May 08, 2024 02:30 UTC
  • Jumatano, tarehe 8 Mei, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 29 Shawwal 1445 Hijria sawa na Mei 8, 2024.

Tarehe 8 ya kila mwezi Mei inatambuliwa kuwa siku ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu.

Msalaba Mwekundu ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa kwa ajili ya kutuliza machungu ya wanadamu na kulinda maendeleo ya sekta ya afya ya kijamii kwa mujibu wa mkataba wa Geneva, Uswisi hapo mwaka 1864 Miladia.

Jean Henri Dunant raia wa Uswisi, alikuwa na nafasi kubwa katika kuundwa shirika hilo la kimataifa. Hii ni kwa kuwa mwaka 1862 alitoa pendekezo la kusaidiwa wagonjwa na majeruhi wa kijeshi, pendekezo ambalo lilipokelewa na asasi za masuala ya misaada ya kibinaadamu na kukubaliwa hapo baadaye na kongamano la kimataifa mjini Geneva mwaka 1864.

Ni baada ya hapo ndipo shirika hilo la Msalaba Mwekundu likaundwa na kuanza kuenea duniani. Katika nchi za Kiislamu shirika hilo linaitwa kwa jina la Hilali Nyekundu. 

Tarehe 8 Mei 1794 aliuawa Antoine Laurent - de Lavoisier mtafiti, mvumbuzi na msomi wa Kifaransa na mmoja kati ya waanzilishi wa elimu ya kemia ya kisasa, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kukatwa kichwa kutokana na amri ya utawala wa Kifalme baada ya mapinduzi ya Ufaransa.

Lavoisier aligundua elementi zinazounda hewa katika utafiti wake. Baada ya hapo, mkemia huyo wa Kifaransa aliweza kuvumbua gesi ya oksijeni. Lavoisier anafahamika kama 'Baba wa Kemia ya Kisasa. 

Antoine Laurent - de Lavoisier

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita tatibu James Parkinson wa Uingereza aligundua ugonjwa wa Parkinson.

Dalili kuu za ugonjwa huo ni zile zinazohusiana na kutetemeka sana kwa baadhi ya viungo vya mwili, kukaza misuli, mwendo wa pole yaani mtu hushindwa kutembea haraka pamoja na kupepesuka.

Ugonjwa huo unasababishwa na baadhi ya matatizo ndani ya ubongo na hadi kufikia sasa tiba mujarabu ya maradhi hayo haijapatikana.   

James Parkinson

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita mwafaka na tarehe 8 Mei 1902, mji wa Saint-Pierre uliteketea baada ya kulipuka volkano kwenye mlima Pelee kusini mwa Ufaransa. Watu wasiopungua elfu 30 walipoteza maisha yao kwenye maafa hayo yaliyochukua muda wa dakika tatu tu.   

Volkano kwenye mlima Pelee

Miaka 97 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 19 Ordibehesht mwaka 1306 Hijria Shamsia, sheria ya "Capitulation' ilifutwa na Bunge la Kitaifa la Iran.

Kimsingi sheria hii ilikuwa na lengo la kuwapa kinga ya kutoshtakiwa raia wa kigeni waliopatikana na hatia ya kufanya uhalifu nchini Iran. Haki ya  'Capitulation' ilitumika mara ya kwanza nchini Iran baada ya mapatano ya Torkmanche ya mwaka 1206 wakati wa utawala wa Fath-Ali Shah ambapo Warusi walipata kinga hiyo na baada ya hapo serikali zingine za kigeni nazo ziliweza kupata haki hiyo ya raia wao kutoshtakiwa nchini Iran.

Hata hivyo sheria hiyo ilipitishwa tena na bunge la kitaifa la Iran mwaka 1343 kwa lengo la kuwapa kinga Wamarekani. Imam Khomeini MA alipinga vikali sheria hiyo na utawala wa Shah ulikasirishwa sana na malalamiko hayo na ukachukua uamuzi wa kumbaidisha Imam nchini Uturuki.

Hatimaye, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, sheria ya 'Capitulation' ilifutwa daima nchini Iran. 

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Mei 1945, vilimalizika Vita vya Pili vya Dunia baada ya Wanazi wa Ujerumani kusalimu amri bila ya masharti.

Ujerumani ilianza kushindwa vita hivyo tokea mwaka 1943. Vita vya Pili vya Dunia vinahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi kutokea katika historia ya mwanadamu, kwani karibu watu milioni 55 waliuawa katika vita hivyo vilivyosababisha pia hasara kubwa. 

Japan iikisalimu amri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia

Na katika siku kama hii ya leo miaka 36 iliyopita, siku 50 baada ya maafa ya Halabja, azimio nambari 612 la Baraza la Usalama lilitolewa kuhusu matumizi ya silaha za kemikali ya utawala wa Iraq katika vita vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Iran dhidi ya Iraq kuhusiana na mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyofanywa na utawala wa Saddam Hussein dhidi ya wananchi wa Iran, baada ya kutembelea maeneo ya pande zote mbili, wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa waliwasilisha ripoti yao wakieleza jinsi utawala huo ulivyotumia silaha za kemikali dhidi ya jeshi na raia wa Iran pamoja na jeshi la Iraq kwa Katibu Mkuu. 

Maafa ya Halabja