Dec 06, 2016 10:17 UTC
  • Familia Salama (14)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia Salama. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k.

Kadhia ya kulinda afya ya familia ni kati ya masuala muhimu zaidi katika dunia ya leo. Moja ya njia muafaka ambazo zinaweza kutumika katika kudumisha afya ya familia ni uzingatiwaji wa michezo.

Watafiti wamefikia natija kuwa sababu mojawapo ambazo hupelekea kuibuka magonjwa sugu na yanayosababisha kifo ni kukosekana harakati za kimwili na michezo ya riadha. Harakati za kimwili au mazoezi na michezo hasa riadha huwa na nafasi ya kipekee katika kulinda afya ya kimwili na kiakili.

Michezo anuai mbali na kuzuia magonjwa mengi pia huweza kutibu magonjwa au kupunguza makali ya magonjwa mengi.

Chunguzi mbali mbali zimebaini kuwa, iwapo mwanadamu atafanya mazoezi mepesi ya angalau dakika 30 kwa siku, katika kipindi cha siku tano katika wiki na mazoezi makali ya dakika 20 kwa muda wa siku tatu kila wiki, basi ataweza kupunguza kwa asilimia 8 hatari ya maradhi ya moyo na maradhi mengine.

 

Hali kadhalika wataalamu wanasema iwapo mwanadamu atafanya mazoezi atajiepusha na mauti ya mapema na magonjwa mengine kama vile shinikizo la damu, kisukari au diabetes aina ya pili na aina nyingi za saratani.

Madaktari wanasema moja ya sababu za kuibuka kisukari aina ya pili ni kukosa kufanya mazoezi. Iwapo mwanadamu hafanyi mazoezi basi hukumbwa na matatizo kama vile unene na kwa wale ambao wana historia ya kisukari katika familia, wajawazito na wenye umri wa juu ndio ambao huwa na hatari ya kupata kisukari.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, iwapo kutakuwepo mazoezi ya kawaida kila siku sambamba na chakula kinachofaa na chenye lishe bora pamoja na mapumziko kila mwaka, basi mwanadamu anaweza kupunguza tatizo la shinikizo la damu. Ni kwa msingi huo ndio aghalabu ya  wanamichezo hawakumbwi na matatizo ya shinikizo la damu, kisukari aina ya pili na magonjwa mengine yanayotokana na ukosefu wa kufanya mazoezi.

Kufanya mazoezi hata katika kipindi cha umri wa miaka 60 hadi 80 ni jambo linaloweza kuleta mlingano katika shinikizo la damu mwilini.

Hii ni kwa sababu michezo huimarisha mishipa ya damu na hivyo kuleta mlingano katika shinikizo la damu mwilini. Michezo au mazoezi ambayo yanatiliwa mkazo sana ni kutembea kwa miguu na kupanda mlima.

Hata kwa watu wenye umri wa miaka 60-80 pia wanaweza kuzuia tatizo la shinikizo la damu  kwa kufanya mazoezi hasa kutembea kwa miguu na kupanda milima.

Kufanya michezo au mazoezi yasiyo magumu si tu kuwa huzuia magonjwa kama vile ya moyo, kisukari na shinikizo la damu bali pia hupunguza maumivu ya makumi ya magonjwa mengine mbali mbali. Mazoeozi pia huondoa mgando wa damu katika moyo na hivyo kuzuia hatari ya kuibuka mshtuko wa moyo.

Aidha mazoezi huzuia kujikusanya vipande vya mafuta katika mishipa ya damu katika moyo na maeneo mengine ya mwili na kwa msingi huo kuzuia maradhi mbali mbali ya moyo.

Leo imethibitika kuwa, kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari na hata wale wanaotumia sindano za insulin, iwapo watafanya mazoezi wanaweza kupunguza athari mbaya za ugonjwa huo hatari.

Michezo na mazoezi hupelekea kuimarika mfumo wa kinga mwilini na pia huweza kuzuia baadhi ya saratani.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa wataalamu wa Korea Kusini, kufanya mazoezi ya kawaida kunaweza kuimarisha mfumo wa kinga mwilini na hata kuwasaidia wale ambao wamefanyiwa upasuaji kutokana na saratani ya utumbo.

 

Uchunguzi waliofanyiwa wagonjwa 25 ambao walipasuliwa donda la saratani katika utumbo ulibaini kuwa, utendaji kazi wa kinga mwilini kwa watu ambao walifanya mazoezi sahali siku mbili baada ya upasuaji ulikuwa bora zaidi ya wale ambao hawakufanya mazoezi. Uchunguzi huo ulibaini kuwa, seluli zilizo dhidi ya saratni hushambulia seluli za saratani  katika mwili wa mwenye kufanya mazoezi.

Kwa msingi huo, watafiti walibaini kuwa iwapo mfumo wa kinga mwilini utadhoofika, basi seluli ambazo huibua saratani hupata nguvu. Hivyo ili kuzia tatizo hilo kuna haja ya kufanya mazoezi ili kuimarisha mfumo wa kinga mwilinil.

Mbali na  hayo, mazoezi pia huimarisha mifupa, huondoa sononeko au depression, mafua na pia kupunguza makali ya ugonjwa wa pumu, na husaidia pia ukuaji wa mimba kuwa mzuri kiafya.

Hali kadhalika mazoezi huwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ufahamu. Kwa hivyo hakuna shaka kuwa mazoezi ni moja ya misingi mikuu katika familia salama na kunapaswa kuwepo ratiba maalumu ya kufanya mazoezi katika kila familia.

Wapenzi wasikilizaji, tunafikia tamati hapa katika Makala yetu ya familia salama, usikose kujiunga nasi katika Makala yetu ijayo panapo majaliwa yake Mola. Kwaherini.

 

Tags