Oct 13, 2016 02:38 UTC
  • Alkhamisi, Oktoba 13, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 13 2016.

Siku kama ya leo, miaka 1377 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (swa), ulianza kuelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa kidhalimu wa Yazidi bin Muawiya baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura.

Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe yoyote ya ubinaadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (swa). Askari hao sanjari na kuchoma moto hema za Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao, huku wakiwaacha bila stara wanawake. Hatimaye jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), uliendelea na safari kutoka mjini Kufa, Iraq kuelekea Sham, baada ya watukufu hao kuamsha hamasa ya kimapinduzi dhidi ya madhalimu, kuwalaumu watu wa mji huo kwa kumsaliti Imam Hussein (as) na kufichua maovu ya watawala wa Bani Umayyah.

 

Siku kama ya leo miaka 2555 iliyopita mji wa kihistoria wa Babel ulitekwa na Kurosh, mwasisi wa utawala wa kizazi cha Hakhamaneshi nchini Iran. Ili kuweza kuudhibiti mji huo ambao ulikuwa na ngome kubwa na imara, Kurosh kubadilishwa mkondo wa Mto Tigris uliokuwa ukipita katikati ya mji wa Babel. Kwa utaratibu huo askari wa Kurosh walitumia njia ya zamani ya maji ya mto huo kuingia na kisha kuuteka mji wa Babel. Mji huo ulioko kusini mwa eneo la Mesopotamia katika Iraq ya sasa ulikuwa katika kilele cha maendeleo na nguvu kubwa katika kipindi hicho.

 

Vitabu vya jadi

Na Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita alifariki dunia mwandishi na mwanafalsafa wa Kifaransa Joseph Arthur Gobineau. Gobineau alizaliwa mwaka 1816 mjini Paris na baada ya kumaliza masomo yake alijishughulisha na uandishi wa habari. Aidha Gobineau aliwahi kuwa katibu na balozi wa Ufaransa nchini Iran na kupata kujifunza lugha za Kifarsi na Kiarabu. Mwandishi huyo wa Kifaransa aliamini kuwa watu weupe hasa wale wenye asili ya Aryan ndio watu bora zaidi na kuhusiana na suala hilo akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na kutokuwepo usawa kati ya wanadamu. Nadharia ya kuwa kizazi cha Aryan ndicho kizazi bora zaidi kuliko vizazi vingine vya wanadamu ni moja ya sababu zilizompelekea Adolf Hitler kuanzisha Vita vya Pili vya Dunia na kuua kwa umati watu wasiokuwa wa asili ya Aryan.

 

 

 

Tags