Jul 04, 2016 06:20 UTC
  • Jumatatu, 04 Julai 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 28 Ramadhani mwaka 1437 Hijria sawa na 4 Julai 2016.

Siku kama ya leo miaka 1165 iliyopita aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani. Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri sana wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawaliid as-Saghirah.

Siku kama ya leo miaka 240 iliyopita wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini tangazo la uhuru wa nchi hiyo huko katika mji wa Filadelphia. Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa milki ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 Miladia wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la Marekani.

Miaka 34 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo wanadiplomasia watatu na mwandishi habari mmoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walitekwa nyara na wapiganaji wa chama cha Falanja cha Lebanon kaskazini mwa Beirut. Wanadiplomasia hao na mwandishi wa habari wa Iran walitekwa nyara wakati walipokuwa wakielekea kazini katika ubalozi wa Iran mjini Beirut. Wakati tukio hilo lililopijiri jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilikuwa limeishambulia Lebanon na chama cha Falanja kilikuwa na ushirikiano wa karibu na utawala huo ghasibu. Awali ilisemekana kuwa Sayyid Muhsin Musawi, balozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Beirut na wenzake walikwishauawa, lakini ushahidi na nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa raia hao wa Iran wanashikiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Licha ya kuwa Iran imefanya jitihada kubwa za kutaka kurejeshwa wanadiplomasia wake hao wanaoshikiliwa na utawala wa Kizayuni lakini utawala huo haujatoa jibu lolote na hata taasisi za kimataifa pia zimeshindwa kutoa msaada wa maana katika uwanja huo.

Na tarehe nne Julai mwaka 2010 Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulamaa mashuhuri na marja taqlidi wa Waislamu wa Lebanon alifariki dunia. Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji wa mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Allama Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Hauza ya kielimu ya mji wa Najaf tangu akiwa kijana. Msomi huyu mkubwa alijishughulisha na masuala ya kutwalii makala na kuandika vitabu na alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisi harakati ya kisiasa huko Iraq iliyojulikana kwa jina la "Hizbul Da'awa al Islamiya". Mwaka 1966 baadhi ya wananchi na maulamaa wa Lebanon walimwalika nchini humo Allama Fadhlullah na akiwa huko alifanya kazi kubwa za kielimu, kiutamaduni na kijamii, shughuli ambazo athari zake zinaendelea kushuhudia hadi leo hii. Allama Muhammad Hussein Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na harakati ya Muqawama wa kiislamu ya Lebanon Hizbullah na sababu hiyo ndiyo iliyokuwa ikizikasirisha Marekani na utawala wa Kizayuni na kupelekea kiongozi huyo kukoswakoswa kuuawa kwa mara kadhaa. Ayatullah Sayyid Muhammad Husseinn Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani yenye juzuu 25 kwa jina la "Min Wahyil Qur'an."