Iran yashinda idadi kubwa ya medali katika olimpiadi za kisayansi
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utaweza kunufaika.
Tamasha la Kimataifa la Uvumbuzi linalojulikana kama International Inverse Invention and Innovation lilifanyika Mwezi Agosti kwa kushirikisha watafiti kutoka nchi 34 zikiwemo: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani, Kanada na China. Kongamano hilo lililandaliwa na jumuiya ya kimataifa ya uvumbuzi, sayansi na utafiti pamoja na mashirika ya Google na Microsoft.
Mehrdad Soleimani, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kisayansi la Tawatron la Iran, kama mwakilishi wa Tamasha la Kimataifa la Uvumbuzi la Inverse nchini Iran, alisema kuhusiana na hili:
Katika hafla hii, timu zinazojumuisha wanafunzi, maprofesa na wafanyabiashara kutoka kote nchini Iran walishiriki katika sehemu mbili za wazo, uvumbuzi, ubunifu pamoja na akili mnemba yaani Artificial Intelligence na changamoto za programu. Watafiti wa Iran walijishindia medali 9 za dhahabu, 5 za fedha na 4 za shaba katika sehemu ya wazo, uvumbuzi na ubunifu, na medali 1 ya dhahabu, medali 3 za fedha na 1 ya shaba katika sehemu ya changamoto za mnemba na programu.
@@@
Baada ya kumalizika Olympiadi za Sayansi mwaka 2024, katika Olympiads 5 zilizokuwa na idadi kubwa ya nchi zilizoshiriki (kutoka nchi 53 hadi 110), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishika nafasi ya tatu duniani baada ya Marekani na China kwa kushinda jumla ya medali 10 za dhahabu, 10 za fedha na 2 za shaba.
Yamkaini mafanikio hayo hayakuakisiwa sana kwani katika msimu wa joto Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya Paris iliangaziwa zaidi.
Katika kipindi hicho hicho, kikundi cha wanafunzi wa Iran pia kilikwenda kwenye Olympiadi za kisayansi za dunia na kuiletea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran idadi kubwa ya medali. Kwa hakika, Iran iliweza kushika nafasi ya 3 duniani kwa kushinda medali 22 katika Olympiadi 5 za sayansi pekee bila kutaja medali za Olympiadi za fizikia na geosayansi. Kwa kuzingatia medali za Olympiadi hizo mbili ziada idadi ya medali za Iran mwaka huu imefika 30.
Seyedreza Hosseini, Mkuu wa Klabu ya Wasomi Vijana ya Iran alisema: "Hadi sasa katika mwaka 2024, wanachuoni wa Iran, wamefanikiwa kupata nafasi ya kwanza katika Olympiad ya Dunia ya Astronomia na Astrofizikia, nafasi ya nne katika Olympiadi za Biolojia na Fizikia, nafasi ya nane katika Olympiad ya Kemia, nafasi ya tisa katika Olympiad ya Kompyuta na nafasi ya kumi na tisa katika Olympiad ya Hisabati. Pia wanafunzi wa Iran walishiriki Olympiadi ya Sayansi ya Dunia mwaka huu kwa mara ya kwanza na kujishindia medali za fedha na 2 za shaba."
Kuhusiana na hilo, Hosseini aliongeza: “Asilimia 30 ya washindi wa medali ni wasichana katika mashindano haya, lakini washiriki wa kiume na wa kike ni sawa. Mwaka huu pia, uwepo wa wasichana umeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo ina maana kwamba uwepo wa wasichana wa Iran katika majukwaa ya kimataifa ni muhimu sana.
@@@
Watafiti wa Immunolojia wa Chuo Kikuu cha Tehran cha Sayansi ya Tiba wamefanikiwa kuunda seli ili kuongeza athari za kupambana na uvimbe wa saratani.
Tahera Sultan Tuye, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika elimu ya kinga ya Chuo Kikuu cha Tehran cha Sayansi ya Tiba, alielezea kuhusu sababu ya kutekeleza mradi huu kwa kusema: "Saratani ni moja ya matishio muhimu kwa afya, ni sababu ya pili ya kifo baada ya magonjwa ya moyo na mishipa. Hadi sasa, hatua nyingi za matibabu ni pamoja na upasuaji, chemotherapy, radiotherapy, matumizi ya kingamwili ya monoclonal na dawa za kifamasia zimetumika kutibu saratani, lakini kwa bahati mbaya, njia hizi za matibabu hazijafanikiwa sana. Katika mpango huu, tulijaribu kusaidia kuongeza mafanikio ya matibabu hayo na kupambana na uvimbe wa saratani zenye kiwango kikubwa mesothelin kwa kuzalisha seli zenye muundo utakaoleta ufanisi zaidi.
@@@
Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Uhandisi Jeni na Bioteknolojia ya Iran Javad Mohammadi, na balozi wa Sudan mjini Tehran, Abdulaziz Hassan Saleh Taha, wamekutana hivi karibuni kujadili njia za kupanua uhusiano wa kisayansi.
Akitembelea taasisi hiyo ambayo kifupi inajulikana kama NIGEB, Balozi Saleh Taha amesema amevutiwa na maendeleo ya Iran katika nyanja za teknolojia ya kibayoteknolojia na jenetiki. Ameongeza kuwa Taasisi hiyo ya Iran ya Uhandisi Jeni na Bayoteknolojia inaweza kuwa kielelezo kamili cha kisayansi cha kuanzisha vyuo vikuu na vile vile vyuo nchini Sudan.
Aidha Balozi Taha ameendelea kusema kuwa, Sudan inataka kuimarisha ushirikiano na Iran katika kutibu magonjwa kama vile saratani na magonjwa ya kuambukiza, pamoja na kubadilishana maprofesa na wanafunzi. Amesema Sudan iko tayari kujifunza kutokana na uzoefu wake muhimu katika nyanja ya kisayansi ya kimataifa.
Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Uhandisi Jeni na Bioteknolojia ya Iran Javad Mohammadi kwa upande wake amesema kwa kuzingatia sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kustawisha ushirikiano wa kimataifa katika uga wa diplomasia ya kisayansi, taasisi hiyo inakaribisha ushirikiano wa kisayansi na maingiliano na nchi nyingine hususan mataifa ya Kiislamu.
Aidha amesema wakati wa magonjwa ya milipuko katika nchi za Afrika, taasisi ya utafiti inaweza kushirikiana na Sudan na nchi nyingine za Afrika kutengeneza vifaa vya tiba na matibabu.
@@@
Naam na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia. Ni matumaini yangu kuwa umeweza kunufika.