Dec 01, 2023 09:52 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (36)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuhu. Wasikilizaji wapenzi, hii ni sehemu ya 36 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 36.

Wapenzi wasikilizaji, katika Hikma ya 31 ya Nahjul Balagha, Imam Ali (AS) ameelezea nguzo za imani. Kwa kuzingatia umuhimu wa suala la imani na wajibu wa kuwa na ufahamu mzuri kuhusu hikma hii, tumeamua kuizungumzia na kuichambua katika vipindi sita mfululizo hii ikiwa ni sehemu ya sita na ya mwisho ya kuichambua hiyo hikma ya 31 ya Nahjul Balagha. Leo tutazungumzia nguzo ya shaka kama ilivyotajwa na Imam Ali AS kwenye hikma hiyo.

Katika Hikma 31, Imam Ali AS baada ya kuelezea kwa balagha ya hali ya juu sababu zinazopelekea mtu kuingia kwenye ukafiri, anaendelea kufafanua hikma hiyo ya 31 kwa kuzungumzia matawi ya shaka. Anasema:

وَالشَّکُّ عَلَى أَرْبَعِ شُعَب: عَلَى التَّمَارِى، وَالْهَوْلِ، وَالتَّرَدُّدِ، وَالاْسْتِسْلاَمِ

Na shaka inatokana na mambo manne: Kuwa na tabia ya kujihusisha na mijadala isiyo na faida iliyochanganyika na ubishi. Pili, kuogopa kufanya uchunguzi na utafiti. Tatu; kujitia wasiwasi usio na maana na mwisho kuvunjika moyo, kusalimu amri na kujidunisha mbele ya mambo ya shubha na kuishia kwenye kuchukua maamuzi ya pupa

Shaka ni miongoni mwa mambo yanayoharibu dini na imani ya mtu. Tab'an, shaka ambayo inakuza mawazo na kumfanya mtu apate nguvu za kufanya utafiti, ni nzuri sana na inakubaliwa na kusifiwa kwani huwa sababu ya kutia nguvu itikadi na imani ya mtu. Lakini shaka ambayo iko mbali na misingi ya kiakili na kimantiki, ambayo inamsukuma mtu kwenye upotofu, hupelekea kupoteza mtu dini na dunia yake. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Imam Ali AS katika kubainisha na kutoa ufafanuzi kuhusu hikma hii iliyojaa busara na balagha akaanza kwa kuonesha chanzo cha shaka na baada ya hapo akatoa ufafanuzi kuhusu tawi moja baada ya jingine. Anaendelea kwa kusema:

فَمَنْ جَعَلَ الْمِرَاءَ دَیْدَناً لَمْ یُصْبِحْ لَیْلُهُ

Mtu mwenye tabia ya kuingia kwenye mijadala isiyo na maana, hufunikwa na kiza cha shaka na kumzuia kuiona nuru. Mtu huyo muda wake wote huwa ni usiku usiopambazuka. Na sababu yake ni kuwa, mtu anapokuwa mbishi na kujiingiza kwenye mijadala isiyo na tija, moyo wake hutekwa na taasubu ya kile anachokitetea na huwa mbali na ilmu na yakini na hilo kwa hakika ni pazia hatari linalomzuia kuifikia haki. 

Amma kuhusu vitawi vya pili na vya tatu vya watu wa shaka, Imam anavitolea uchambuzi vitawi hivyo akisema:

وَمَنْ هَالَهُ مَا بَیْنَ یَدَیْهِ نَکَصَ عَلى عَقِبَیْهِ وَ مَنْ تَرَدَّدَ فِی الرَّیْبِ وَطِئَتْهُ سَنَابِکُ الشَّیَاطِینِ

Mtu anayeongopa kuukiri ukweli ulioko mbele yake na kujizuia kuchukua maamuzi sahihi, huporomoka na kugeuka mgongoni kwake na yule ambaye anasitasita na kutoitumia vizuri akili yake katika kuchukua maamuzi na akawa mwingi wa wasiwasi na atiati katika mambo yake, husagwasagwa chini ya kwato za shetani.

Imam Ali AS anasema kuwa, wasiwasi na shaka zisizo na maana ni kazi ya shetani na humwangamiza aliye nazo. Kila mmoja ameiona hali hiyo kwa watu wenye wasiwasiwasi. Watu wenye wasiwasi kamwe hawawezi kuchukua maamuzi sahihi na ya wazi katika masuala muhimu kama ya wakati wa ibada. 

Mwishoni mwa hikma ya 31, Imam Ali AS anasema:

وَمَنِ اسْتَسْلَمَ لِهَلَکَهِ الدُّنْیَا وَالاْخِرَهِ هَلَکَ فِیهِمَا

“Mwenye kusalimu amri mbele ya maangamizo ya duniani na Akhera na asipambane kujiweka mbali na shubha na maangamizo hayo, basi huangamia humo. Ataangamia katika yote mawili, maangamizi ya duniani na maangamizi ya Akhera. Tunajua kwamba mashetani majini na watu hujaribu kuwatia shaka binadamu katika imani zao za kidini ili kuwaburuta motoni pamoja nao. Watu wenye imani dhaifu, woga na wasio na misimamo huwa ni kama manyoya na majani makavu yanayopeperushwa huku na kule na upepo. Huwa wanashindwa kuchukua maamuzi sahihi na wanashindwa kushikamana na itikadi sahihi wala hawawezi kufuata njia iliyonyooka.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags