondoa (uzito wa siku hiyo) isipo kuwa Mwenyezi Mungu. 

أَفَمِنْ هَٰذَا الْحَدِيثِ تَعْجَبُونَ

Je! Mnayastaajabia maneno haya?

وَتَضْحَكُونَ وَلَا تَبْكُونَ

Na mnacheka, wala hamlii? 

وَأَنتُمْ سَامِدُونَ

Nanyi mmeghafilika? 

فَاسْجُدُوا لِلَّهِ وَاعْبُدُوا

Basi msujudieni Mwenyezi Mungu, na mumuabudu.

Aya hizi, ambazo ndizo aya za mwisho za Suratu-Nnajm zinawahutubu kwa lugha ya kuhoji watu waliojisahau na wakaingiwa na ghururi kwa kuwaambia: inakuwaje mnayapuuza maonyo na indhari za Mitume wa Mwenyezi Mungu kuhusu kuhudhurishwa kwenye kisimamo cha Kiyama na kwenda kuwajibika kwa mliyoyatenda duniani, na kulichukulia hilo kuwa ni jambo baidi kutokea na lisiloingia akilini? Hali ya kuwa mauti yanakukaribieni; na baada ya kifo Kiyama ndicho kitachofuatia!? Kwa hakika dunia imekushughulisheni mpaka mumeghafilika na kuisahau akhera! Badala ya kuzililia na kuzifikiria nafsi zenu mnaangua vicheko; mnazifanyia shere na stihzai imani na itikadi za walioamini na kuwatazama wao kwa jicho la kedi na dharau. Aya ya mwisho ya sura hii ya An-Najm inabainisha kuwa njia ya uokovu na ya kumnusuru mtu na ghururi na hali ya kujisahau, ni kuonyesha khudhuu na unyenyekevu kwa Allah SWT na kujiweka mbali na kila aina ya shirki katika kumwabudu Yeye Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tusikidhanie Kiyama kuwa ni kitu kilicho mbali. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, kama tunaipa uzito kweli nusra na uokovu wa nafsi zetu, basi tuanze sasa hivi hapa duniani kuzifanyia kazi njia za kupatia uokovu huo, kwa sababu huko akhera tunakoelekea hakutakuwa na njia wala lolote tutakaloweza kufanya ili tuokoke. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kilio hakihusiani na mambo ya duniani tu. Mawalii wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakilia na kumwomba Mola maghufira kila walipokuwa wakiwaza na kufikiria vipi zitakuwa hali zao Siku y Kiyama. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 968 ya Qur'ani imefikia tamati; na ndiyo inayotuhitimishia tarjumi na maelezo ya sura ya 53 ya An-Najm. InshaaLlah tuwe tumeaidhika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah atufishe katika Uislamu na imani sahihi ya Tauhidi, atufufue akiwa ametughufiria dhambi zetu na aijaalie Pepo yake ya milele yawe ndio makazi yetu. Wassalamu Walaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags