Jumamosi, 03 Agosti, 2024
Leo ni Jumamosi 28 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria, mwafaka na tarehe 3 Agosti 2024
Siku kama ya leo miaka 790 iliyopita mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi, ulitekwa na Hulagu Khan. Hulagu alimuua mtawala Musta'sim na kukomesha kabisa utawala wa kizazi cha Bani Abbasi uliotawala maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 500. Katika unyama huo mkubwa, Hulagu Khan alifanya ukatili mkubwa na kuua nusu ya watu wasiokuwa na hatia wa mji wa Baghdad. Hulagu Khan pia alichoma moto nyumba na majengo mengi ya kihistoria ikiwemo maktaba kubwa ya Baghdad na idadi kubwa ya vitabu vyenye thamani kubwa vya maktaba hiyo viliteketea au kutumbukizwa katika mto Tigris. ***

Katika siku kama ya leo miaka 532 iliyopita baharia wa Kiitalia Christopher Columbus alianza safari kubwa zaidi ya kiuvumbuzi. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya inayoelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania. Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Baharia huyo wa Kiitalia na wenzake walidhani kuwa wamefika India. Hata hivyo walikuwa wamefika katika kisiwa kilichojulikana kwa jina la Salvador katika bara la Amerika. ***

Miaka 110 iliyopita katika siku kama hii ya leo Mfereji wa Panama ulifunguliwa baada ya meli ya kwanza kupita katika mfereji huo. Mfereji wa Panama ulianza kujengwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye ujenzi huo ukakamilishwa na Wamarekani. Mfereji wa Panana ulio na urefu wa kilomita 68 unaunganisha bahari mbili za Atlantic na Pacific. ***

Katika siku kama ya leo miaka 94iliyopita, alizaliwa katika mji wa Mash'had, Iran, Ayatullah Sayyid Ali Sistani faqihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kishia. Alianza kujifunza Qur'ani akiwa na miaka 5,na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf, Iraq hapo baadaye. Hii leo Ayatullah Ali Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali amekuwa pia na nafasi muhimu katika kuimarisha umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu. ***

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, mwafaka na tarehe 3 Agosti 1960, nchi ya Kiafrika ya Niger ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Niger ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa tangu karne ya 18 na mwaka 1922 ikawa koloni rasmi la Wafaransa baada ya nchi hiyo kujenga vituo vyake vya kijeshi nchini humo. Hata hivyo taratibu wananchi wa Niger walianzisha uasi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa na hatimaye nchi hiyo ilifanikiwa kupatia uhuru katika siku kama hii ya leo. Niger iko magharibi mwa Afrika na inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin. ***

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hatua yake nyingine ya kigaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uliwauwa Izzuddin Qalq mjumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel, MOSSAD, katika miongo miwili ya 70 na 80 liliwauwa kigaidi viongozi wengi wa PLO ili kuidhoofisha harakati hiyo na kuilazimisha kuanzisha mazungumzo eti ya mapatano kati ya Wapalestina na Israel. ***
