Jumapili, 19 Januari, 2025
Leo ni Jumapili 18 Rajab 1446 Hijria mwafaka na 19 Januari 2025.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita alifariki dunia mtoto mdogo wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ibrahim akiwa na umri wa miezi 18 tu. Ibrahim ambaye alifariki dunia kutokana na maradhi alikuwa mtoto pekee wa kiume wa Mtume ambaye hakuzaliwa na Bibi Khadija (as). Mama yake alikuwa Maria al Qibtiyya ambaye alitumwa na mfalme wa Misri ya wakati huo kuwa hadimu na mtumishi wa Mtume na aliolewa na mtukufu huyo baada ya kusilimu. Kifo cha Ibrahim kilimhuzunisha sana Mtume (saw) kwa sababu mtukufu huyo alikuwa akimpenda sana mtoto huyo.

Tarehe 18 Rajab miaka 1020 iliyopita alifariki dunia Ibn Samh huko katika mji wa Andalucia. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa hesabu, nyota na tabibu. Alizaliwa katika mji wa Cordoba, Andalucia mnamo mwaka 370 Hijiria. Msomi huyu wa Kiislamu alifanya utalii na utafiti mwingi katika elimu za hesabu na nyota, sambamba na kuwalea wanafunzi wa zama zake. Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa na Ibn Samh kwa lugha ya Kiarabu na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Al Madkhalu Ila al Handasah", "Al Muamalat" na "Kitabuz Ziyj."

Siku kama hii ya leo miaka 289 iliyopita alizaliwa mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini. ***

Miaka 227 iliyopita inayosadifiana na siku hi ya leo, alizaliwa Auguste Comte mwanafalsafa, mwanahisabati wa Kifaransa na mtaalamu wa falsafa umbile au positivism kwa kimombo. Comte alifikia daraja ya uhadhiri katika hisabati akiwa na umri wa miaka 18 tu. Vitabu mashuhuri vya mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni Auguste Comte and positivism na Early Political Writings. Comte aliaga dunia mwaka 1517. ***

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran. Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi. Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah. Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah waliwashambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. ***

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita sawa na tarehe 30 Dei 1357 Hijria Shamsia, Mhandisi Mehdi Bazargan, Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifariki dunia. Mhandisi Bazargan alizaliwa mjini Tehran na kuhitimu masomo yake ya uhandisi wa magari huko nchini Ufaransa. Alikuwa mhadhiri pia katika Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika harakati za kisiasa wakati wa kujiri tukio la kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa. Muda mchache kabla ya mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Mehdi Bazargan alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na kwa pendekezo la baraza hilo alitakiwa kuunda serikali ya muda. Hata hivyo serikali yake ilidumu kwa muda wa miezi 9 tu kutokana na kuwa na tofauti za kimsingi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kupenya katika serikali hiyo vibaraka waliokuwa dhidi ya mapinduzi. Hatimaye Bazargan aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua maradhi ya moyo.***

Katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, Abdul Rauf Mahmoud al-Mabhuh, mmoja wa makamanda waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) aliuawa shahidi huko Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Mabhouh aliuawa na makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel walioingia nchini Imarati wakitumia pasipoti bandia. Mabhuh alizaliwa katika familia iliyoshikamana na dini katika kambi ya Jabalia katika Ukanda wa Gaza, Palestina. Shahidi Mahmoud al-Mabhuh ni miongoni mwa waasisi wa Brigedi ya Izzudeen al-Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Baada ya kupita miezi kadhaa, Israel ilitangaza wazi kwamba, ilihusika na jinai ya kumuua Mabhuh. ***
