Dec 06, 2016 10:04 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (145)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain.

Katika kipindi hiki tutaendelea kujadili suala ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi kadhaa vilivyopita ambalo linazungumzia majukumu tunayopasa kuyatekeleza sisi Waislamu kwa Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw).

Tulipata kujua katika vipindi hivyo kwamba mengi ya majukumu hayo ambayo tuliyafahamu kutokana na maandiko matakatifu kutoka madhehebu zote mbili za Shia na Suni ni sawa kabisa na majukumu ambayo Waislamu wanapasa kuyatekeleza kumuhusu Mtume Mtukufu (saw). Hili ni jambo ambalo linahusiana na jukumu la kwanza ambalo ni wajibu wa utiifu mutlaki kwa watukufu hawa na kuwafuata katika masuala yote ya maisha yetu, kama inavyoashiri hili aya tukufu ya 59 ya Surat an-Nisaa na hadithi tukufu ambazo zinaifasiri aya hiyo na zinazohusiana na madhumuni yake. Hivyo wajibu wa pili ni upi? Karibuni tupate kusikiliza na kunufaika kwa pamoja na jibu la swali hili.

 

Ndugu wasikilizaji, ili kufahamu wajibu wa pili katika wajibu wetu kuhusiaa na Maimamu wa Nyuma ya Mtume Muhammad (saw), tunasoma na kuzingatia kwa makini aya ya 83 ya Surat an-Nisaa ambayo inasema: Na inapowajia habari ya amani au ya hofu huitangaza. Na lau wangeirejesha kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wenye kuchunguza katika wao. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngemfuata shetani isipokuwa wachache wenu tu.

Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, aya hii tukufu inaashiria kwamba miongoni mwa wajibu na majukumu ya Umma wa Kiislamu ni kumrejea Mtume Mtukufu (saw) na walio na mamlaka miongoni mwao kuhusu matukio yanayotokea kwenye maisha na zama zao ili wapate kuwatatulia matatizo na changamoto zinazowakabili kwa kutegemea hukumu ya Mwenyezi Mungu wanayoitoa kwenye kitabu cha Qur’ani Tukufu. Na Imethibiti kwa dalili za kiakili, kitafsiri na kihadithi kwamba maana na makusudio ya ‘Ulil Amri’ kama tulivyoona katika vipindi vilivyopita ni Ahlul Beit wa Mtume tu (as).

Uzingatiaji wa aya hii unatufikisha kwenye natija wamba kuwarejea Maimamu watoharifui ndiyo njia ya pekee ya kuweza kutufikisha kwenye maarifa na hukumu sahihi ya Qur’ani Tukufu kuhusiana na matukio ya zama baada ya kuthibiti kwamba kitabu hiki kitakatifu kinabainisha na kufafanua kila jambo katika kila zama. Inabainika wazi pia kutokana na aya hii kwamba kuwarejea Maiamamu wa Ahlul Beit (as) ndiyo njia iliyowekwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuondolewa hitilafu na tofauti zinazozuka baina ya Waislamu na uhasimu unaozuka baina yao. Suala hilo linabainika wazi kwa kuiunganisha aya hii na aya nyingine ya 59 katika Sura hiyohiyo ya an-Nisaa ambayo inasema: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hilo ni bora zaidi na ndilo lenye mwisho mwema.

Hivyo kumrejea Mwenyezi Mungu na Mtume wake kunathibiti kwa kuwarejea wale walio na mamlaka katika Umma wa Kiislamu na ambao wamepewa isma yaani kinga ya kutofanya dhambi na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama inavyobainisha wazi halo aya ya 83 ya Surat a-Nisaa tuliyotangulia kusoma inayosema:………Na lau wangeirejesha kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wenye kuchunguza katika wao. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngemfuata shetani isipokuwa wachache wenu tu.

Hii ina maana kwamba hii ndiyo njia ambayo Mweyezi Mungu aliwaajilia Maimamu watukufu wa Nyumba ya Mtume (saw) ili kutuwezesha sisi tuepuke kumfuata shetani. Na hili ni jambo ambalo linasisitizwa na hadithi nyingi za kuaminika ikiwemo hii ambayo imepokelewa kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) kupitia vyanzo vya Kisuni  kikiwemo kitabu cha Mustadrak al Hakim inayosema: ‘Nyota ni amani kwa walimwengu dhidi ya kughiriki na Ahlu Beit wangu ni amani kwa Umma wangu dhidi ya hitilafu. Hivyo Basi iwapo kabila lolote katika Warabu litawapinga, litahitilafiana na kuwa katika kundi la shetani.’

 

Ndugu wasikilizaji, wajibu na jukumu hili limezungumziwa na kusisitizwa na hadithi nyingi ambazo zimepokelewa na madhehebu yote mawili ya Shia na Suni kutoka kwa Bwana Mtume (saw), zikiwemo zile hadithi zinazozungumzia Maimamu (as) kurithishwa elimu ya Qur’ani na Mtume Mtukufu (saw), hadithi za Safina za wongofu, Thaqalain (Vitu Viwili Vizizto) na hadithi nyinginezo nyingi. Mbali na hadithi hizo kuna hadithi nyingine nyingi tu zinazobainisha wazi kwamba kuwarejea Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) ni kuirejea Qur’ani ambayo inabainisha kila jambo, na ni wazi kuwa si kila mtu aliye na uwezo wa kufikia na kufahamu vyema makusudio ya kila jambo lililomo kwenye kitabu hicho cha mbinguni. Suala hili linatiliwa nguvu na Qur’ani yenyewe ambayo inasema kwamba kwenye kitabu hicho kuna mambo yaliyohifadhiwa humo ambayo si kila mtu anaweza kuyafahamu isipokuwa wale waliotakaswa na kusafishwa kutokana na maovu na madhambi, ambao si wegine bali ni wale waliokusudiwa kwenye aya ya Tat’hir. Qur’ani yenyewe inasema kuwa humo kuna aya ambazo zinahitajia ufafanuazi ambao haufahamiki ila na Mwenyezi Mungu mwenyewe na waliobobea kwenye elimu na ni wale watukufu ambao walipewa elimu yote ya kitabu hicho kitakatifu.

Maulana al-Imam al-Ja’ffar as-Swadiq (as) anasema kama ilivyopokelewa katika kitabu cha al-Mahasin: ‘‘Watu wawili hawahitilafiani katika jambo ila lina asili yake katika kitabu cha Allah, lakini akili za watu hazilifikii.’

Na watu wanaokusudiwa kutokuwa na uwezo wa kulifikia jambo hilo yaani hakika ya Qur’ani, ni watu wasiotakaswa. Watu walio na uwezo wa kudiri na kufikia hakika ya jambo hilo ni wale ambao wamebobea kwenye elimu na ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaridhia kuwa na uwezo wa kuweza kupata hukumu ya Qur’ani katika kila hitilafu ndogo na kubwa, kitabu ambacho kinabainisha kila jambo. Suala hili linawapa sifa ya kuwa marejeo ya kila hitilafu na ugomvi na hivyo kuwa marejeo salama ya Umma wa Muhammad, iwapo utafuata ipaswavyo kauli na amri zao zinazouepusha na hitilafu na ufuasi wa shetani.

 

Kwa maelezo hayo, tunakamilisha kipindi cha juma hili cha Mswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa kusema kwamba wajibu wetu wa pili kwa Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) ni kuwajibika kuwarejea wakati hitilafu zinapotokea miongoni mwetu ili wapate kutupa hukumu sahihi kutokana na mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Qur’ani Tukufu.

Na kufikia hapa ndio tunafikia mwisho wa kipidi hiki kwa juma hili. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.