Feb 27, 2024 09:51 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (42)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 42 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 42 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 38.

یَا بُنَیَّ، احْفَظْ عَنِّی أَرْبَعاً، وَأَرْبَعاً، لاَ یَضُرُّکَ مَا عَمِلْتَ مَعَهُنَّ

Mwanangu kipenzi! Nihifadhie mambo manne na mambo manne. Utakapoyafanyia kazi mambo hayo, hutodhurika maadamu utayafanyia kazi mambo hayo.

Katika hikma hii ya thelathini na nane ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatupatia hazina nane zenye thamani kubwa mno kwa kutumia maneno mafupi yaliyojaa hikma. Ingawa nasaha hizi muhimu Imam Ali AS alizitoa kwa mwanawe yaani Imam Hasan al Mujtaba AS, lakini wazi kwamba ni nasaha zinazowahusu wanadamu wote. Katika nasaha hizi Imam anasema: Ewe wanangu, nilindeni mambo manne na mambo manne. Ukishikaana nayo hutodhurika. Mambo hayo ni zawadi kutoka kwangu, hakuna madhara yatakayokupata iwapo utashikamana nayo.

 

Amma kitu cha kuzingatia hapa kabla ya jambo lolote ni kwamba, katika hikma hii, Imam hakusema nakuusia mambo maneno, bali amesema nakuusia mambo manne na mambo manne! Wafasiri na wachambuzi wa Nahjul Balagha wanasema: Hikma ya Imam Ali AS hapo katika kubainisha kwa sura hiyo ni kwamba alitaka kuonesha kuwa, kuna tofauti baina ya mambo manne ya kwanza na mambo manne ya pili. Na hivyo ndivyo yanavyoonesha mafungu hayo mawili ya mambo manne manne. Fungu la kwanza linahusiana na kuijenga mtu mwenye nafsi yake kimaadili na fungu la pili linahusiana na mlahaka na tabia za mtu kwa wengine. Vile vile mambo manne ya kwanza yanahusiana na maamrisho na fungu la mambo manne ya pili linahusiana na makatazo.

Mwanzo kabisa Imam Ali anazungumzia thaani kubwa ya akili akisema: Hapo mwanzoni, Imam alitaja baraka ya akili na akasema: إِنَّ أَغْنَى الْغِنَى الْعَقْلُ Mwanangu! Utajiri bora kabisa ni akili.

Akili katika maana yake ya asilli kabisa ni kuzuia na kudhibiti kitu. Neno akili katika lugha ya Kiarabu linatokana na neno ‘Iqal lenye maana ya kamba ambayo hufungwa gotini ngamia muasi ili kudhibitiwa na asitetereke. Hivyo neno akili limetumika kwa sababu inamzuia mtu kufuata hawaa za nafsi na kumuwezesha kudhibiti hisia za kishetani.  

Mtu mwenye akili ni tajiri kimaanawi na kimaada. Kwa maneno mengine ni kwamba, mtu huyo hupata mafanikio ya duniani na ya Akhera pia. Mtu mwenye akili huelewa vyema kwamba maisha si mepesi kuweza kuyaendesha peke yake. Hivyo hujiwekea mikakati na tadibiri za kushirikiana vizuri na wengine na kutumia akili yake ipasavyo kumaizi nani ni rafiki mzuri na nani ni rafiki mbaya. Mwenye akili huzidiriki vizuri fursa na kutumia ipasavyo nishati ya wenzake katika maisha yake ya kimaada. Katika upande wa kimaanawi pia, akili humuongoza mtu kumtambua Mungu wa kweli na kujipamba kwa akhlaki bora na matendo mazuri kwa sababu akili yake inamfundisha madhara makubwa ya tabia mbaya na inamdhibiti asijipambe nazo.

 

Katika hadithi nyingine iliyopokewa kutoka kwa Imam Ali AS ananukuliwa akisema: Mwenyezi Mungu ameweka ndani ya Malaika akili isiyo na matamanio, na ameweka katika wanyama matamanio yasiyo na akili, na amewe katika wana wa Adam; mambo yote mawili, akili na matamanio. Kwa hiyo, mwenye akili ya kushinda matamanio yake, basi huyo ni mbora kuliko Malaika, na yeyote ambaye matamanio yake yanashinda akili yake, huyo ni duni kuliko wanyama.

Kwa hivyo, ikiwa tunataka kutoa ufafanuzi wa mwanadamu, tunaweza kusema; mwana wa Adam ni kiumbe ambaye ana akili na matamani, lakini kuwepo kwa nguvu hizi mbili kunahitaji nguvu ya tatu, ambayo ni nguvu ya maamuzi na kuchagua njia gani sahihi. Kila kitu kinategemea maamuzi na chaguo la mwanadamu mwenyewe. Anaweza kufuata kwa uhuru imma akili yake au matamanio ya nafsi yake. Kwa hiyo, kiwango cha thamani ya mwanadamu kinachoweza kumweka katika nafasi ya juu zaidi kuliko Malaika ni utashi wake wa kimantiki, na kinachosababisha mwanadamu kuwa kiumbe muovu kabisa na kumuweka daraja ya chini kuliko hata mnyama, ni maamuzi yake ya kufuata hawaa na matamanio mabaya ya nafsi yake. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Imam Ali AS akasema kuhusu suala hili muhimu sana kwamba: "Hadhi na thamani ya kila mwanadamu inatokana na hikma na kutumia kwake vizuri akili yake.”

Tags