Hikma za Nahjul Balagha (51)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 51 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 51 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 44.
طُوبَى لِمَنْ ذَکَرَ الْمَعَادَ، وَ عَمِلَ لِلْحِسَابِ، وَ قَنِعَ بِالْکَفَافِ، وَ رَضِیَ عَنِ اللَّهِ
Hongera kwa anayekumbuka siku ya kufufuliwa, akatenda kila kitu kwa ajili ya siku ya hisabu, akakinai kwa anachoruzukiwa na Muumba na akawa radhi na Allah.
Katika hikma ya 44 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatuusia kwa kusema: Hongera kwa anayekumbuka siku ya kufufuliwa ambayo ni siku isiyo na shaka na kila anayekumbuka siku ya kufufuliwa lazima atajiandaa kwa kutenda kila kitu kwa ajili ya siku ya hisabu na atakinai na anachoruzukiwa na Muumba. Vile vile atakuwa radhi na Allah na Allah Naye atamridhia.
Katika mafundisho ya Imam Ali (AS) yaliyomo kwenye kitabu cha Nahjul Balagha, kukumbuka kifo na kutafakari juu ya siku ambayo mtu ataondoka hapa duniani, ni jambo muhimu sana. Kwa sababu hakuna kitu kingine kinachoshinda kukumbuka kifo ambacho kinaweza kumtoa mtu kwenye kiburi, majigambo na majivuno na kumpeleka karibu na unyenyekevu. Kitu cha kuzingatia hapa ni kwamba kila mmoja wetu huwa anakumbushwa kifo na Mwenyezi Mungu mara kwa mara. Mwenyezi Mungu ana njia nyingi za kutukumbusha siku ya kuondoka duniani ikiwa ni apmoja na kuondokewa na wapendwa wetu, marafiki na jamaa zetu. Na kwa kweli kama Mwenyezi Mungu asingelikuwa anatukumbusha kifo mara kwa mara tungefanya nini? Bila ya shaka mghafala ungetuvaa na kuyaghilibu maisha yetu na tungekuwa viumbe asi na waovu mno. Imam Ali AS hapa amejaribu sana kutuondoleaa mghafala huo kwa kutwambia Hongera kwa anayekumbuka siku ya kufufuliwa, akatenda kila kitu kwa ajili ya siku ya Hisabu, akakinai kwa anachoruzukiwa na Muumba na akawa radhi na Allah. Bila ya shaka yoyote mtu akikumbuka kifo na akaona fursa aliyo nayo ya kuishi hapa duniani ni fupi na akawa na yakini kwamba kuna Siku ya Hisabu ambayo atakwenda kuulizwa kila sekunde na lahdha ya maisha yake, bila ya shaka atajitayarisha kwa siku hiyo na atatumia muda huu aliopewa na Allah kwa njia na namna sahihi. Atakuwa mcha Mungu na mpole mbele ya viumbe wa Mwenyezi Mungu na atajipinda katika kutenda mambo ya kheri kujiwekea akiba bora kwa ajili ya Siku ya Hisabu na hatopuuza kutenda wema wowote ule.
Moja ya matatizo makubwa ya mwanadamu ni kukosa kukinai na kuridhika. Kwa maana ya kwamba chochote anachopata mtu huwa haridhiki na hakinai na matokeo yake ni mtu huyo kukosa utulivu na kunufaika na raha za maisha. Tunachoshuhudia leo duniani ni kwamba watu wengi hawaridhiki na walivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Pupa imewapofua macho watu na tamaa imebadilisha kabisa makhusiano ya binadamu. Pupa hiyo inayafanya mashirika ya uzalishaji bidhaa kujali tu faida na yanawatumikisha watu kupita kiasi kuzalisha bidhaa nyingi kupindukia. Matokeo yake ni kukosekana soko la watumiaji, na sasa imekuwa ni kulazimishwa watu kuwa na matumizi ya kuchupa mipaka kwa vitu ambavyo sehemu yake kubwa si ya dharura katika maisha yao. Imam Ali anatuonya kuhusu mtindo huo mbovu wa maisha uliotawala duniani leo kwa kututaka tutosheke na tulichoruzukiwa na Allah na hizo ni nasaha zile zile za Bwana Mtume Muhammad SAW alipowausia Waislamu akiwaambia toshekeni na mnachoruzukiwa na Allah, mtakuwa matajiri kuliko watu wote. Kuna hadithi moja maarufu inayosema kuwa, siku moja Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa safarini jangwani yeye na masahaba wake. Wakafika kwa mkulima mmoja wakataka kununua maziwa kutoka kwake. Mkulima yule alifanya ubakhili. Aliwaambia maziwa haya yaliyomo kwenye chombo ni kwa ajili ya chakula chetu na yaliyomo kwenye chuchu za mnyama pia ni kwa ajili ya watu wa kijijini kwetu na hata hayatoshi. Mtume alimuomba dua apate utajiri mwingi na watoto wengi. Wakaendelea na safari wakafika kwa mchungaji. Walipotaka kununua, yule mchungaji si tu alikusanya maziwa ya kwenye vyombo, bali alikamua mengine pia akampelekea Bwana Mtume kwa heshima zote. Mtume alimuombea dua kwamba Mwenyezi Mungu ampe kwa kiwango kinachomtosha. Masahaba walishangaa wakasema Yaa RasulaLlah, yule mtu bakhili umemuombea apate mali na watoto wengi lakini huyu muumini wa kweli na mkarimu mno umemuomba apate kidogo ikilinganishwa na yule bakhili. Bwana Mtume alijibu kwa kusema, kiwango kidogo kinachoweza kumtosheleza mja kwenye maisha yake ni bora kuliko kiwango kikubwa ambacho kinamfanya mtu amsahau Muumba wake.