Apr 07, 2024 04:20 UTC
  • Jumapili tarehe 7 Aprili 2024

Leo ni Ijumaapili ya Mwezi 27 Ramadhani mwaka 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Aprili 2024 Miladia.

Miaka 885 iliyopita katika siku ya mwezi 27 Ramadhani mwaka 560 Hijria, alizaliwa huko Andalusia kusini mwa Uhispania ya leo Muhyiddin Abu Bakr bin Muhammad, maarufu kama Ibn Arabi, alimu mkubwa na Aa'rif wa Kiislamu. Akiwa na umri wa miaka minane, Ibn Arabi alielekea Seville, moja ya miji mashuhuri ya Andalusi,a alikosoma Quran, Fiqhi na Hadithi. Ibn Arabi alianza pia kusomea irfani na kujijenga kiroho tangu akiwa kijana mdogo. Alikuwa na umri wa miaka 30 alipoelekea katika nchi nyingine za Kiislamu ili kujifunza zaidi elimu na taaluma nyinginezo, lakini bila kughafilika na kualifu vitabu hata alipokuwa safarini. Ibn Arabi aliishi Damascus kuanzia mwaka 620 na akaanza kufundisha na kuandika vitabu. Mwanachuoni na Aa'rif huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi, miongoni mwao tunaweza kutaja Al-Futuuhatul-Makkiyya, Fusuusul-Hikam na Al-Mabaadii wal-Ghaayaat. Ibn Arabi alifariki dunia huko Damascus mwaka 638 Hijiria.

Ibn Arabi

Miaka 335 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwezi 27 Ramadhani mwaka 1110 Hijria, Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu, alifariki dunia. Alimu huyo aliandika na kukusanya athari nyingi, vikiwemo vitabu muhimu zaidi vya marejeo kwa Waislamu. Allamah Majlisi alikuwa na nafasi ya juu ya umahiri katika taaluma za dini na ukusanyaji wa Hadithi na uandishi wa vitabu katika nyuga za elimu za dini. Wakati wa uhai wake, mwanachuoni huyo mashuhuri alifanya juhudi nyingi sana katika kusimamia Sala ya Ijumaa na za jamaa, kuanzisha madrasa za kidini na kueneza Hadithi za Mtume SAW na Ahlu Bayt zake. Imeelezwa kuwa idadi ya vitabu alivyoalifu Allamah Majlisi ni zaidi ya majalada 600, na mashuhuri zaidi kati yao ni Bihaarul-Anwar. Kitabu hiki ni majimui ya habari na Hadithi zilizoandikwa kwa lugha ya Kiarabu ambazo Allamah Majlisi alikuwa amezikusanya kwa miaka mingi. Athari nyingine za mwanachuoni huyu mkubwa wa Kiislamu ni  A'inul-Hayaat, Hayaatul-Quluub na Zaadul-Ma'ad.

Muhammad Baqir Majlisi

Miaka 303 iliyopita, mnamo tarehe 7 Aprili 1721, Mfalme wa Urusi Peter the Great aliishambulia kijeshi Sweden. Kuanzia mwaka 1700, Urusi na Sweden pamoja na Poland na Denmark, zilitumbukia kwenye vita vya kaskazini. Wakati jeshi la Urusi lilipoivamia Sweden, nchi hiyo ilikuwa imefanya suluhu na nchi zingine ilizokuwa ikipigana nazo na ikawa imepanga kufanya suluhu na Urusi pia; lakini Peter the Great, ambaye alitaka kujipanulia maeneo ya ardhi, alilishambulia na kulishinda jeshi la Sweden kwa jeshi lake lililojiandaa kwa vita na kujizatiti kwa silaha na kuilazimisha nchi hiyo kusaini mkataba wa suluhu ilioutaka. Kwa mujibu wa mkataba huo, maeneo kadhaa ya ardhi ya Sweden pamoja na Finland, iliyokuwa inakaliwa na nchi hiyo, yakakabidhiwa kwa Urusi. Kwa njia hiyo, nguvu za Sweden zikapungua sana na mkabala wake, Urusi ikageuka kuwa dola lenye nguvu kubwa barani Ulaya.

Peter the Great

Miaka 135 iliyopita mnamo Aprili 7, 1889, Bi Gabriela Mistral, mshairi na mwandishi mashuhuri wa Amerika ya Kusini, alizaliwa nchini Chile. Katika athari zake, mshairi huyo wa Amerika ya Latini, ameienzi na kuitukuza hadhi ya mama pamoja na hisia zake za upendo. Gabriela Mistral alikuwa mshairi wa kwanza wa Amerika ya Kusini kutunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi mnamo mwaka 1945. Amechapisha kazi zake muhimu zaidi katika majimui yenye anuani ya Gabriela. Mwandishi na mshairi huyo maarufu wa Chile aliaga dunia mwaka 1957.

Gabriela Mistral

Miaka 102 iliyopita, tarehe 7 Aprili 1922, alizaliwa Annemarie Schimmel, Mtaalamu wa Kijerumani wa masuala ya Uislamu. Alipenda sana kujifunza kuhusu Ustaarabu wa Kiislamu; na akiwa na umri wa miaka 19, Schimmel alipata shahada yake ya Uzamivu (Phd) ya Taaluma za Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin. Kwa miaka mingi, Bi Schimmel alifundisha Historia ya Dini na I'rfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Ujerumani, Marekani na Uturuki. Mbali na Kijerumani na Kiingereza, alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kituruki, Kiurdu na Kibengali ili kuwa na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya Kiislamu. Mtaalamu huyu wa Kijerumani wa masuala ya Uislamu alikuwa na shauku maalumu ya I'rfani ya Kiislamu na shakhsia wa elimu hiyo kama Hafez na Molavi, ambao ni miongoni mwa malenga na wanairfani wakubwa wa Kiirani. Profesa Schimel ametunukiwa tuzo nyingi na shahada za heshima. Amealifu vitabu kadhaa vikiwemo Muhammad SAW Mtume wa Allah, Mwanamke Katika I'rfani na Tas'awuf ya Kiislamu (Women in Islamic Mysticism and Sufism), Jalaluddin Rumi na Ghazali za Ulimwengu wa Mashariki (Oriental Ghazliat). Bi Shimmel alifariki dunia mwaka 2003.

Annemarie Schimmel

Na miaka 77 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Aprili 7, 1947, Henry Ford, mvumbuzi na mwanasayansi wa Marekani, alifariki akiwa na umri wa miaka 84. Alizaliwa mwaka 1863 katika familia maskini huko Greenfield, Marekani. Ford alijishughulisha na utengenezaji wa saa akiwa mtoto na umekanika akiwa kijana, lakini kufikia wakati wa kifo chake, alikuwa ameunda himaya na mtandao mkubwa katika sekta ya uundaji magari. Ford anahesabiwa pia kuwa mmoja wa wavumbuzi wa magari.

Henry Ford

 

 

Tags