Jul 01, 2024 06:06 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (59)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 59 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 59 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 52.

أَوْلَى النَّاسِ بِالْعَفْوِ، أَقْدَرُهُمْ عَلَى الْعُقُوبَة

Anayestahiki zaidi kusamehe ni yule mwenye uwezo mkubwa zaidi ya kutoa adhabu.

Katika Hikma hii ya 52 ya Kitabu cha Nahj al-Balaghah, Imam Ali AS anatoa somo jingine muhimu akisema: Mtu anayefaa na mwenye ustahiki zaidi wa kusamehe, ni yule mwenye nguvu na uwezo mkubwa zaidi wa kuadhibu.

 

Kama tunavyojua, chuki na fikra ya kulipiza kisasi ni moja ya sababu za kuendelea ugomvi na migogoro kati ya watu wawili au watoto wa familia moja au makabila na mataifa mawili kwa miongo kadhaa. Kwa bahati mbaya kadiri fikra hiyo ya kulipiza kisasi na kutokubali kushindwa inavyoendelea ndivyo inavyozidi kutatanisha mambo na kuongeza uadui, ni mithili ya maji ya mafuriko, kila yanaposonga mbele yanazidi kuwa mengi na yenye uharibifu mkubwa zaidi. Lakini kama upande mmoja wa mzozo utafanya uungwana na busara ya kusamehe mgogoro huo huweza kuisha hapo hapo na usijitokeze tena milele.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana tunayaona mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu, yanatoa umuhimu mkubwa kwenye suala la kusamehe. Msamaha, kwa upande mmoja, huimarisha uhusiano wa kijamii na mahusiano ya kirafiki, na kwa upande mwingine, humlazimisha mkosaji kufikiria upya vitendo vyake na kujirekebisha, ambayo humfanya mtu kuimarika kiroho na kimaanawi.

 

Imam Ali AS katika hikma hii adhimu anatufundisha kuwa kusamehe si ishara ya udhaifu, bali ni ushahidi wa mtu kuwa na nguvu zaidi. Aidha anatufundisha kuwa, yule mwenye nguvu zaidi, yule mwenye nafasi na uwezo mkubwa zaidi wa kutoa adhabu, ndiye yeye anayestahiki zaidi kusamehe. Wakati mtu mwenye uwezo wa kutoa adhabu anapoamua kutumia nguvu zake na badala yake kumsamehe aliyemkosea, mtu huyo huthibitisha kivitendo kwamba yeye ni muungwana. Hii ni tofauti na yule mtu ambaye anaamua kusamehe pale anapokuwa hana uwezo wowote wa kutoa adhabu lakini akipata fursa kidogo tu hurejea kwenye kinyongo chake na kutoa adhabu kwa waliomkosea. Aya za Qur'ani Tukufu zimejaa mafundisho hayo. Kwa mfano katika kisa cha Nabii Yusuf AS, wakati alipokuwa azizi wa Misri na uwezo wa kutoa adhabu kali kwa kaka zake waliomfanyia maovu na ukatili wa kuchupa mipaka, aliamua kuwasahe. Muda wa dakika hizi chache hauruhusu kuchambua kila kitu. Imepokewa kwamba Nabii Musa AS alimuuliza Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ni mja gani unayempenda zaidi? Ukaja wahyi unaosema: Yule aliyedhulumiwa na ana uwezo wa kulipiza kisasi, lakini akasamehe. Pia aya ya 199 ya Sura ya al A'raf inasema: Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na majahili.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

عفو و گذشت را پیشه کن، و به کار پسندیده فرمان ده (ایه 199 سوره اعراف)