Apr 25, 2024 02:45 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 25 Aprili, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Shawwal 1445 Hijria sawa na Aprili 25 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 532 serikali ya mwisho ya Kiislamu barani Ulaya ilisambaratika huko Granada. Baada ya kudhihiri dini ya Uislamu na kupanua mamlaka yake katika maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika, jeshi la Waislamu liliingia kusini magharibi mwa Ulaya kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na kulitawala eneo hilo kwa kipindi cha karne 8. Eneo hilo ambao kwa sasa linaitwa Uhispania, wakati huo lilijulikana kwa jina la Andalusia. Katika kipindi cha ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu eneo la Granada lilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu huo na makao makuu ya kueneza Uislamu hususan barani Ulaya. Dola la Kiislamu la Andalusia liliangushwa kupitia njia ya kueneza ufuska na maovu baina ya watawala na makhalifa wa wakati huo. 

Granada

Miaka 126 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Uhispania. Kabla ya hapo, Marekani ilikuwa imeitaka Uhispania ilipatie ufumbuzi suala la Cuba kupitia njia za amani. Baadhi ya Wacuba kwa miaka mingi walikuwa wakipigania mamlaka ya kujitawala na mara kadhaa walifanya majaribio ya mapinduzi na kuendesha mapigano ya silaha. Kulipuka manowari ya kijeshi ya Marekani ya Maine katika maji ya Cuba, kilikuwa kisingizio kizuri kwa Marekani cha kuingia katika vita dhidi ya Uhispania. Katika vita hivyo vilivyoanza tarehe 25 Aprili hadi Agosti 12 mwaka 1898 vilimalizika kwa kushindwa Uhispania; na kwa mujibu wa mkataba wa Paris ardhi za Ufilipino, Ouerto Rico, Guam na Cuba zipatiwa Marekani.***

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Ordibehesht 1315 Hijria Shamsia, kituo cha kwanza cha matangazo ya redio na telegrafu kilianza kazi nchini Iran.

Mwanzoni mwa kuanzishwa kwake, kituo hicho kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Vita. Miaka iliyofuata vituo vya kurusha matangazo ya redio na telegrafu vilianzishwa katika miji mbalimbali ya Iran na idara hiyo ikakabidhiwa kwa Wizara ya Posta na Telegrafu. 

Miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo, Wamarekani laki mbili walifanya maandamano mjini Washington wakiendeleza upinzani wao dhidi ya mashambulizi ya nchi hiyo huko Vietnam.

Maandamano hayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vikubwa vya upinzani wa wananchi wa Marekani dhidi ya siasa za kichokozi za serikali ya nchi hiyo huko Vietnam.

Katika vita vya Vietnam vilivyoanza mwaka 1964 Marekani ilituma askari laki tano nchini humo ambako maelfu miongoni mwao waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa sababu hiyo wananchi wa Marekani walizidisha upinzani dhidi ya vita hivyo na mwaka 1975 Marekani ililazimika kufunga virago na kuondoka Vietnam kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa na kushindwa mara kwa mara jeshi la nchi hiyo katika medani za vita. 

Athari za vita vya Vietnam