Jumamosi, 09 Agosti, 2025
Leo ni Jumamosi 15 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria mwafaka na 9 Agosti 2025.
Tarehe 9 Agosti ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili (Indigenous). Siku hiii ambayo huadhimishwa kila mwaka ilitangazwa rasmi ili kukumbuka na kutetea haki za zaidi ya watu milioni 370 wa asili katika nchi 90 duniani. Siku hii imekuwa ikiadhimishwa kwa ajili ya kuwakumbuka maelfu ya wanaume na wanawake wa asili wanaoshikamana na mila, tamaduni na desturi zao. Watu wa asili (Indigenous) ni makundi na mataifa ambayo yanadai kuwa, yana mfungamano makhsusi wa kihistoria na kiutamaduni na jamii za ardhi au eneo lao la asili. Neno hili hutumika kumaanisha wakazi wa awali na wenyeji wa kila nchi . Hii leo inakadiriwa kuwa, kuna watu wa asili (Indigenous) karibu milioni 370 katika nchi 90 duniani. Hii ina maana kwamba, asilimia 5 ya jamii ya watu wote duniani inaundwa na watu wa asili (Indigenous). Hata hivyo watu hawa wanahesabiwa kuwa ni sehemu ya asilimia 25 ya watu masikini zaidi duniani.

Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo, makubaliano ya aibu na ya kikoloni kati ya Uingereza na Iran yalitiwa saini na Vossouq al-Dawlah, Waziri Mkuu wa Iran wakati huo, na Lord Curzon, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza. Kulingana na makubaliano hoya, yanayojulikana kama "Mkataba wa 1919", masuala ya kiuchumi, kijeshi na kisiasa ya Iran yaliwekwa chini ya usimamizi wa mawakala wa Uingereza. Uingereza iliitwisha Iran mkataba huu baada ya kutokea mapinduzi nchini Urusi na nchi hiyo kujiondoa katika uwanja wa ushindani wa kikoloni. Hata hivyo wapigania uhuru wa Iran walisimama kuyapinga makubaliano hayo kwa sababu kwa hakika yaliiweka Iran chini ya ulinzi wa Uingereza. Kwa upande mwingine, baadhi ya wapinzani wa Uingereza wa Magharibi pia walipinga makubaliano hayo, na makubaliano ya 1919 hatimaye yalibatilishwa. Hata hivyo, mwaka mmoja na nusu baadaye, Uingereza ilipanga na kutekeleza mapinduzi, na kumfanya Reza Khan kutawala na kupitia serikali yake ikaimarisha utawala wake kwa Iran.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, zikiwa zimepita siku tatu tangu Marekani iushambulie kwa bomu la nyuklia mji wa Hiroshima nchini Japan, Washington iliushambulia pia kwa bomu jingine la nyuklia mji wa bandari wa Nagasaki kwa amri ya Harry Truman, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Jumla ya watu elfu themanini walifariki dunia dakika chache tu baada ya shambulizi hilo la bomu la nyuklia huko Nagasaki, na wengine walipoteza maisha baada ya kupita miezi na miaka, kutokana na athari mbaya za mada hatari za mionzi ya nunurishi au radioactive kwa kimombo. Maafa makubwa ya mashambulizi ya mabomu ya nyuklia ya Marekani huko Hiroshima na Nagasaki yaliyofanyika kwa lengo la kuilazimisha Japan isalimu amri kikamilifu mbele ya majeshi ya waitifaki, yalikuwa kengele ya hatari kwa walimwengu kwamba, nchi zinazomiliki silaha za atomiki hususan Marekani, hazisiti kufanya jinai za kutisha kama kuangamiza kizazi cha wanadamu kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, Hermamn Hesse mwandishi na malenga mashuhuri wa Ujerumani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1877 katika familia ya kidini na kuanza kazi ya utunzi wa mashairi katika kipindi cha kuinukia kwake. Akiwa na umri wa miaka 20, Hesse alitoa diwani yake ya kwanza wa mashairi. Mwaka 1912 mwandishi na malenga huyo mashuhuri wa Ujerumani alichukua uraia wa Uswisi na kuichagua nchi hiyo kuwa makazi yake ya kudumu. Mwishoni mwa umri wake alifanya safari katika baadhi ya nchi za mashariki na kuathirika na tamaduni, mafunzo na mienendo ya kiamaadili ya wananchi wa maeneo hayo. Mnamo mwaka 1946 malenga huyo alitunukiwa tuzo ya Nobel.

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Singapore ilijitenga na Malaysia. Japan iliiteka Singapore katika Vita vya Pili vya Dunia lakini mnamo mwaka 1945 uvamizi huo wa Japan ulikomeshwa na kwa mara nyingine tena nchi hiyo ikakoloniwa na Uingereza. Mwaka 1963 Singapore iliunganishwa na Shirikisho la Malaysia na mwaka 1965 ilijitenga na kuwa nchi huru.

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo Richard Nixon Rais wa zamani wa Marekani kutoka chama cha Republican alilazimika kujiuzulu baada ya kukumbwa na kashfa ya kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi wa Rais, kashfa iliyojulikana kwa jina la "Watergate".Nixon alilazimika kung'atuka kwenye nafasi ya urais na kumpisha Gerald Ford aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye aliendeleza kipindi hicho cha urais kwa muda wa miaka minne.
