Jumamosi, 13 Julai, 2024
Leo ni Jumamosi 7 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na 13 Julai 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1960 iliyopita, moto mkubwa ulitokea huko Roma mji mkuu wa utawala wa kifalme wa Roma. Sehemu kubwa ya mji wa kihistoria na mkongwe wa Roma iliungua na wakazi wengi wa mji huo walipoteza maisha yao kutokana na moto huo. Moto huo ulikuwa kisingizio tosha kwa Nuren mtawala mmwagadamu wa Kirumi ambaye aliwauwa kwa umati watu zaidi ya laki moja na baadaye kuwatuhumu Wakristo kuwa ndio walioanzisha moto huo. ***

Miaka 1385 iliyopita, Omar Bin Saad, alitoa amri ya kuuzuia msafara wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) kutumia kwa aina yoyote maji ya mto wa Furati (Euphrates.) Baada ya Ubaidullah Bin Ziyad, kutuma jeshi kubwa kwa ajili ya kupambana na mjukuu huyo wa Mtume, alituma barua kwa Ibn Saad ili kumzingira Imam Hussein na masahaba zake. Katika ujumbe huo, Bin Ziyad alimtaka Omar Bin Saad kumwamuru Al-Imamul-Hussein kumbai Yazid mwana wa Muawiya. Aidha sehemu nyingine ya barua hiyo ilimtaka kamanda huyo wa jeshi katili kumtenga mjukuu huyo wa Nabii wa Allah na maji ya Mto Furati na asimruhusu kamwe kuweza kuyanywa yeye au vamilia yake. Bila kuchelewa Ibn Saad aliwaamuru askari 500 wapanda farasi kumzuia Imam Hussein na maji ya mto huo. Kitendo hicho cha kikatili, kilijiri ikiwa ni siku tatu kabla ya kuuawa shahidi Imam Huusein (as). Hata hivyo Abul-fadhlil-Abbas alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwaletea maji watu wa msafara huo ingawa hata hivyo askari wale katili walimzuia na kumuua kinyama mtukufu huyo. Hadi asubuhi ya siku ya tisa ya mwezi huu wa Muharram, hakukuwa na tone la maji lililokuwa limesalia kwa wafuasi wa mjukuu huyo wa Mtume (Imam Hussein) suala ambalo liliwafanya watukufu hao kuvumilia tabu ya kiu kali kutokana na joto kali lililokuwepo eneo hilo. ***

Miaka 624 iliyopita katika siku kama ya leo, liliundwa jeshi la kale zaidi duniani nchini Uswisi. Jeshi hilo la kale zaidi duniani hadi hii leo limebakia kama lilivyokuwa na hata mavazi ya wanajeshi wake hayajabadilika. Idadi ya wanajeshi wa jeshi hilo dogo lakini lenye nidhamu kubwa ni watu 83. Jeshi hilo ambalo wanachama wake daima huwa raia wa Uswisi, liliundwa kwa ajili ya kulinda viongozi wa Kikatoliki wa wakati huo na hii leo baada ya kupita zaidi ya miaka zaidi ya 600 tangu liundwe, jeshi hilo lina jukumu la kumlinda Papa wa Kanisa Katoliki huko Vatican. ***

Katika siku kama ya leo miaka 253 iliyopita, baharia na nahodha mashuhuri wa Kiingereza aliyejulikana kwa jina la James Cook alikamilisha safari yake ya kitafiti na kielimu ya kuelekea The Great Southern Continent. Safari hiyo ilikuwa imeanza tarehe 26 Julai mwaka 1768. Safari hiyo ndefu iliishirikisha pia timu ya watalaamu wa elimu ya Sayansi Asilia au Natural Science kwa kimombo. Wataalamu hao walikuwa na nia ya kufanya utafiti wa kielimu kuhusiana na mimea pamoja na viumbe wanaopatikana katika maeneo hayo. ***

Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alizaliwa Sayyid Mohammad Hadi Milani, marjaa mkubwa wa Waislamu wa Shia. Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammad Hadi Milani alizaliwa tarehe saba mwezi Muharram mwaka 1313 Hijiria Qamaria huko mjini Najaf, Iraq. Alianza kusoma elimu ya dini akiwa na umri mdogo ikiwa ni pamoja na kujifunza Qur'ani Tukufu mjini hapo. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kifarsi na Kiarabu huku akiandika pia vitabu vingi. Aidha kando na shughuli hiyo alikuwa akifundisha idadi kubwa ya wanafunzi elimu ya hawza ya kidini na kufikia daraja ya umarjaa. Msomi huyo alitambulika kwa uchaji-Mungu, taqwa, na tabia njema ya hali ya juu. Kitabu cha 'Muhaadharat fii Fiqhil-Imaamiyyah' ni miongoni mwa athari za msomi huyo. ***

Miaka 41 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 23 Tir mwaka 1362 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake ilianza shughulki zake. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Baraza la Wanazuoni ni moja ya nguzo na asasi muhimu katika mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini. Wawakilishi wa baraza hilo ni lazima wawe mafakihi waliotimiza masharti na huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi. Jukumu muhimu la Baraza la Wataalamu ni kumchagua Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusimamia shughuli za utendaji wake. Uchaguzi wa baraza hilo la Iran hufanyika mara moja kila baada ya miaka minane. ***

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, alifariki dunia Mahdi Hamidi Shirazi, malenga, mtafiti na mwandishi mkubwa wa zama hizo. Mahdi Shirazi alizaliwa mwaka 1293 Hijria katika mji wa Shiraz wa kusini mwa Iran na kutunukiwa shahada ya udaktari katika taaluma ya lugha na fasihi ya Kifarsi. Dakta Hamidi ameandika vitabu vingi vya mashairi ya Kifarsi, ambapo vingi vinahusiana na elimu ya mitindo, fasihi, historia na fani mbalimbali za mashairi. ***

Na tarehe 13 Julai inayosadifiana na Jumamosi ya leo ni siku ya kumbukumbu ya Romania kujipatia uhuru kutoka kwa Utawala wa Othmania. Kijiografia Romania ipo kusini mashariki mwa Ulaya na magharibi mwa Bahari Nyeusi. Romania ina zaidi ya wakazi milioni 22 na dini rasmi ya nchi hiyo ni Ukristo na madhehebu ya Orthodox ndiyo yenye wafuasi wengi. Nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Othmania kuanzia karne yay 15. Hata hivyo mwaka 1877 Romania iliungana na Russia katika vita dhidi ya utawala wa Othmania. Hatimaye katika siku kama ya leo Romalia ikajipatia uhuru na miaka mitatu baadaye ikawa imepata uhuru kamili. ***
